Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa nini Tshabalala tajiri? Mwamba huyu anahusika!

SHABA Pict
SHABA Pict

Muktasari:

  • Mastaa wanaosimamiwa na meneja Carlos Sylvester  ‘Mastermind’ kutoka Simba na Yanga wamekuwa na thamani inapofika wakati wa usajili na pia wana  maendeleo ya kimaisha kuwawezesha kujiandaa baada ya kustaafu uwanjani.

KUNA kitu nyuma ya pazia kuhusiana na mastaa wanaopiga pesa ndefu kutoka Simba na Yanga. Lakini, yupo pia mtu anayejua kusuka mipango ya namna wachezaji hao kupandisha thamani zao na kuwafanya kuwa muhimu katika timu zilizowaajili.

Mastaa wanaosimamiwa na meneja Carlos Sylvester  ‘Mastermind’ kutoka Simba na Yanga wamekuwa na thamani inapofika wakati wa usajili na pia wana  maendeleo ya kimaisha kuwawezesha kujiandaa baada ya kustaafu uwanjani.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na meneja huyo ambaye pia jambo muhimu analofanya kwao ni kutowategemea kiuchumi ili kujipatia kipato kutoka katika dili zao, bali ana biashara zake ambazo wakati mwingine anawasaidia.

“Mameneja wengi wanakimbiwa na wachezaji kwa sababu wanataka kugawana pesa kati kwa kati, wanasahau kwamba wengi wao wanatoka familia za kimaskini, hivyo wanapomaliza pesa za usajili wanabakia hawana kitu,” anasema Carlos na kuongeza:

“Siwezi kukataa kwamba sipati chochote, ila nachukua kidogo na kuhakikisha nawashauri wafanye maendeleo ya maisha yao. Pia nafuatilia kile wanachofanya uwanjani na kuzungumza nao mara kwa mara. Kwangu nachukulia kama nawasaidia na siyo kuchuma pesa kupitia jasho lao.”

SHAB 05

TSHABALALA TAJIRI

Ni nadra wachezaji wa ndani kutoka kupata mapumziko baada ya ligi kwisha, lakini hilo kwa nyota wa Ligi Kuu limekuwa likifanywa na wale wa kigeni ambao huenda sehemu mbalimbali kama Zanzibar au Arusha, kama alivyowahi kufanya Clatous Chama na Keneddy Musonda, lakini kwa Tshabalala sio zake kama anavyothibitisha meneja wake.

“Tshabalala ni tajiri. Ni wale wachezaji ambao wakitaka kwenda sehemu fulani muda huohuo wanakata tiketi na kwenda wanapotakiwa kwenda bila kujali gharama gani anatoa. Namfurahia kwa hilo ni tofauti na wachezaji wengine,” anasema.

“Unajua hii sasa ni maisha binafsi wachezaji 10 hadi 12 hawawezi kuwa sawa, mfano Bakari Mwamnyeto akiona mapumziko tu anataka kwenda Tanga kufurahi na wazazi wake hivyo hivyo kwa Zawadi Mauya na yeye pia ni Morogoro na Dar es Salaam.”

Anasema Tshabalala linapokuja suala la mapumziko ni mtu wa familia akiwa na mtoto wake, mke yeye yupo tayari kwenda popote shida iliyopo ni ratiba inambana kwasababu wa kipa nafasi ya kumpumzika wanakutana na ratiba ya kujiunga na kambi ya timu ya taifa.

“Taifa Stars inamkwamisha kwenye mambo mengi, nafikiri angekuwa amesafiri nchi nyingi sana hadi sasa, lakini kuna utaratibu fulani ligi ikiisha watu wanahitajika kambini,” anasema Carlos.

“Mimi namsifu kwa sababu nilikuwa namuuliza zamani kwa nini Pogba (Paul aliyekuwa kiungo wa Manchester United na Juventus) akipata mapumziko anakwenda Dubai wewe kwa nini huwezi, shida ni nauli au ni nini, akasema ni uamuzi tu hivyo sasa anaamua tu kutoka.

“Maisha anayoyaishi Tshabalala nje ya ubora wake uwanjani pia anajiweka kwenye nafasi nzuri ya kujiweka kwenye soko kwa thamani, kwani akionekana kwa ukubwa nje ya uwanja anajipa thamani nyingine kubwa ambayo inamfanya aonekane kuwa na thamani ya juu.’’

SHAB 04

MTU POA

Tshabalala ukimuona tu utamtafsiri kwa upole kutokana na namna alivyo akiwa hana mambo mengi na ni mtu wa vitendo hasa anapokuwa uwanjani na kitambaa chake cha unahodha mkononi.

Carlos anasema: “Nafikiri hata viongozi wa Simba walizingatia hilo (la kumpa unahodha), lakini ni mchezaji pale unapopigwa muziki hauwezi ukamkuta amekaa.

“Tshabalala sina hakika kuna mtu anamfahamu vizuri. Mnavyomuona anacheza mchangamfu sio huyo ni kijana mmoja mstaarabu mpole, sio muongeaji, mpole sana, mnaweza mkakaa bila kuongeleshana hata mwezi usipomtafuta. Ni mnyenyekevu anaweza akapitia magumu na asiseme.

