GOLDEN BOOT: Ukizitaja ligi zao wana ufalme wao 2025/26
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England anaongoza kwa mabao mengi barani Ulaya akiwa amefikisha zaidi ya mabao 33 katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) na asisti tano.
PARIS, UFARANSA: KATIKA soka la kisasa, ushindani wa kufunga mabao katika ligi kuu tano za Ulaya yaani England, Hispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa umeendelea kuwa mkali zaidi kuliko wakati wowote, ambapo msimu wa 2025/2026 umeibua majina makubwa na vipaji vipya vinavyokimbiza rekodi za mabao kila wiki.
Hapa tunaangazia wachezaji saba wanaofanya vizuri zaidi kwa sasa kwa upande wa ufungaji, wakiongozwa na kinara wa orodha ambaye ni Harry Kane wa Bayern Munich.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England anaongoza kwa mabao mengi barani Ulaya akiwa amefikisha zaidi ya mabao 33 katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) na asisti tano.
Uwezo wake wa kufunga kwa miguu yote, kichwa na pia kupiga penalti kwa ustadi umemfanya kuwa silaha kuu ya Bayern Munich. Kane anafuatiwa na Deniz Undav wa VfB Stuttgart aliyetupia mabao 18 na Luis Diaz anayecheza naye kikosini mwenye 15. Lakini ndani ya Bayern kuna mtu anaitwa Michael Olise, dogo wa Kifaransa mwenye asisti 31 katika Bundesliga pekee na mabao ya kufunga 13.
Nafasi ya pili Ulaya inashikiliwa na staika Kylian Mbappe wa Real Madrid, ambapo nyota huyo wa Ufaransa ameendelea kuthibitisha ubora wake akiwa na zaidi ya mabao 24 katika Ligi Kuu Hispania (La Liga).
Mbappe anajulikana kwa kasi ya ajabu, uwezo wa kupenya mabeki na utulivu mbele ya lango. Ni mchezaji anayebadilisha matokeo ya mchezo ndani ya sekunde chache.
Kwa Hispania, pia kuna Vedat Muriqi wa Real Mallorca anayekamata nafasi ya pili akiwa na msimu bora na mabao 21. Ingawa timu yake si miongoni mwa kubwa, lakini mchango wake umeifanya Mallorca iwe na matumaini ya kubaki kwenye ligi. Muriqi ni mfano wa wachezaji wanaozibeba timu mabegani mwao.
Hukohuko Ulaya kwenye Ligi Kuu England, Erling Haaland wa Manchester City bado ni tishio akiwa na mabao 24. Haaland anaendelea kuonyesha ubabe kama mshambuliaji wa kisasa akitumia nguvu, kasi na umakini wa hali ya juu ndani ya boksi.
Rekodi zake zinaonyesha kuwa ni mmoja wa washambuliaji hatari zaidi duniani kwa sasa. Kwa ujumla nyota huyo ana mabao 35 katika mechi 47 za mashindano yote msimu huu.
Mshangao mkubwa msimu huu ni straika wa Brentford, Igor Thiago akiwa na mabao 21 aliyofunga Ligi Kuu England akiendelea kumfukuzia kwa karibu Haaland.
Kwa ujumla Tudor ana mabao 24 katika mashindano yote na kinachofurahisha zaidi ni kwamba amempiku Antoine Semenyo wa Manchester City aliyekuwa akija juu kwa kasi katika miezi ya karibuni.
Mchezaji huyo ameibuka kama mmoja wa vipaji vinavyokuja juu kwa kasi, ambapo silaha yake kubwa ni matumizi ya nguvu na uwezo wa kushindania mipira juu anapokabiliana na mabeki wa timu pinzani, akiifanya Brentford kuwa timu hatari dhidi ya vigogo.
Katika Bundesliga pia, mbali na Kane, kuna mchango mkubwa wa Luis Díaz ambaye ameonyesha kiwango cha juu kwa kufunga mara 15 na asisti 13 jambo linaloonyesha ubora wake tangu alipoondoka Liverpool.
Kwa upande wa Ligi Kuu Italia (Ligue 1), majina yanayokimbiza kwa sasa ni matatu ambayo yanachezea timu za kawaida, isipokuwa moja ambalo lipo Marseille, mojawapo wa timu kongwe na kubwa nchini humo. Nyota wanaokimbiza kwa sasa ni Esteban Lepaul anayekipiga Rennes aliyehusika na mabao 22, akifunga 18 na asisti nne, huku akifuatiwa na Joaquin Panichelli wa Strasbourg aliyetupia mara 16 nyavuni akitoa pasi ya mwisho moja na anayefunga pazia ni Mason Greenwood wa Marseille mwenye mabao 15 na asisti sita.
Licha ya matukio ya kuumia mara kwa mara na kuwa nje ya uwanja muda mwingi msimu huu, lakini jina la Lautaro Martinez katika Ligi Kuu Italia (Serie A), limeendelea kubakia juu kwenye orodha ya wafungaji bora hadi sasa, ambapo mwamba ana mabao yake 16 na asisti nne hadi sasa, akifuatiwa na Marcus Thuram aliyehusika na mabao 17 akifunga 12 na asisti tano.
Lakini kinachofurahisha ni kwamba kuna mwamba mmoja katika kikosi chao cha Inter Milan, Federico Dimarco, ambaye kiasili ni 'wing-back' ndiye mpishi wa timu wa mabao akiwa na asisti 23.
Kwa ujumla, msimu huu unaonyesha kuwa ushindani wa Golden Boot Ulaya ni mkali. Kiatu cha dhahabu kwa Ulaya kitaamuliwa wiki ya mwisho ya mwezi ujao ambapo nyota mwenye mabao mengi ndani ya msimu atatunukiwa tuzo.
Kwa mashabiki wa soka, huu ni msimu wa kipekee kushuhudia vipaji vikubwa vikivunja rekodi na kuweka viwango vipya. Kama mwenendo huu utaendelea, basi ulimwengu wa soka utaendelea kushuhudia ushindani mkali na burudani ya hali ya juu kutoka kwa nyota hao.