Prime
NIONAVYO: Soka limemsahau Abramovic?

Muktasari:
- Ni rahisi sana kwa mtu kumkumbuka Sir Alex Ferguson na David Beckham kwa walichokifanya pale Manchester United katika miaka ya 1990 na 2000, lakini ukiwauliza watu wapi ilitoka fedha ya kuiwezesha Manchester United hutapata jibu.
ULIMWENGU wa michezo unasahau haraka sana. Huwasahau haraka wadau wake na hasa wale walioweka rekodi katika kutenda shughuli za kuonekana kila siku kama watawala na wawekezaji.
Ni rahisi sana kwa mtu kumkumbuka Sir Alex Ferguson na David Beckham kwa walichokifanya pale Manchester United katika miaka ya 1990 na 2000, lakini ukiwauliza watu wapi ilitoka fedha ya kuiwezesha Manchester United hutapata jibu.
Mafanikio yoyote katika michezo, hasa katika ulimwengu wa sasa hayaji bila fedha. Wanamichezo na klabu zilizofanikiwa kuanzia katika michezo ya mtu mmoja kama tenisi, ndondi na riadha hadi michezo ya timu kama mpira wa kikapu, soka na raga wameweza kufanya hivyo kwa kiasi kikubwa kutokana na msukumo wa kifedha pamoja na uwepo wa vipaji.
Leo utasikia watu wanaiongelea Simba iliyoitwa ‘taifa kubwa’ au Yanga iliyoitwa ‘Umoja wa Mataifa’ na watawataja wachezaji maarufu wa enzi hizo na makocha maarufu wa wakati huo, lakini mara chache utasikia wanatajwa Azim Dewji na Abbas Gulamali ambao kazi yao ilinogesha mpira hasa miaka ya tisini.
Hata matajiri na kampuni zilizopo sasa watasikika kiasi na watasahaulika muda si mrefu wanapoacha kujihusisha na klabu husika.
Kwa kipindi cha miaka karibu 20 iliyopita ilikuwa ni vigumu kutaja soka la England hususan Ligi Kuu (EPL) bila kumtaja tajiri Roman Abramovic na klabu ya Chelsea FC ya jijini London. Chelsea ilipata nguvu baada ya kununuliwa na Roman kiasi cha kuua ubabe au ushindani uliokuwepo kati ya Arsenal ya London na Mancheser United ya Manchester, Kaskazini mwa England.

Ni ufufuko wa Manchester City baada ya kupata uwekezaji kutoka Mashariki ya mbali na Ghuba ya Arabuni ndiyo kwa kiasi fulani ulitishia utawala wa Chelsea. Katika kipindi hicho, Chelsea na Roman Abramovic walishinda mataji matano ya EPL na mawili ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya.
Abramovic aliinunua Chelsea ikiwa hoi bin taaban kifedha. Miradi yake kama Chelsea Village na Uwanja wa Stamford Bridge ilikuwa inaenda kusambaratika. Nafasi ya pili waliyoipata katika msimu wa 2023/24 na tiketi yake ya kucheza Ligi ya Mabingwa zilikuwa ndizo aseti za uhakika kwa timu hiyo iliyokuwa chini ya kocha mtaliano Claudio Ranieri na Mwenyekiti Ken Bates.
Bates ambaye aliipata Chelsea iliyo mufilisi kwa Paundi moja ya kugongewa muhuri wa serikali (kama Sh3500) inasemekana aliiuza timu hiyo kwa Roman na kupata kiasi kisichopungua Pauni 17 milioni katika akaunti yake.
Kwa jumla ilimgharimu Abramovic kiasi cha Pauni milioni 150 ikiwa ni gharama za kununua timu na kulipa madeni yaliyokuwa kama nusu ya kiasi cha fedha hiyo.
Abramovic baada ya kuinunua Chelsea kwa kuwekeza fedha nyingi kwanza alimfukuza kocha Claudio Ranieri na kumleta Jose Mourinho aliyekuwa amechukua ubingwa wa Ulaya na FC Porto. Jose Mourinho alipewa hundi ya wazi kununua wachezaji wote wazuri aliowataka kama kina Didier Drogba aliyetoka Marseille, Arjen Roben kutoka PSV na wengine wengi.

