Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DEBORA: Mama hapendi ngumi, huzifananisha na kujiuza

DEBORA Pict

Muktasari:

  • Lakini huenda hajakosea kujiita bondia mrembo, labda kutokana na kubarikiwa kuwa na sura nzuri ya kuvutia pamoja na mtindo wa mavazi ambayo kawaida huwezi kukubali kama utakutana naye mtaani na kuambiwa ni bondia.

DEBORA Mwenda ni binti wa miaka 26 pekee, lakini mashabiki wengi wa mchezo wa ngumi za kulipwa wamekuwa wakimtaja ‘bondia mrembo’.

Lakini huenda hajakosea kujiita bondia mrembo, labda kutokana na kubarikiwa kuwa na sura nzuri ya kuvutia pamoja na mtindo wa mavazi ambayo kawaida huwezi kukubali kama utakutana naye mtaani na kuambiwa ni bondia.

Debora hana muda mrefu tangu aingie katika mchezo wa ngumi za kulipwa, lakini amekuwa ni mmoja katika mabondia wachache wa kike waliojiweka tofauti na kuweza kutengeneza wafuasi wake katika mitandao ya kijamii  akiwa na wafuasi 16,000 katika mtandao wa Instagram.

Bondia huyo ambaye ni mzaliwa wa mkoani Njombe katika Wilaya ya Makambako, mpaka sasa rekodi yake inaonyesha amecheza mapambano matano ya ngumi za kulipwa, akichezea kwenye uzani wa feather ‘unyoya’.

Katika mapambano matano aliyocheza bondia huyo amefanikiwa kushinda mawili, na kati ya hayo moja likiwa kwa knockout, amepigwa mara mbili na sare mara moja.

Mwenda kwa sasa anakamata nafasi ya tatu kati ya mabondia watano bora wa uzani wake nchini wakati duniani akiwa anakamata nafasi ya 148 kati ya mabondia 259 huku akiwa na hadhi ya nusu nyota.

Raundi 19 mpaka sasa ndizo ameweza kucheza katika mapambano matano ikiwa kila raundi moja ina wastani wa dakika mbili ambapo kwa raundi 19 ametumia dakika 38 huku uwezo wake wa kuwapiga wapinzani kwa knockout ni asilimia 50.

Mwanaspoti limepiga naye stori na bondia huyo ambaye amegusia mambo mengi yaliyomfanya aingie katika mchezo wa ngumi za kulipwa kama bondia wa kike kutoka mikoa Nyanda za Juu Kusini.

Debora anaeleza kuwa alianza ubondia kama mtu ambaye anapenda kufanya mazoezi wanavyofanya watu wengine akiwa kwao Njombe kabla ya kuhamia Dar es Salaam.

Lakini kadri muda ulivyokwenda ndivyo alijikuta anaingia katika mchezo wa ngumi.

“Binafsi upande wangu ilianza kama sehemu ya mazoezi ya kuweka mwili fiti, lakini kadri muda ulivyoenda na ushawishi wa watu ambao nilikuwa nafanya nao mazoezi walinieleza inaweza kuwa sehem ya ajira yangu nyingine,” anasema.

DEBO 01

SWALI: Ulipataje nafasi ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa?

JIBU: Nakumbuka kuna mzee mmoja ambaye alikuwa bondia anaitwa Omari Yazidu yeye ameishi Makambako na alikuwa kila akija kutoka Dar es Salaam lazima azunguke kwenye maeneo wanayofanya mazoezi ya ngumi ndiye aliniona huko.

Lakini kwa bahati nzuri amekuwa akifahamiana na baba yangu kwa sababu na yeye alikuwa bondia huko zamani. Akamshawishi nijiunge na ngumi za kulipwa kwa yeye kuniruhusu ila alimueleza hadi atapojiridhisha kuwa naweza - basi ataniruhusu.

Haikuchukua muda sana baba akajiridhisha ndiyo nikapewa nafasi katika pambano langu la kwanza kupigana kama bondia mwaka 2022. Nashukuru nikafanikiwa kumpiga mpinzani wangu kwa pointi.


SWALI: Ukiangalia rekodi yako unajiona wapi?

JIBU: Najiona mbali kwa sababu katika mapambano matano niliyopigana, mapambano manne nimepigana nikiwa sina msingi mzuri wa ngumi. Kama nilivyosema nilianzia Makambako sehemu ambayo haina makocha wazuri  wala gym za kisasa.

Lakini pambano langu la mwisho, nadhani ndiyo naweza kusema nimecheza kwa utofauti mkubwa na kutokea hapo naamini nitaendelea kuonyesha utofauti mkubwa na kuhakikisha nafanya vizuri.

