Prime
Miaka 32 ilivyoikomaza Simba CAF

Muktasari:
- Kuna wakati hususani mwanzoni mwa miaka 2000 Simba ilikuwa ikipitia wakati mgumu haswa inapokutana na timu za Kaskazini. Lakini wachambuzi wa mambo wanasema ilikuwa ni lazima ipitie hapo ili ifike kwenye uthubutu ilionao sasa.
KATIKA klabu za Tanzania ambazo zimepambana na kupitia mengi kwenye michuano ya kimataifa huenda Simba ikawa inaongoza.
Kuna wakati hususani mwanzoni mwa miaka 2000 Simba ilikuwa ikipitia wakati mgumu haswa inapokutana na timu za Kaskazini. Lakini wachambuzi wa mambo wanasema ilikuwa ni lazima ipitie hapo ili ifike kwenye uthubutu ilionao sasa.
Miaka 32 si mchezo katika ushindani wa soka la Afrika. Mwaka 1993 Mnyama iliposhika nafasi ya pili kwenye Kombe la CAF, wengi walidhani Simba ilikuwa karibu sana kulibeba taji. Lakini muda ukapita,matumaini yakayeyuka na miaka ikazidi kujongea pasipo na mafanikio makubwa.
Safari ya Simba SC kwenye mashindano ya kimataifa imekuwa na sura nyingi zile za mapambano, za mabadiliko ya kiutawala na sura za mashujaa.
Safari hii imekuwa ya milima na mabonde, lakini mwaka 2025, tunaiona Simba ikikaribia kilele, ikiwa imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara nyingine tena baada ya kupita kwa miongo mitatu.
Lakini mabadiliko ya kiutawala, kuingia kwa wawekezaji kama Mohamed Dewji ambaye yupo kwenye mchakato wa kupewa hisa na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, yaliibua Simba mpya.

KUMBUKUMBU ZA STELLA ABIDJAN
Simba SC ilianza safari ya kuisaka fainali ya michuano ya CAF mwaka 1993 kwa kuitoa Manzini Wanderers ya Eswatini ushindi wa jumla ya mabao 2-0, walishinda bao 1-0 kwenye kila mchezo, nyumbani na ugenini.
Ushindi huo uliwafanya kucheza robo fainali wakati huo hapakuwa na muundo wa makundi baada ya raundi ya pili, hivyo Simba ilikutana na USM El Harrach ya Algeria na kuing'oa kwa jumla ya mabao 5-0, walianza kwa kushinda mabao 3-0 wakiwa nyumbani kabla ya kumaliza kazi ugenini kwa mabao 2-0.
Matokeo hayo yaliifanya Simba kuwa timu ya kwanza Tanzania kutinga fainali ya michuano hiyo. Hata hivyo, katika mchezo wa fainali, waliambulia kichapo kutoka kwa Stella Abidjan ya Ivory Coast na kukosa taji hilo. Kuanzia hapo, ukame wa mafanikio ya kimataifa ukaanza.

MIKAO YA UKAME (1994–2017)
Katika kipindi hiki, Simba SC ilishiriki mara kwa mara michuano ya CAF, iwe Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho, lakini haikufua dafu.
Kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo maandalizi duni,miundombinu hafifu,maamuzi ya kiufundi yasiyokuwa na tija na kutokuwa na bajeti madhubuti ya kushindana katika ngazi ya kimataifa.
Mara kadhaa, Simba iliondolewa mapema kabisa katika hatua ya awali au raundi ya kwanza. Katika kipindi hicho, klabu ilikuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa kawaida wa uongozi wa wanachama na si wa kitaasisi, jambo lililoathiri mikakati ya maendeleo ya muda mrefu.
Mara chache walipopata nafasi ya kushiriki, waliishia kuwa wapita njia, wakikosa uthabiti wa kikosi na ubora wa benchi la ufundi. Ndio kipindi hicho ambacho kufungwa na timu za Arabuni hususani Misri haikuwa ajabu.

THIS IS SIMBA
Simba SC ilianza kuonesha mabadiliko makubwa kuanzia mwaka 2017/18 chini ya uongozi wa Rais wa Heshima Mohamed Dewji 'Mo Dewji' ambaye alianza kuibadilisha klabu hiyo kiutawala, kifedha na kiutendaji.
Alianzisha mfumo wa uendeshaji wa kisasa ulioweka msingi wa uwekezaji, uboreshaji wa miundombinu na usajili wa kimkakati.
Katika msimu wa 2018/19, Simba SC ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa makundi uanze. Safari hiyo iliwahusisha wachezaji kama Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, John Bocco, Aishi Manula, Erasto Nyoni, na Shiza Kichuya. Walifundishwa na Aussems.
"Nilipojiunga na Simba, lengo lilikuwa kufika hatua ya makundi. Tulivuka na kufika robo fainali hiyo ilikuwa historia. Lakini zaidi ya yote, niliwaaminisha wachezaji kuwa wana uwezo wa kushindana na timu kubwa za Afrika. Huo ndio msingi wa kila kitu." anasema Aussems.