Jeuri ya fedha ya Roman haikumuacha mtu salama, Jose alikuja kutimuliwa na kufuatiwa na makocha wengine kama Scolari, Guus Hiddink na wengine. Katika miaka 19 aliajiri karibu makocha 15.
Hilo halikuwa jambo la ajabu kwa Roman ambaye hadi sasa ameoa mara tatu na ameshaandika talaka mara 3. Wakati mbaya kwa Chelsea ulikuja mwanzoni mwa mwaka 2022 baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Serikali ya Uingereza na serikali nyingine za Ulaya Magharibi na Marekani ziliweka vikwazo dhidi ya Urusi, Rais Vladmir Putin na washirika wake.
Abramovic ni mmoja wa wafanyabiashara wa Urusi waliotajwa kuwa karibu na Rais Putin hivyo akalazimishwa kuiuza Chelsea kwa kundi la kampuni za wamarekani kwa kiasi cha Pauni bilioni 2.5 ambazo hata hivyo akaunti yake imefubazwa kusubiri uamuzi wa kama zikabidhiwe kwa serikali ya Ukraine au vinginevyo.
Abramovic hajatia kibindoni hata shilingi moja kutokana na mauzo ya Chelsea. Huyu Abramovic ni nani? Pesa aliipata wapi kiasi cha kuinunua Chelsea kama klabu ya kumpa burudani na wala si uwekezaji wa kibiashara hivyo kama walivyokuwa wawekezaji kwenye klabu nyingine?

Abramovic alizaliwa tarehe 24 Oktoba mwaka 1966 na kuwa yatima miaka minne baadae na baada ya kuvunjika kwa dola ya kisovieti, serikali ya Russia ilikuja na sera ya ubinafsishaji wa mashirika makubwa ya umma.
Abramovic na mkewe waliokuwa na biashara ya kutengeneza midoli au wanasesere wakatumia nafasi hiyo kuibadilisha kampuni na kupata hisa katika kampuni za nishati, chuma na mengineyo.
Hayo yote yaliwezekana kutokana na ukaribu walioujenga Roman na mkewe kwa wanasiasa wa Russia wa kipindi cha Boris Yetsin hadi wakati wa Putin na alikuwa pia gavana wa jimbo la Chukotka la Urusi.
Abramovic ambaye amekuwa na uraia wa Usovieti, Urusi, Ureno na Israeli alikuwa pia na viza iliyomruhusu kukaa Uingereza muda wote kwani pamoja na kuimiliki klabu ya Chelsea aliwekeza na alikuwa na makazi na nyumba zipatazo 70 Uingereza.
Hata hivyo, inasemekana mara nyingi alikaa Uingereza kwa siku mbili kwa ajili ya kuiona timu yake ikicheza na kisha kurudi Urusi, Israeli, Ureno au katika meli yake ya kifahari iitwayo Eclipse ambayo ilimgharimu zaidi ya Dola 300 milioni.
Abramovic mwenye utajiri unaokadiriwa kupita Dola 9 bilioni na akiwa miongoni mwa mabilionea watano wakubwa katika nchi ya Israeli, amekuwa kimya tangu apigwe marufuku kuishi Uingereza ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kuiuza timu ambayo aliipenda kwa moyo wote.

Kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais wa Marekani, Donald Trump za kumaliza vita ya Ukraine, huenda baadhi ya watu na taasisi za Urusi zikaondolewa vikwazo na hata mali na akaunti zilizofubazwa kuachiwa. Je kuna nafasi nyingine ya kumuona Abramovic akirudi Chelsea au kuwekeza tena katika michezo? Kwa sasa ni vigumu kulijibu hilo.
Yote kwa yote, Abramovic atakumbukwa kama mtu aliyeongeza thamani Chelsea, EPL na mpira wa Uingereza na Ulaya kwa ujumla. Itakuwa vizuri siku moja akionekana kwenye banda la wakurugenzi pale darajani London. Anaweza kuwa amesahauliwa na mpira lakini alama alizoziweka haziwezi kusahaulika.
Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.