“Pia ni mtu wa watu sina hakika kama kuna mtu anaweza kujitokeza hapa akasema amekosewa na Zimbwe, hata uwanjani hana tabia za kufanya fujo au kafanyiwa kitu kibaya akarudishia.

“Kwenye masuala ya kunifurahisha sina siku alinikwaza kwa sababu kazi yake anayoifanya uwanjani tu kwangu nafurahia kwa sababu anacheza kwa ubora... ananifurahisha kumtazama.”

Carlos anasema sio Tshabalala pekee kwenye kikosi chake mwenye nidhamu ya unyenyekevu, pia anamtaja  Mwamnyeto ambaye vilevile ni nahodha wa Yanga kuwa sio muongeaji sana, lakini ni msikivu.

SHAB 03

MALENGO KWA WACHEZAJI

Kama unajiuliza kwanini Tshabalala anapambana kupanda na kushuka kuzuia uwanjani hupati jibu, basi Mwanaspoti linakufahamisha kwa nini anafanya hivyo kupitia kwa meneja wake, Carlos anayewaelezea wachezaji wake wote.

“Wachezaji wangu kulingana na nafasi huwa tunakaa na kila mmoja anaandika malengo ya msimu na kufanya makubaliano kwa maandishi, na kila anayeshindwa kufikia huwa anahama nayo mwezi unaofuata... naamini kwenye utendaji kazi mzuri ni kuwekeana makubaliano,” anasema.

“Mfano Tshabalala malengo yake mara nyingi ni kufunga mabao mawili kwenye ligi kwa msimu, asisti kuanzia tano na kuendelea kimataifa, kufunga bao moja kimataifa na kutoa pasi za mwisho kuanzia tatu na kuendelea... msimu huu amefikisha kimataifa.”

Anasema ofisini kwake ni mchezaji mmoja baada ya mwingine anaingia kwenye makubaliano hayo na kila mmoja ana malengo yake na hii ni kwa ajili ya kuwapa nguvu na morali wapambane na kujiweka kwenye utofauti na wachezaji wengine na hilo limekuwa likiwasaidia.

SHAB 02

MAISHA BAADA YA SOKA

Wachezaji wengi bora waliokuwa na majina makubwa miaka ya nyuma walipokuwa wanacheza si wote wamekuwa bora kwenye kipato, kwani kuna baadhi yao wamegeuka ombaomba, na kutokana na hilo Carlos anaeleza wanavyowaandaa wachezaji kimaisha baada ya kustaafu mpira.

“Sisi kwenye kampuni yetu tuna mtaalamu ambaye anawaandaa wachezaji wetu kisaikolojia, Gideon (anamtaja kwa jina moja). Amekuwa akitusaidia sana kuwajenga kisaikolojia, changamoto inapotokea, lakini pia maisha ya baadaye kuishi bila kucheza mpira.

“Uzuri na mimi ni mtu wa biashara, hivyo huwa nakaa nao na kuwaeleza masuala ya biashara, lakini naamini maisha yao hayatakiwi kujengwa baada ya kustaafu wanatakiwa kujitengeneza sasa kwa kuwekeza kwenye maisha baada ya mpira.”

Anasema kwa namna anavyowaangalia wachezaji wake haoni kama kuna mtu ana ndoto za kuwa kocha anawatazama kwa namna nyingine na ndoto yake kubwa ni kuona wanakuwa na mitaa ya nyumba, kampuni au maduka makubwa ya biashara.

“Kesho na keshokutwa mtashangaa mmoja anaweka udhamini wake kwenye timu za Simba au Yanga au unakutana na Zimbwe Mall. Hili linawezekana kutokana na akili ya wachezaji wangu wengi na nimekuwa nikiwajenga kwenye mambo makubwa kama hayo.”

SHAB 01

FAIDA ZA MAPUMZIKO

Licha ya wachezaji kupata mapumziko mara baada ya ligi kumalizana na msimu soka ni wachache wanaotoka nje ya Tanzania kama ilivyo kwa mastaa kibao wa Ulaya ambao wamekuwa wakizunguka mataifa mbalimbali na Carlos amezungumzia faida za kufanya hivyo.

“Mchezaji anapopata nafasi ya kutoka na kwenda mbali zaidi ya mazingira aliyoyazoea kuna faida tatu anatengeneza - kutengeneza nguvu mpya, kupunguza shida za msimu mzima, kupumzisha mwili na kutoka kwenye mazingira yaliyo na maumivu kwake,” anasema

“Unatoka Tabora unakuja Dar es Salaam, lazima utakumbuka mazingira yenye maumivu na wewe kama Uwanja wa Mkapa, KMC, hivyo bado utakuwa unarudisha mawazo ya kimchezo, lakini kutoka mbali zaidi hasa mazingira ambayo hujayazoea unasahau shida zote... hii ni faida kubwa.”

Carlos anasema ndio maana mastaa wakubwa kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakitoka nchini mwao na kwenda nchi nyingine za mbali kukutana na mazingira tofauti na waliyozoea, na kuhoji kwanini wachezaji wetu wa ndani wanashindwa kufanya hivyo.


