Prime
Hii hapa njia ya Simba kubeba ubingwa CAF, RS Berkane ijipange

Muktasari:
- Simba ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Jumapili iliyopita huko Durban, Afrika Kusini baada ya miaka 32 ya kusubiri na sasa itavaana na RS Berkane kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni mafanikio yanayobeba hisia, furaha, matumaini na ari mpya.
KWA muda wa zaidi ya miaka 30, mashabiki wa Simba wamekuwa wakisubiri kwa hamu siku ambayo timu hiyo itaandika historia mpya katika ramani ya soka la Afrika. Hatimaye, siku hiyo imefika.
Simba ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Jumapili iliyopita huko Durban, Afrika Kusini baada ya miaka 32 ya kusubiri na sasa itavaana na RS Berkane kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni mafanikio yanayobeba hisia, furaha, matumaini na ari mpya.
Katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, Simba ambayo ilifuzu kwa ushindi wa bao 1-0 ilionyesha ukomavu kimchezo, kiakili na uimara wa kiufundi. Haikuwa kazi rahisi, lakini Simba ilijipambanua kuwa timu iliyo tayari kupambana kwa ajili ya heshima, taifa na historia.
Sasa ni wakati wa klabu hiyo ya Msimbazi kuelekeza nguvu katika mchezo wa fainali dhidi ya RS Berkane ya Morocco ambapo wataanzia ugenini Machi 17. Yapo mambo mengi ya kutazama ikiwamo njia iliyowafikisha fainali, kauli ya kocha Fadlu Davids, maoni ya wachezaji mara baada ya kufanikisha hilo na hata wapinzani wao.

SAFARI YA FAINALI
Timu hizo mbili zilianzia raundi ya pili ya michuano hiyo Simba ikiing’oa Al Ahli Tripoli ya Libya kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1 huku Berkane wakiishushia mvua ya mabao 7-0 Dadje ya Benin.
Matokeo hayo yalizifanya timu hizo kutinga hatua ya makundi. Simba ilipangwa kundi A na Berkane ikiwa kundi B. Wababe hao kila mmoja alimaliza hatua hiyo akiwa kinara wa kundi lake.
Simba iliongoza kundi A ikiwa na pointi 13 baada ya kushinda mechi nne, sare moja na kupoteza moja. Tofauti na Simba, Berkane yenyewe ilivuna pointi 16 kwa kushinda mechi tano na kutoa sare moja. Wakati Simba ikifunga mabao manane na kuruhusu manne katika hatua ya makundi wapinzani wao, walifunga mabao 12 na kuruhusu bao moja tu, wakitajwa kuwa na safu bora ya ulinzi na ushambuliaji.
Katika hatua ya robo fainali, Simba iliitoa Al Masry kwa mikwaju ya penalti 4-1, baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 2-2, Berkane wao waliitoa ASEC Mimosas kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-0, kila mchezo ikishinda bao 1-0. Upande wa nusu fainali, Simba haikuruhusu bao dhidi ya Stellenbosch na imetinga fainali ikiwa ugenini. Berkane wametinga hatua hiyo kufuatia ushindi wa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya CS Constantine, likiwa ndiyo bao la pili wameruhusu kwenye michuano hiyo msimu huu.
Tangu hatua za awali, Simba imefunga mabao 14 huku ikiruhusu saba kwenye michezo 12. Kwa upande wa Berkane imefunga mabao 25 na kuruhusu mawili ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi na kuruhusu machache.

FEDHA ZA KUTOSHA
Kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC na Berkane zimejihakikishia kitita cha dola milioni moja za Kimarekani (takriban shilingi 2.6 bilioni za Kitanzania) kutoka CAF.
Hili ni ongezeko kubwa la mapato ambayo klabu inaweza kuyatumia kwa maendeleo zaidi ya ndani kama vile kuimarisha kikosi, kuboresha miundombinu, au kuimarisha utawala.
Aidha, endapo Simba watafanikiwa kushinda taji hilo, watavuna zaidi ya mara mbili ya kiwango hicho zaidi ya dola 2milioni, ambazo ni takriban shilingi 5.2 bilioni za Kitanzania.
Mkwanja huo unaonyesha wazi kwamba Simba si tu wanapigania heshima ya soka la Tanzania, bali pia wanatengeneza msingi wa kifedha unaoweza kuipeleka klabu hiyo kwenye ngazi nyingine zaidi barani Afrika.
UMRI
Kikosi cha Simba kina wastani wa umri wa miaka 25, huku Berkane ikiwa ni wastani wa miaka 27.
HAWA NDIO RS BERKANE
Katika fainali, Simba watakutana na RS Berkane ya Morocco iliyobobea katika mashindano hayo.
RS Berkane ni mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika, wakilitwaa mara mbili (2019/20 na 2021/22), na ni timu inayojulikana kwa nidhamu ya kiufundi, uzoefu mkubwa, na wachezaji wenye ubora wa juu.
RS Berkane wanacheza soka la kujilinda vyema na pia kushambulia kwa kasi. Wana wachezaji mahiri kama Youssef El Fahli na Adil Tahif ambao ni hatari katika mashambulizi ya kushtukiza. Ni timu yenye uzoefu mkubwa wa mechi za fainali, jambo ambalo linawafanya kuwa wapinzani hatari kwa Simba. Hata hivyo, Simba wameonyesha kuwa na uwezo wa kukabiliana na presha kubwa. Kwa maandalizi sahihi, mbinu na morali kubwa, Simba wana nafasi nzuri ya kupindua meza dhidi ya mabingwa hawa wa Morocco kwa kuwa mchezo wa mwisho wa fainali unapigwa Kwa Mkapa sehemu ambayo imekuwa mhimili mzuri zaidi kwa Simba.

