Prime
Dabi ya Machi 8 Simba 1, Yanga 1

Muktasari:
- Timu hizo ambazo ni watani wa jadi zinatarajiwa kuvaana wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika pambano la Ligi Kuu Bara baada ya awali kukutana Oktoba 19 mwaka jana na Yanga kushinda kwa bao 1-0.
MASHABIKI wa soka hususani wa Simba na Yanga kwa sasa wanahesabu siku tu, kabla ya kuzishuhudia timu hizo zikishuka uwanjani katika pambano la marudiano la Dabi ya Kariakoo.
Timu hizo ambazo ni watani wa jadi zinatarajiwa kuvaana wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika pambano la Ligi Kuu Bara baada ya awali kukutana Oktoba 19 mwaka jana na Yanga kushinda kwa bao 1-0.
Katika mchezo huo wa kwanza Simba ijikiweka yenyewe baada ya beki wa pembeni, Kelvin Kijili kujifunga katika harakati za kuokoa mpira langoni mwake.
Jumamosi hii, timu hizo zitakutana tena, likiwa ni pambano la 114 kwa timu hizo katika ligi tangu mwaka 1965, huku likiwa ni la tatu ndani ya Machi 8, lakini ni la 11 kukutana katika ndani ya Machi ikiwamo 10 za Ligi Kuu na moja la michuano ya Kombe la Tusker (haipo kwa sasa).
Pambano hilo la Machi 8 litakuwa ni la tatu kwa timu hizo kukutana katika tarehe kama hiyo, kwani tayari zilishakutana mara mbili, ya kwanza ikiwa ni mwaka 2015 na mara ya mwisho 2020.

Rekodi zinaonyesha timu hizo katika pambano la Machi 8 ambayo ni Siku ya Wanawake Duniani, hakuna aliye mbabe kwani kila moja imeshinda mchezo mmoja na kupoteza mwingine.
Simba ndio walioanza kushinda ndani ya Machi 8 zilipokutana 2015 na mshambuliaji kutoka Uganda, Emmanuel Okwi alifanya yake kwa kumtungua kipa Ally Mustafa 'Barthez' kwa shuti kali la mbali la dakika ya 52 lililoipa Simba ushindi.
Okwi alipiga shuti hilo la umbali wa mita 22 baada ya kupokea pasi tamu kutoka kwa Said Ndemla na kumchungulia Barthez alipo na kuachia fataki hilo lililojaa wavuni.
Timu hizo zilisubiri kwa miaka mitano baadae kabla ya kukutana tena katika tarehe kama hiyo, yaani Machi 8, 2020 na safari hii Yanga ilijibu mapigo kwa kupata ushindi wa bao 1-0, lililowekwa kimiani na Bernard Morrison 'BM33'.
Kiungo mshambuliaji huyo raia wa Ghana ambaye kwa sasa anakipiga KenGold, alifunga bao hilo sekunde chache kabla ya mapumziko, akimtungua kipa Aishi Manula kwa mkwaju wa friikikii, iliyotokana na Jonas Mkude kumchezea madhambi BM33.

Hivyo mechi ya wikiendi hii ni ya kusaka mbabe wa Machi 8 baina yao, kwani timu hizo zitakutana kwa mara ya tatu, huku zikiwa katika mbio za kuwania ubingwa, Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 58, huku Simba ikifuata na pointi 54.
Ukiachana na mechi ya Machi 8, kwa rekodi za jumla kwa mwezi wa tatu, Yanga ndio wababe mbele ya Simba, kwani imeshinda michezo minne kati ya 10 ya Ligi Kuu tangu zilipoanza kukutana katika mwezi huo kuanzia mwaka 1968.
Simba yenyewe imeshinda mara moja tu katika mechi za Ligi Kuu, lakini ina ushindi mwingine wa fainali ya Kombe la Tusker na Yanga ililala kwa mabao 4-1 na kuibuka vurugu kubwa mbele ya aliyekuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia mwanzoni mwa mwaka jana.
Mechi nyingine tano baina ya timu hizo zilipokutana Machi, zimeisha kwa sare tofauti huku, Yanga ikivuna mabao mengi zaidi ya watani wao, kwani katika mechi 10 za ligi za mwezi huo imevuna mabao tisa, wakati Simba imefunga matano tu.

Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza Machi 30, 1968 na Yanga kushinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Kitwana Manara 'Popat' kabla ya kuja kukutana tena Machi 3, 1969 likiwa ni pambano la pili katika mwezi huo.
Mchezo huo haukumalizika baada ya Simba kuugomea na Yanga kupewa ushindi wa mezani wa pointi mbili na mabao mawili na timu hizo zilikaa hadi mwaka 1984 zilipokutana kwa mara ya tatu mwezi Machi.
Pambano hilo la ligi, lilichezwa Machi 10 na liliisha kwa sare ya bao 1-1, Simba ikitangulia kwa bao la penalti iliyopigwa na kipa, Idd Pazi 'Father' aliyekuwa kipa wa kwanza kufunga katika Dabi ya Kariakoo kabla ya Juma Kaseja kuja kuilipa Mei 6, 2012 wakati Simba ikiizima Yanga kwa mabao 5-0. Bao la kusawazisha la Yanga katika mechi hiyo ya Machi 10, 1984 liliwekwa wavuni na Omar Hussein 'Keegan' dakika ya 72 na kuiepushia Yanga kipigo katika mwezi Machi.
Miaka miwili baadae timu hizo zilikutana tena Machi, mchezo ukipigwa Machi 15, 1986 na kuisha pia kwa sare ya 1-1, Simba ikitangulia kwa bao la John Hassan Douglas dakika ya 20 na Abeid Mziba 'Tekero' akaichomolea Yanga dakika ya 44.

Mwaka 1993, ikiwa ni miaka saba tangu zilipokutana kwa mara ya mwisho, Yanga iliibuka tena kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Machi 27, mabao yote mawili ya Yanga yakifungwa na Said Mwamba 'Kizota' dakika ta 47 na 57 kabla ya Edward Chumila 'Eddo Boy' kufunga la kufutia macho la Simba dk ya 75.
Simba na Yanga zilikutana tena Machi 18, 1995 na Machi 26, 2006 na mara zote zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu mara zote mbili kisha Machi 5, 2011 timu hizi zilikutana tena katika mchezo wa Ligi Kuu na kutoka sare ya 1-1.
Hii ndio mechi ndio iliyotajwa kuzindua mfumo wa VAR, kwani Yanga ilitangulia kwa bao la dakika ya 59 kupitia beki wa kushoto, Stephano Mwasyika kisha Mussa Hassan Mgosi aliichomolea Simba dakika ya 73 kwa kichwa mpira uliogonga besela na kudondokea ndani, lakini bado lilikataliwa na mwamuzi, Oden Mbaga.

Wachezaji wa Simba na mashabiki walilalamikia uamuzi wa Mbaga na kumtaka aangalie marejeo kupitia televisheni iliyopo uwanjani na kubaini ni kweli mpira uligongea ndani kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga na kulikubali bao hilo la Mgosi na kufanya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.
Mechi ya tisa kwa timu hizo kukutana Machi, ilikuwa Siku ya Wanawake Duniani, yaani Machi 8 2015 likiwa la kwanza kwao kukutana katika siku kama hiyo na Okwi alifunga bao kali la mbali, kabla ya Yanga kujibu Machi 8, 2020 kwa bao la Morrison.
Pambano pekee la Machi lililo la Ligi Kuu ni lile la fainali ya Kombe la Tusker iliyopigwa Machi 31, 2002 na Yanga kulala kwa mabao 4-1, yaliyofungwa na Mkenya Mark Sirengo dk. 3 na 76, Madaraka Selemani dk. 32 na Emmanuel Gabriel dk. 83, huku Sekilojo Chambua akifunga bao la kufutia machozi la Yanga dk 16.
Mechi hii nusura ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao la tatu likitokana na kuutengeza kwa mkono kabla ua kumtungia kipa Peter Manyika.
Kw ujumla katika mechi zote 11 za mashindano tofauti ndani ya Machi ikiwamo ile ya Kombe la Tusker, bado Yanga ina mabao mengi ikiwa na 10 dhidi ya tisa ya Simba, kuonyesha Vijana wa Jangwani ina kismati na mwezi huo. Usilolijua ni kwamba katika mechi hizo 11, Simba na Yanga zimekutana mara saba katika siku za Jumamosi, huku siku hiyo ikiibeba Yanga zaidi. Pia zimekutana mara tatu siku za Jumapili na siku hizo zimekuwa na kismati zaidi kwa Simba na mara moja tu zimekutana Jumatatu na Simba iliingia mtini na kuipa Yanga ushindi wa mezani.
Hata hivyo, kwa aina ya vikosi na makocha ilizonazo timu hizo ni wazi Jumamosi kutakuwa na kazi kubwa katika vita ya kuwania pointi tatu za mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaoanza kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin.