MABADILIKO YANAYOENDELEA
Simba iliendelea kujiimarisha na kufikia hatua ya robo fainali tena ya Ligi ya Mabingwa Afrika, safari ambayo iliwafanya kuwa miongoni mwa klabu zinazohofiwa Afrika. Wakati huo, waliwafunga AS Vita na Al Ahly katika hatua ya makundi na kuonekana kuwa klabu imara. Wachezaji kama Luis Miquissone, Clatous Chama, Larry Bwalya, Chris Mugalu na Bernard Morrison walionesha kiwango kikubwa.
"Tulikuwa na timu ya kupambana, lakini hatukubahatika kufika mbali zaidi. Ushirikiano kati ya benchi la ufundi na wachezaji ulikuwa mkubwa. Simba ina uwezo wa kuwa timu ya nusu fainali na hata fainali kila mwaka, iwapo wataendeleza juhudi." anasema Didier Gomes Da Rosa.

MWAKA 2023: MAJONZI NA FUNZO
Mwaka 2023 ulileta machungu kwa Simba SC baada ya kutolewa na Wydad Casablanca katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mikwaju ya penalti licha ya kushinda mchezo wa kwanza nyumbani 1-0 wakati huo chama hilo lilikuwa chini ya Robertinho.
"Michuano ya Afrika ni migumu, kila kosa linaadhibiwa. Nilijifunza mengi ndani ya Simba, tulikuwa na njaa ya mafanikio. Tunaweza kusema kuwa tulikosa bahati dhidi ya Wydad." anasema Robertinho Oliveira.

KUANDIKA HISTORIA TENA
Baada ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2024/25, Simba ilipata tiketi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Ndipo wakaanza safari yao mpya ambayo sasa imewafikisha kwenye hatua ya nusu fainali kwa mara ya pili katika historia yao ya mashindano hayo.
Katika hatua hiyo, wameonesha ubora mkubwa kwa kuwatoa Al Masry, katika robo fainali kwa penalti 4-1 baada ya kupindua matokeo ya mabao 2-0 ambayo walipoteza kwenye mchezo wa kwanza. Sasa wanajiandaa kukutana na Stellenbosch FC kutoka Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar uwanja uliobeba matumaini mapya.
Kikosi chao kinaongozwa na nyota kama Leonel Ateba, Charles Ahoua, Debora Fernandes, Joshua Mutale, Elie Mpanzu, Shomary Kapombe na Kibu Denis. Chini ya Kocha Fadlu Davids, timu imeonesha nidhamu na uimara wa kimbinu.
"Tuna ndoto ya kutinga fainali, lakini tunachukua kila mechi kama fursa ya kujifunza na kusonga mbele. Ushindi dhidi ya Al Masry ni ushahidi wa kazi kubwa ya wachezaji wetu. Tunajiandaa kwa nguvu zote dhidi ya Stellenbosch. Tunanafasi ya kuandika historia mpya." anasema Fadlu Davids.

UFANISI KATIKA MICHUANO YA CAF
Ligi ya Mabingwa Afrika: Kushiriki mara 12
2002 – Rundi ya Kwanza
2003 – Makundi (Top 8)
2004 – Hatua ya awali
2005 – Raundi ya Kwanza
2008 – Raundi ya Kwanza
2011 – Mchujo wa makundi
2013 – Hatua ya awali
2018–19 – Robo fainali
2019–20 – Hatua ya awali
2020–21 – Robo fainali
2021–22 – Raundi ya pili
2022–23 – Robo fainali
2023–24 – Robo fainali
Kombe la Klabu Bingwa Afrika: Kushiriki mara 9
1974 – Nusu fainali
1976 – Raundi ya pili
1977 – Raundi ya pili
1978 – Raundi ya pili
1979 – Raundi ya pili
1980 – Raundi ya pili
1981 – Raundi ya kwanza
1994 – Robo fainali
1995 – Raundi ya pili
Kombe la Shirikisho Afrika: Kushiriki mara 6
2007 – Hatua ya awali
2010 – Raundi ya pili
2011 – Mchujo
2012 – Raundi ya pili
2018 – Raundi ya kwanza
2021–22 – Robo fainali
2024-25- ?
CAF Cup: Kushiriki mara 2
1993 – Fainali
1997 – Raundi ya kwanza