MAANDALIZI YAANZA
Kocha wa Simba, Fadlu Davids, alitoa kauli ya busara mara tu baada ya mchezo dhidi ya Stellenbosch. Akionekana mtulivu licha ya furaha ya mafanikio, Fadlu alikumbusha kwamba hatua ya kutinga fainali si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa changamoto kubwa zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo, Fadlu anasema: “Sasa si wakati wa kusherehekea. Tumefanikisha kutinga fainali, lakini kazi kubwa bado iko mbele yetu. Tutasherehekea baada ya kuchukua ubingwa.”
Kauli hii inaonyesha aina ya falsafa ambayo Fadlu ameileta Simba falsafa ya ukomavu wa kisaikolojia na kuepuka kuridhika mapema. Katika historia ya soka, timu nyingi zimewahi kufika hatua za mwisho, lakini kushindwa kutokana na kulewa mafanikio mapema. Fadlu anaonekana kuelewa hilo vyema na anataka Simba ibaki na njaa ya ushindi hadi mwisho.
Fadlu ameweka wazi pia kuwa maandalizi ya fainali yameanza mara moja. Hakuna muda wa kupoteza. Kila mchezaji, kila mfanyakazi wa benchi la ufundi, kila mtu ndani ya klabu anahitajika kuweka akili na nguvu zote kuelekea fainali hiyo muhimu.

HISIA ZA WACHEZAJI
Ndani ya Uwanja wa Stellenbosch baada ya kipenga cha mwisho kulisikika nderemo na vifijo kutoka kwa wachezaji wa Simba. Hata hivyo, walijua kwamba walikuwa wamepiga hatua moja tu kuelekea lengo kubwa.
Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, alieleza hisia zake kwa maneno ya hisia kuu: “Hii ni ndoto ya kila mchezaji kuifikisha timu yake kwenye fainali kubwa kama hii. Lakini hatutaki kuishia hapa. Tunataka taji, kwa ajili yetu, kwa ajili ya mashabiki wetu, kwa ajili ya Tanzania.”
Katika mahojiano mengine, Elie Mpanzu alisema kuwa walijipanga vilivyo kwa mchezo huo na waliamini kuwa wanaweza kufika mbali. Mpanzu alisisitiza kuwa wanatambua ukubwa wa nafasi waliyoipata na watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanawapa mashabiki wa Simba sababu ya kufurahia zaidi.
Shomary Kapombe, mmoja wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa Simba, alisema mafanikio hayo ni ushahidi wa bidii kwa misimu mingi. “Tumekuwa tukipambana kwa miaka mingi. Sasa hatimaye tumefika. Sasa tunahitaji umoja zaidi, juhudi zaidi, nidhamu zaidi,” anasema.
Fabrice Ngoma, kiungo wa kimataifa kutoka DR Congo, anasema: “Hii ni hadithi ya kujivunia. Simba ni familia kubwa. Naamini tunaweza kutwaa ubingwa huu, huu ni wakati wetu kuionyesha Afrika.”

WASAUZI WAIPA NAFASI SIMBA
Baada ya kipigo, baadhi ya mastaa wa Stellenbosch hawakusita kuongelea ubora wa wapinzani wao.
Kiungo Andre de Jong, alikiri kwamba wameumizwa sana na matokeo hayo lakini akaonyesha heshima kubwa kwa Simba.
“Simba walicheza kama timu kubwa. Walituonyesha tofauti ya uzoefu wa mashindano haya makubwa. Tunawapongeza,” anasema.
Kwa upande wake, Devin Titus anasema Simba ina kikosi bora ambacho kinaweza kupigania ubingwa.
“Wanajua walichokuwa wanakifanya. Walitumia kila nafasi vizuri. Wanastahili kuwa kwenye fainali.”
Naye Brian Mandela, beki wa kati wa Stellenbosch licha ya machungu ya kutolewa, anasema anaamini Simba ina nafasi nzuri ya kutwaa taji.
“Kwa maonyesho yao dhidi yetu, naamini Simba wana uwezo wa kuwa mabingwa. Wana wachezaji wakomavu, benchi la ufundi madhubuti, na morali nzuri.”