Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DAKIKA ZA JIOOONI: Mashujaa ina mitihani mitatu

DAKIKA Pict

Muktasari:

  • Mayanga alitambulishwa kikosini hapo Machi 21, mwaka huu, akichukua mikoba ya Mohamed Abdallah ‘Bares’ ambaye alikuwa na timu hiyo tangu msimu uliopita iliposhiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza.

KUNA mitihani mitatu inamkabili kocha wa zamani wa Taifa Stars, Salum Mayanga katika kikosi cha Mashujaa chenye maskani yake mkoani Kigoma.

Mayanga alitambulishwa kikosini hapo Machi 21, mwaka huu, akichukua mikoba ya Mohamed Abdallah ‘Bares’ ambaye alikuwa na timu hiyo tangu msimu uliopita iliposhiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza.

Katika dakika 450 zilizobaki sawa na mechi tano, kocha huyo ambaye pia aliwahi kuinoa Mtibwa Sugar, anapaswa kufanya kile ambacho mabosi wa Mashujaa wamekiona kutoka kwake.

Ikumbukwe, ubora aliounyesha kocha huyo msimu huu akiwa na Mbeya City alichokiacha nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship, ndicho kiliwavutia mabosi wa Mashujaa na kuona anaweza kuwa mkombozi wao.

DAKI 01

Sasa basi, Mayanga anakabiliwa na mtihani wa kwanza kuhakikisha anaibakisha timu hiyo ligi kuu, pili kuongeza idadi ya mabao ya kufunga na kupunguza uwezekano wa nyavu zao kutikiswa, mwisho kuipiku rekodi ya Bares aliyemaliza msimu uliopita nafasi ya nane kwenye msimamo na pointi 35.

Kwa sasa Mashujaa ina pointi 30 zilizotokana na mechi 25, ikishinda saba, sare tisa na kupoteza tisa. Hapo Mayanga anahitaji pointi tano katika mechi tano zilizobaki ili kuzifikia 35 alizomaliza nazo Bares msimu uliopita. Huo ni mtihani wa kwanza kwake.

Katika mechi hizo tano zilizobaki, si nyepesi kwani inakwenda kucheza dhidi ya timu ambazo duru la kwanza hazikufanya vizuri sana baada ya kukusanya pointi sita, ikishinda mechi moja, sare tatu na kupoteza moja dhidi ya timu hizo. Hata hivyo, katika msako wa pointi tano, takwimu hizo zinaweza kumbeba.

DAKI 02

Ukiweka kando hilo, mtihani wa pili ni kufunga mabao mengi zaidi na kupunguza uwezekano wa kuruhusu nyavu zao kugusa.

Msimu huu hadi sasa, Mashujaa imefunga mabao 25 na kufungwa 28, rekodi ambayo si nzuri kwani mabao ya kufunga ni machache kuzidi yale ya kufungwa.

Hali hiyo iliwakumba msimu uliopita walipofunga mabao 30 na kufungwa 33 huku wakimaliza ligi na deni la mabao matatu. Hivi sasa wana deni la mabao matatu pia.

Wakati Mayanga akiwa katika mtihani huo, ameanza vizuri kibarua chake akishinda mechi ya kwanza nyumbani mabao 3-0 dhidi ya Tabora United.

DAKI 03

Baada ya hapo, Jumapili hii anakwenda ugenini kukabiliana na Namungo, kisha Mei 2 atatua Dar kucheza na Simba. Mei 12 itaenda ugenini kucheza na Kagera Sugar. Mei 21 na 25 itakuwa dimba la nyumbani kumalizana na KMC na JKT Tanzania.

Rekodi zinaonyesha katika duru la kwanza, Mashujaa dhidi ya wapinzai hao watano waliobaki matokeo yalikuwa hivi; Mashujaa 1-0 Namungo, Mashujaa 0-1 Simba, Mashujaa 1-1 Kagera Sugar, KMC 0-0 Mashujaa na JKT Tanzania 0-0 Mashujaa.

Ndani ya kikosi hicho, David Ulomi ndiye mtaalamu wa kucheka na nyavu akiwa na mabao matano, akifuatiwa na Seif Rashid aliyefunga matatu sawa na Jafary Kibaya.

DAKI 04

Eneo la ulinzi, kipa Patrick Munthary anasimama vizuri langoni akifanikiwa kukusanya clean sheet 12, akishika nafasi ya tatu kwa makipa wenye clean sheet nyingi nyuma ya Moussa Camara wa Simba (15) na Djigui Diarra wa Yanga (13).

Mayanga amezungumzia ishu ya kuongeza mabao na kupunguza kuruhusu nyavu zao kutikiswa akisema: “Unaweza kuona katika mabao tuliyofunga washambuliaji wetu hawajafunga mengi, ipo hivyo kwa sababu ushirikiano wa wachezaji uliopo kutimiza majukumu yao.

“Hakuna mchezaji ambaye kazi yake ni kufunga, kila mmoja kikosini anaweza kufanya hivyo. Naamini hili likifanyiwa kazi tutaongeza idadi ya mabao, pia mabeki wanatakiwa kupunguza makosa ili kuwa salama eneo hilo.”

Mtihani wa mwisho na mkubwa zaidi ni kuipambania Mashujaa ibaki kwenye ligi kwa msimu wa tatu baada ya kushiriki misimu miwili sasa huku ule wa kwanza ikimaliza nafasi ya nane na sasa kuendelea kuwa hapo kabla ya mechi za jana.

DAKI 05

Mayanga katika hesabu za kuibakisha Mashujaa, amenukuliwa akisema ana kazi kubwa ya kufanya kwani mechi zilizobaki wanakwenda kucheza na wapinzani ambao nao wana uhitaji mkubwa wa pointi ili kufikia malengo.

Wakati Mayanga akisema hivyo, beki wa timu hiyo, Mpoki Mwakinyuke anasema wana kazi ya kufanya kuhakikisha wanavuna pointi 15 katika mechi tano zilizosalia, ingawa alikiri siyo kazi ndogo kwani wanakutana na timu zinazojikwamua na hatari ya kushuka daraja.

“Malengo yetu makubwa zaidi ni timu isalie Ligi Kuu, jambo la pili hatutaki kumaliza kinyonge kabla ya msimu kumalizika tuwe tunapambana kushinda mechi kwa kishindo na tuweze kumaliza nafasi kati ya sita, saba ama nane, itategemeana na matokeo ya wapinzani watu,” anasema.

Kwa upande wa kipa wa timu hiyo, Patrick Munthari ambaye ana clean sheet 12, anasema mbele yao wana kazi kubwa kuhakikisha wanajiondoa kwenye presha ya hatari ya kushuka.

“Ligi ilipofikia ni ngumu, kama wachezaji kazi yetu kubwa ni kujitoa tuwezavyo na matumaini yangu angalau tumalize katika nafasi sita au saba kwenye msimamo wa ligi,” anasema.