DAKIKA ZA JIOOOONI: Pamba Jiji inavyokataa kuizima ndoto ya miaka 23

Muktasari:
- Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 26, inafahamu kwamba kwa kuendelea kuwa hapo, italazimika kucheza mechi za mtoano ‘play off’ ili kutoshuka daraja kama ambavyo Kanuni za Ligi Kuu Bara zinavyosema timu itakayomaliza nafasi ya 13 na 14, zitacheza mechi hizo, huku zile za 14 na 15 zikishuka moja kwa moja.
PAMBA Jiji kwa sasa wanaumiza kichwa kuona ile ndoto yao waliyoiota kwa takribani miaka 23 kushiriki Ligi Kuu Bara, haipotei kwa haraka. Wanachokifanya ni kuweka mikakati mizito kuilinda ndoto hiyo.
Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 26, inafahamu kwamba kwa kuendelea kuwa hapo, italazimika kucheza mechi za mtoano ‘play off’ ili kutoshuka daraja kama ambavyo Kanuni za Ligi Kuu Bara zinavyosema timu itakayomaliza nafasi ya 13 na 14, zitacheza mechi hizo, huku zile za 14 na 15 zikishuka moja kwa moja.
Walipoanza msimu huu kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kuikosa kwa muda mrefu kutokana na kushuka daraja 2001, walikuwa na Kocha Mserbia, Goran Kopunovic, lakini hakudumu sana, Oktoba 16, 2024 akaondolewa kwenye benchi la ufundi.

Uamuzi huo ulifanya ikiwa ni baada ya timu hiyo kucheza mechi saba za Ligi Kuu bila ya kushinda hata moja zaidi ya kuambulia sare nne na kupoteza tatu.
Moja kwa moja uongozi ukaona mwenendo wa timu yao sio mzuri, ukafikia makubaliano ya kuachana na kocha huyo wa zamani wa Simba SC, ndipo Fred Felix ‘Minziro’ akakabidhiwa mikoba yake hadi sasa anaipambania timu isiipoteze ndoto yake kirahisi.
Licha ya kwamba Minziro hakuanza vizuri, lakini baadaye alipokaa na timu kwa muda kisha kufanya maboresho ya usajili dirisha dogo, angalau matumaini yameibuka licha ya kwamba bado timu haipo sehemu nzuri sana.
Kutokea hapo hadi sasa, Minziro ameiongoza Pamba Jiji kucheza mechi 19, akishinda sita, sare tano na kupoteza nane.

Zikiwa zimebaki mechi nne kumaliza msimu, Minziro amezipigia hesabu pointi sita katika mechi mbili zijazo za ugenini kabla ya kurudi nyumbani kumalizia mbili kufunga hesabu. Katika hesabu za ugenini dhidi ya Simba (Mei 8) na KenGold (Mei 13), Minziro anasema hawatakwenda kinyonge zaidi ya kusaka pointi zitakazowasogeza sehemu nzuri.
“Tunajiandaa na mechi hizo mbili za kwanza za ugenini, tutaanza na Simba kisha baadaye tutawafuata KenGold.
“Tunahitaji pointi zisizopungua sita katika mechi mbili za kwanza kabla ya kurudi nyumbani, ili tuwe na uhakika wa kubaki kwenye ligi, tutazitafuta na tutazipata kwenye mechi hizi zilizosalia,” anasema Minziro.
BADO HIZI
Wakati Minziro akiyasema hayo, rekodi zinaonesha katika duru la kwanza dhidi ya wapinzani hao wanne waliobaki, Pamba Jiji ilipata pointi nne kati ya 12 kufuatia kushinda dhidi ya KenGold (1-0) na sare dhidi ya JKT Tanzania (0-0), huku ikipoteza mbili dhidi ya Simba (1-0) na KMC (1-0). Hata hivyo, licha ya kupoteza mechi hizo mbili, lakini haikuwa kwa idadi kubwa ya mabao hali inayoonesha kuna matumaini fulani yapo. Ratiba ipo hivi; Mei 8, 2025 Simba vs Pamba Jiji. Mei 13, 2025; Ken Gold vs Pamba Jiji. Mei 21, 2025; Pamba Jiji vs JKT Tanzania, Mei 25, 2025; Pamba Jiji vs KMC.

MIKAKATI ILIVYOANZA
Baada ya kumaliza duru la kwanza kwa kukusanya pointi 11 baada ya kucheza mechi 15, Pamba Jiji ikafanya usajili wa wachezaji zaidi ya 10 wenye uzoefu zaidi ili kuongeza nguvu na waliopo, kati ya hao wanne wazawa ambao ni Habib Haji kyombo (Mshambuliaji), Hamad Majimengi (Winga), Deus Kaseke (kiungo) na Zabona Mayombya (Winga). Wengine wa kimataifa ni beki wa kushoto Sharif Ibrahim (Cameroon), kiungo mshambuliaji Shassir Nahimana (Burundi), kipa Mohamed Kamara (Sierra Leonean), mshambuliaji Francois Bakari (Cameroon), mshambuliaji Mathew Tegis (Kenya), kiungo Abdulaye Yonta Camara (Guinea) na beki wa kati Modou Camara (Gambia).
Kuingia kwa wachezaji, kikosi kikapata nguvu nyingine huku usajili mpya baadhi yao ukionekana kulipa kwa haraka zaidi.
Kati ya nyota wa Pamba Jiji walioingia dirisha dogo, Mathew Tegis ameonesha uongozi haukukosea kwani anaongoza kwa mabao kikosini hapo akifunga matano na asisti mbili, hivyo amehusika kwenye mabao saba kati ya 17 yaliyofungwa na timu hiyo, huku Zabona Mayombya naye ni kinara wao wa asisti akifikisha tatu. Wawili hao wamekuwa wakicheza kikosi cha kwanza mara kwa mara na kuipa uhai mpya Pamba. Mwingine aliyeingia dirisha dogo na kufanya vizuri ni Abdulaye Yonta Camara mwenye mabao mawili na asisti moja na Deus Kaseke aliyefunga moja.

WANA KAZI
Benchi la ufundi la Pamba Jiji linaloongozwa na Minziro, lina kazi kubwa ya kufanya kujenga nidhamu linapokuja suala la kukaba.
Hiyo inatokana na kwamba Pamba Jiji ni miongoni mwa timu zilizopigiwa penalti nyingi katika ligi msimu huu ambazo ni tano, hiyo inadhihirisha haichezi kwa tahadhari kubwa eneo lao la hatari, lakini pia yenyewe imepewa mikwaju miwili ya penalti huku mmoja ikiutumia vizuri na mwingine ikikosa, zote zikipigwa na Mathew Tegis.

Mbali na hilo, pia katika orodha ya timu zenye kadi nyekundu, Pamba Jiji inazo tatu kupitia Saleh Masoud, Eric Okutu na Abalkassim Suleiman. Wakati hali ikiwa hivyo, eneo la ulinzi licha ya kuruhusu mabao 27, lakini kipa wao Yona Amos anafanya kazi kubwa kuhakikisha anaipambania timu akiwa na clean sheet tisa, akishika nafasi ya nne nyuma ya Moussa Camara wa Simba mwenye 15, Djigui Diarra (Yanga 13), Patrick Munthary (Mashujaa 12) na Mohamed Mustafa (Azam 10).