Nyuma ya mkate huu mkubwa wa Mo Salah

Muktasari:
- Mkataba huu mpya umeongeza ukubwa wa mkate wa Salah akitia kibindoni Pauni 10 milioni kama bonasi ya usaliji lakini hatuwezi kuzungumzia hesabu hizi za juu bila kumtaja Magi, mke na mama watoto wa mchezaji huyo mzaliwa wa Misri.
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Mo Salah amebakiza mabao 76 kuifikia rekodi ya mfungaji bora wa Ligi Kuu England (EPL) kwa muda wote, ana misimu miwili mbele ya kufanya maajabu baada ya kusaini mkataba mpya hadi mwaka 2027.
Mkataba huu mpya umeongeza ukubwa wa mkate wa Salah akitia kibindoni Pauni 10 milioni kama bonasi ya usaliji lakini hatuwezi kuzungumzia hesabu hizi za juu bila kumtaja Magi, mke na mama watoto wa mchezaji huyo mzaliwa wa Misri.
Magi ni baraka, chachu na shuhuda wa kweli wa mafanikio ya mumuwe, amekuwapo kabla Salah hajafunga bao lake la kwanza EPL na hadi sasa akiwa na mabao 184 akishika nafasi ya tano katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote.
Vyanzo vingi vinamtaja Salah kuwa miongoni mwa wachezaji watatu wa juu wana-olipwa fedha nyingi zaidi EPL, mkate huu mkubwa Magi ndiye alikuja nao katika maisha ya mchezaji huyo anayeshika nafasi ya 10 kwa kutoa pasi nyingi za mabao ambazo ni 87.

Lakini kwanini tunasema Magi alikuja na mkate mkubwa kwa Mo Salah? Yeye ni nani hasa? Walijuana vipi? Familia yao kwa sasa ipoje? Bila kupoteza muda kaa mkao wa kula nikupe michapo kuanzia kwa Farao hadi huko kwa Mfalme Charles III.
Kwanza jina lake kamili ni Magi Mohammed Sadiq, hilo la Magi Salah limekuja baada ya kuolewa na ndilo linamtambulisha zaidi mwanamama huyu aliyezaliwa mwaka 1995 huko Nagrig, Basyoun nchini Misri, mahali alikozaliwa pia Mo Salah na kukulia miaka 32 iliyopita.
Familia ya Magi imeelimika kwa sehemu kubwa. Wazazi wake walikuwa walimu katika shule ya Mohammed Eyad Al Tantawi huko Nagrig, shule ambayo pia alisoma na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Alexandria na kubobea upande wa teknolojia.
Kwao hakulelewa peke yake, ana kaka zake watatu, dada zake pacha Mohab, na wengine wawili, Mahy na Miriam. Ingawa kuna taarifa chache kuhusu maisha yao ya awali kwa hawa ndugu zake wengine ila inaelezwa wanaishi kwa upendo.
Magi na Salah ni wapenzi wa utotoni, mshambuliaji huyo wa zamani wa AS Roma alikutana na ubavu wake huyo katika shule ambayo walikuwa wakisoma pamoja huko Misri, taifa lenye historia kubwa duniani.

Walikanyaga pamoja mchanga wa jangwani na kusafiri juu ya mto Nile, hatimaye urafiki wa ujana ulistawi na kuwa uhusiano wa kimapenzi, na kufikia Desemba 2013 wawili hao wakafunga ndoa katika sherehe ndogo ya Kiislamu iliyofanyika katika mji wao.
Kipindi hicho Salah alikuwa akiichezea FC Basel ya Misri baada ya kukuzwa katika timu ya vijana ya El Mokawloon. Tunaweza kusema ndoa na Magi ndio ilikuja na mkate mkubwa zaidi mezani kwa Mo Salah na mengine sasa historia. Kivipi?
Miezi michache baada ya ndoa hiyo ndipo Salah anatua darajani kuichezea Chelsea ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza EPL, ligi ambayo amekuja kuweka rekodi kibao za kutisha akiwa na majogoo wa Anfield, Liverpool aliyojiunga nayo mwaka 2017.
Akiwa anakipiga Chelsea, mabingwa wa EPL mara sita, ndipo Salah na mkewe Magi wanajaliwa mtoto wao kwanza waliyempa jina la Makka (2014), jina la mji mtakatifu wa Kiislamu uliopo nchini Saudi Arabia.

Kisha wakajaliwa binti yao wa pili, Kayan (2020) wakati huu Salah akiichezea Liverpool, cha kushangaza ni kwamba watoto wote wa mchezaji huyu wamezaliwa kipindi akicheza EPL, ligi maarufu zaidi duniani na inayomlipa takribani Pauni 500,000 kwa wiki.
Ikumbukwe Salah aliondoka Chelsea na kujiunga na timu nyingi kama Fiorentina na AS Roma zinazoshiriki Ligi Kuu Italia (Serie A) ndipo akarejea EPL, awamu hii akijiunga na Liverpool ambao anahitaji kushinda mchezo mmoja tu ili kuipa taji la pili la EPL.
Mara kadhaa Salah amekuwa akiposti picha za familia yake katika ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 64.4 ila mkewe hajihusishi kabisa na mitandao wa kijamii maaana hakuna ukurasa wake rasmi unaotambulika.
Inaelezwa kuwa Magi anapenda kuishi maisha ya kawaida na ya kujishusha tofauti na wenza wa mastaa wengine wakubwa katika soka, hayupo mitandoni ila anajulikana kwa kuigusa jamii kupitia shughuli za hisani anazofanya.

Wawili hao wanatoa sehemu ya mkate wao na kutoa misaada nchini kwao kama vile kujenga shule, hospitali na kuboresha huduma ya maji safi na salama hasa katika vitogoji walivyokulia, huku Salah kupitia shirika lake la hisani wakiwasaidia watoto yatima.
Hakuna ubishi kuwa Magi ana mchango wa moja kwa moja kwa Mo Salah hadi sasa ambapo ni mchezaji mkubwa duniani na mwenye nguvu ya ushawishi akiwa ndiye staa Afrika mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram, mtandao wenye watumiaji zaidi ya bilioni 2.1.