Timu hizo zinakutana kila moja ikitoka kushinda mabao 3-0 ugenini, Yanga ikitoka kuifyatua Pamba Jiji, jijini Mwanza huku Simba ikitoka kuinyoosha Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Presha imekuwa kubwa kwa wachezaji wa timu hizo mbili, kwa kutambua timu yoyoye itakayopangusha pointi Kwa Mkapa itatoa nafasi kwa mpizani kujiweka pazuri katika mbio za ubingwa kwa msimu huu.
Tayari wachezaji kama Ellie Mpanzu ambaye hii itakuwa ni dabi ya Kariakoo ya kwanza tangu asajiliwe ameshaiomba, lakini kuna nyota wengine wa timu hizo wamekuwa wakiipigia hesabu kwa kutambua kufanya vyema katioka mchezo huo ni kujiwekea alama na heshima kubwa kwa mashabiki.
Na hata makocha wa timu hizo, walishanukuliwa mapema walikuwa wakimalizia mechi zao za mikoani dhidi ya Pamba na Coastal Union, ili kuja kuanza kazi ya kujipanga na mchezo huo wa Dabi ya Kariakoo ambao umeshikilia hatma ya ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Fadlu Davids anayeinoa Simba hiyo ni Dabi ya Kariakoo ya tatu kwa msimu huu baada ya awali kucheza nusu fainali ya Ngao ya Jamii na kulala 1-0 kwa bao la Maxi Nzengeli, kisha kupasuka tena 1-0 katika duru la kwanza la Ligi, tofauti na Miloud Hamdi wa Yanga, hili ni dabi yake ya kwanza nchini.
Nani atakayeibuka na ushindi katika mechi hiyo ya 114 za watani katika Ligi Kuu Bara na nani atakayemaliza ubishi wa Machi 8 kwani ngoma hadi sasa inasoma Simba 1, Yanga 1. Ngoja tuone!
MECHI ZA MACHI
1) Mar 30, 1968 (Jumamosi)
Yanga 1-0 Sunderland
MFUNGAJI: Kitwana Manara dk. 28.
2) Mar 3, 1969 (Jumatatu)
Yanga v Sunderland
(Yanga ilipewa pointi za chee na ushindi wa mabao 2-0, baada ya Sunderland kugoma kuingia uwanjani).
3) Mar 10, 1984 (Jumamosi)
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Omar Hussein dk. 72.
Simba: Idd Pazi kwa penalti dk 20.
4) Mar 15, 1986 (Jumamosi)
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Abeid Mziba dk. 44
Simba: John Hassan Douglas dk. 20.
5) Mar 27, 1993 (Jumamosi)
Yanga 2-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Said Mwamba Kizota dk. 47 na 57
Simba: Edward Chumila dk. 75.
6) Mar 18, 1995 (Jumamosi)
Simba 0-0 Yanga
7) Mar 26, 2006 (Jumapili)
Simba 0-0 Yanga.
8) Mar 5, 2011 (Jumamosi)
Simba 1-1 Yanga
WAFUNGAJI:
YANGA: Stefano Mwasyika (penalti) dk 59.
SIMBA: Mussa Mgosi dk 73.
(Refa Oden Mbaga alizua tafrani uwanjani, kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya kujadiliana na msaidia wake namba moja).
9) Mar 8, 2015 (Jumapili)
Simba 1-0 Yanga
MFUNGAJI: Emmanuel Okwi Dk 52
10) Mar 08, 2020 (Jumamosi)
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Bernard Morrison 44'
11) Mar 31, 2002 (Jumapili)
Simba Vs Yanga 4-1
WAFUNGAJI:
SIMBA: Mark Sirengo dk 3 na 76, Madaraka Selemani dk 32 na Emmanuel Gabriel dk. 83.
YANGA: Sekilojo Chambua dk 16.
Msimamo mechi za watani tangu 1965-2024
P W D L F A PTS
YANGA 113 41 40 32 121 105 163
SIMBA 113 32 40 41 105 121 136