KIBU NORWAY

Mwanaspoti liliwahi kuripoti sintofahamu ya mshambuliaji Kibu Denis kutoroka na kwenda Norway, huku waajiri wake, Simba, wakiwa hawana taarifa na taharuki ilitanda mchezaji huyo akitajwa kila kona kuwa alikwenda kufanya majaribio katika timu moja.

Sakata hilo lilimalizika baada ya Kibu kurejea nchini, lakini hapakuwa na ufafanuzi rasmi, ila wakala wa mchezaji huyo amefunguka ilivyokuwa.

Anasema mchezaji wake alipata ofa kwenda kufanya majaribio nchini humo akiwa tayari amesaini mkataba wa kuitumikia Simba, hivyo kutokana na matamanio ya staa huyo kucheza nje ya Tanzania alifanya jitihada za kwenda kujaribu bahati yake.

“Kocha wakati anamhitaji Kibu timu ilikuwa kwenye hatua mbaya, ni kama dili ilikufa, lakini mtendaji mkuu baada ya kumuajiri kocha mwingine walimuonyesha video vya Kibu pia alivutiwa na ubora wa Kibu ambaye alipigiwa simu moja kwa moja akiwa Marekani,” anasema Carlos.

“Akiwa huko alinipigia simu saa nane usiku akaniambia amepigiwa simu na kocha wa Kristiansund (timu ya Noway) kwamba wananihitaji, nikamjibu sasa mimi nalala tutaongea kesho, lakini hakutaka kukubali kwa sababu ndoto yake ilikuwa kucheza nje na hapo tayari tulikuwa tumesaini mkataba na Simba ambao alivuka vipengele vyote vya mchezaji wa ndani. Unapata picha nawaanzaje Simba na mkataba ulikuwa bado haujaanza kutumika.”

Anasema alizungumza na mchezaji arudi Tanzania na kwenda kwenye kambi ya maandalizi na kama mambo yatakwenda vizuri ataondoka akitokea huko, nashukuru alikubali na akafanya hivyo, lakini presha ya timu iliyokuwa inamtaka haikuwa ya kawaida ikazidi kumchanganya Kibu.

“Unajua baada ya simu nyingi alichanganyikiwa akawa anawasiliana zaidi na ndugu zake, huku akinisahau mimi kama meneja. Lakini nilimuahidi kuwa nitampa ushirikiano hata shida ikitokea sitamuacha. Timu hiyo ilituma tiketi ya kwenda na kurudi.

“(Lakini) Kibu kutokana na ukubwa wa Simba akahofia kutoa taarifa, akaondoka na ndipo taarifa za mchezaji kutoroka zilitoka... hapo mchezaji alikuwa Addis Ababa (Ethiopia), alimpigia Crescentius Magori ambaye alimtaka arudi akimhakikishia tiketi ya kurudi haraka,” anasema na kuongeza:

“Baada ya kuongea na kiongozi wake na kumuambia kuwa amefika Addis Ababa anaomba kufika Norway, akaendelea na safari lakini mara baada ya kufika huko alikutana na taarifa kwamba wamepigiwa simu yeye ni mchezaji wa Simba na kama watampa nafasi hata ya kufanya mazoezi watashtakiwa, lakini alichoambulia ni kupokelewa na kufikishwa uwanja wa mazoezi.”

Anasema Kibu alimwambia kuwa endapo atapata nafasi ya kufanya mazoezi, basi hawezi kurudi kwani ndoto yake ni kucheza Ulaya hawezi kufeli zaidi. Aliishia kukanyaga uwanja, kuonyeshwa mafanikio ya timu hiyo bila kugusa mpira kwani viongozi wa Simba waliionya Kristiansund juu ya kumtumia mchezaji huyo.

“Hivyo Kibu alikaa hotelini siku nne huku uongozi wa Kristiansund ukimsisitiza kuwa hadi hapo Simba watakapokubali kufanya mazungumzo nao au kuwapa ruhusa ya kufanya mazoezi, lakini walikataa kuwa hawawezi kukubali aguse uwanja.

Carlos anasema baada ya hilo timu hiyo iliwaambia kuwa hawatamfanyisha mazoezi, bali wapo tayari kumununua, hivyo Simba watume ofa.

“Simba waliwapa ofa ya bilioni 2.6, uongozi ukasema samahani hatuwezi tukafanya biashara kama hiyo. Mimi kama meneja nikajiongeza kwa kuwaomba Simba turudishe fedha aliyosajiliwa mchezaji na kila kitu alichopewa na kuongeza fedha ili mchezaji aweze kuondoka, bado Simba walikataa,” anasema.

Anasema Kibu alikuwa kwenye changamoto mbaya kama kifaranga aliyefiwa na baba na mama, halafu mvua inanyesha analia asubuhi, mchana na usiku, hivyo hakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kumshauri arudi kitu ambacho hata Serikali iliingilia sakata hilo wakimtaka mchezaji arejee nchini.

USIKOSE SEHEMU YA PILI KESHO