Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga zikikohoa, filimbi inatetemeka

ZENGWE Pict


JANA ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya msimu wa mwaka 2025-2026 wakati timu zote zilipomaliza mechi zao pamoja katika Ligi Kuu Bara, ikiwa ni siku tano zaidi ya siku ya mwisho ya msimu uliopita uliocheleweshwa na mzozo wa Simba na Yanga uliotatuliwa na Ikulu.


Ni msimu ambao haukujaa mizozo kama ilivyokuwa msimu ya huko nyuma ambako watani hao wa jadi katika soka walisababisha sintofahamu baada ya mechi yao kubadilishiwa muda dakika za mwisho na nyingine kuahirishwa saa chache kabla ya muda wa mchezo kuanza.


Moja lililoendelea kutawala mijadala ya soka ni lile lile la makosa ya waamuzi na adhabu zilizochukuliwa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 ambayo maamuzi yake yalithibitisha mijadala ya makosa ya waamuzi ilikuwa sahihi.

Waamuzi wameendelea kuwa mijadala kiasi cha kutuhumiwa kuhusika katika upangaji matokeo, hali ambayo inapunguza utamu wa mchezo maarufu wa soka na kuondoa kukubalika kwa bingwa.

Kamati ya Saa 72 huwa haitoi tathmini ya msimu kwa upande wa uamuzi inayoweza kuonyesha ni makosa gani hasa yamekuwa yakitawala, kuweka idadi ya waamuzi waliochukuliwa hatua na wale waliomaliza msimu bila ya matatizo, na jinsi ya kutatua kasoro zao.

ZENG 01

Tatizo la uamuzi linaweza kuwa kubwa kimtazamo au kiuhalisia. Nasema kimtazamo kwa sababu inawezekana kabisa wanaoadhibu hawana teknolojia sahihi inayoweza kuwapa uhalali wa kuchukua hatua na hivyo kujikuta wakifanya uamuzi kutuliza moto ulio kwenye mijadala.

Lakini yawezekana kabisa kuna tatizo kubwa la uamuzi linalotokana na ama kutojua tafsiri sahihi ya sheria dhidi ya matukio, woga wa kufanya maamuzi sahihi hasa kwenye mechi zinazozihusu Simba na Yanga, ushawishi wa viongozi wa klabu unaopewa nguvu na fedha au maagizo ya viongozi wa mamlaka za mchezo huu.

Dunia imewapa waamuzi mamlaka yote ya kufanya uamuzi ndani ya dakika tisini na dakika chache kabla na baada ya mechi, pale inapoonekana ubinadamu unaweza kuwa kikwazo cha kufanya uamuzi sahihi, waamuzi huongezewa teknolojia ili iwasaidie kufanya uamuzi.

ZENG 02

Teknolojia hizo hufanyiwa marekebisho kabla ya kupitishwa na Bodi ya Mpira wa Miguu na baadaye Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Usaidizi huo ulianza kwa kutumia waamuzi watano kwa ajili ya kumsaidia mwamuzi katika kuamua kama mpira umeingia wavuni au umetoka au haujavuka mstari.

Baadaye ikaja teknolojia ya mstari wa golini (goal line technology), ambayo humshtua refa wa kati sekunde nane tu baada ya tukio.

Bado ikaletwa teknolojia ghali ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) ambayo humpa mwamuzi marudio ya tukio kutoka kila upande ili aweze kufanya uamuzi sahihi.

Sasa hadi mpira unawekwa chip ili utambue matukio ya kuotea. Hapo mwamuzi akikosea au akishindwa kufanya tafsiri sahihi ya sheria, ndipo utaweza kumwadhibu kwa kuwa teknolojia hiyo ipo na huonyeshwa hadharani.

Ili kumuwajibisha, sheria imefanyiwa marekebisho ili baada ya kuangalia marudio ya tukio kwenye runinga iliyopo pembeni ya uwanja, mwamuzi anatakiwa atangaze kwa mashabiki tukio lilivyokuwa na sheria inasemaje kabla ya kutangaza uamuzi wake.

ZENG 03

Teknolojia hizo hatunazo. Sasa hao wanaoadhibu waamuzi wanatumia teknolojia gani iliyoidhinishwa na FIFA? Hata zile video za marudio zinazorekodiwa na kampuni iliyopewa haki za matangazo, hazitoshelezi kumsaidia mwamuzi.

Yaani tukio linaonyeshwa kutoka pande mbili pekee. Hata runinga ingewekwa pale uwanjani, refa wetu asingeweza kuona tukio vizuri na kufanya uamuzi sahihi kwa kuwa kamera bado hazitoshi na teknolojia hiyo haijafikia kiwango hicho.

Kikubwa kabisa, teknolojia wanayotumia Kamati ya Saa 72 kiasi cha kumfungia mchezaji kwa tukio ambalo refa hakutaka kulifanyia uamuzi, imeidhinishwa na FIFA?

Maana yake kama kamati imefikia uamuzi wa kumrekebisha refa kwa kuangalia picha za marudio za tukio, basi ni lazima teknolojia hiyo iwe imeidhinishwa na FIFA kwa kuwa imevuka mipaka ya kuadhibu matukio yanayofanyiwa wakati mchezo umesimama.

Kwa hiyo, tatizo ni kubwa kimtazamo na kiuhalisia na uwezekano wa waamuzi kufungiwa zaidi ni mkubwa na hakuna uwezekano wa mwamuzi mmoja kutoguswa na adhabu za kufungiwa mechi, kushushwa daraja au kuondolewa kwenye ratiba. Wakati Bodi ya Ligi inahangaika kupata maoni ya kuboresha kanuni za ligi, ni muhimu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka mkakati mkubwa wa kushughulikia matatizo ya uamuzi na kuachana na dhana kwamba eti kuonyesha ukali kwa kuwa kufungia ndio kutakomesha kasoro zao.

Badala ya kutafuta suluhisho la muda kwa kualika waamuzi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mechi za Simba na Yanga, ni muhimu kutafuta suluhisho la kudumu.

Badala ya hao waamuzi kualikwa kuchezesha mechi za Simba na Yanga eti kwa sababu kanuni zinaruhusu, hao waamuzi au wakufunzi wangealikwa kwa ajili ya kambi fupi na waamuzi wetu ili kujadili kwa mapana matatizo yao.

Na hilo linaweza kufanyika kwa kuanza na tathmini makini ya matatizo ya uamuzi katika misimu mitatu au minne iliyopita, kuijadili kwa pamoja na kupata ushauri kwa waamuzi wale bora Afrika au wakufunzi mahiri wa jinsi ya kutatua matatizo ya uamuzi.

Matatizo hayo hayawezi kuisha usiku mmoja. Kuyamaliza ni mchakato unaohitaji umakini na subira.

La sivyo, mijadala kuhusu uamuzi mbovu itakuwa sehemu ya uendeshaji mpira wetu na tutaona ya kiwaida na inastahili kuendelea.