DEBO 02

SWALI: Mwaka jana wakati unakwenda kupigana na Samira Kasim ulitamba sana kwamba unakwenda kumpiga lakini mwisho wa siku ulipigwa, ukaangusha kilio nini kilikufanya ukalia?

JIBU: Kwanza hakuna bondia ambaye anakwenda ulingoni akaamini anakwenda kupigwa. Kila mtu anapenda kushinda. Kuhusu Samira nilijiandaa kwenda kushinda na ndicho nilichokuwa nakitaka maana nilifanya maandalizi magumu.

Sasa baada matokeo ya vile ilitokea hali ya kuumia kwamba nimepoteza wakati sikuwa nimetarajia kupoteza, ndiyo maana nililia kwa uchungu wa maumivu ya kupoteza.

Unajua nilijiandaa kushinda kwa sababu nilikuwa naona baadhi ya mapambano yake ila kutokana na mimi kukosa uzoefu na uchezaji wake, nadhani ilifanya kutokea hivyo.

DEBO 03

SWALI: Kitu gani huwa kinakuumiza?

JIBU: Nadhani mara nyingi naumia kama nitashindwa kuonyesha mchezo mzuri kwa sababu sitamani kushinda peke yake, natamani kuonyesha na mchezo mzuri ambao unanipa ushindi. Sasa ikitokea kutokuonyesha mchezo mzuri huwa naumia.


SWALI: Tangu umeingia kwenye ngumi kama mtoto wa kike umekumbana na changamoto gani?

JIBU: Kwanza jamii yetu ya Kitanzania haijazoea kuona mtoto wa kike akijishughulisha na mchezo wa kupigana, hivyo inafanya kutokukubalika kwa sababu watu wanakuwa hawaoni kama unafanya kitu cha kawaida.

Kitu kingine ambacho kama changamoto ni thamani ambayo anapata bondia wa kike na thamani ambayo anapata bondia wa kiume ni tofauti, kwa sababu waandaji wanachukulia wa kike pambano ni kama amesaidia au kuvutia mashabiki, lakini si kwa ajili ya kunufaika kithamani kwa mabondia wa kike.

DEBO 04

SWALI: Familia inakusapoti kwa kiasi gani?

JIBU: Napata sapoti kubwa kutoka kwa baba yangu ambayo naamini inatosheleza kuamini naweza kufanya kitu bila watu wengine kujali wanasema kitu gani.


SWALI: Vipi upande wa mama yako?

JIBU: Mama yangu hapendi kiukweli. Ni mzazi na huwa anasema mchezo ni hatarishi na alishawahi kuniambia kucheza ngumi hakuna tofauti na mwanamke anayejiuza kwa sababu na wao hufanya chochote ili wapate pesa.


SWALI: Nini kifanyike kuboresha maslahi ya mabondia wa kike?

JIBU: Nadhani ni bondia mwenyewe kutambua thamani yako ipo wapi, lakini pia hata waandaji waone hii ni kazi kama kazi nyingine wasione kama kiburudisho au wanafanya kusaidia maana tunafanya kitu ambacho wengine wameshindwa kufanya.

DEBO 05

SWALI: Nje ya ngumi unajishughulisha na kitu gani?

JIBU: Nafanya biashara ya kuuza nguo za mazoezi na vifaa vya mazoezi.


SWALI: Kitu gani kimefanya ujiite bondia mrembo au rangi yako?

JIBU: Hapana, siyo sababu ya rangi naamini neno urembo linaweza kuwa ni kitu chochote ikiwa kinafanyika kwa uzuri na kinavutia. Hicho kitu kinakuwa kirembo. Naamini vitu vyangu navifanya kwa uzuri na vinavutia ndiyo inaleta maana ya bondia mrembo.

DEBO 06

SWALI: Mahusiano yako na wakati unapokuwa na pambano mambo yanakuwaje?

JIBU: “Kwanza mahusiano ninayo, lakini huwa siyo rahisi kuvuruga vitu vingine kwa sababu mwenzangu hayupo karibu, hivyo siyo mtu ambaye tunaonana mara kwa mara... hivyo hata ikitokea mechi kwake inakuwa rahisi kuelewa.


SWALI: Ulimpata au alikupata ukiwa ulishakuwa bondia tayari na ilikuwaje?

JIBU: Tulikutana baada ya kuwa ni’shakuwa bondia... sijui nisemaje ila tulianza kufahamiana mtandaoni na baada ya muda tukakubaliana kuwa na mahusiano. Bado hatuna mpango rasmi ila tunaishi na mahusiano ni mazuri.”