HAINA KUFELI: Soka limeokoa maisha ya mastaa hawa

Muktasari:
- Ingawa ni moja ya kazi za muda mfupi sana lakini ni kimbilio kwa vijana wengi kujaribu maisha yao hasa wale wanaotokea katika familia duni/masikini na baadhi wametoboa kimaisha na sasa wanaishi kifahari.
SAO PAULO, BRAZIL: SOKA ni moja ya michezo inayolipa sana. Wanasoka wengi wamebadilisha maisha yao kutokana na mchezo huu. Wapo waliotokea katika maisha tofauti na wanatengeneza pesa kutokana na soka.
Ingawa ni moja ya kazi za muda mfupi sana lakini ni kimbilio kwa vijana wengi kujaribu maisha yao hasa wale wanaotokea katika familia duni/masikini na baadhi wametoboa kimaisha na sasa wanaishi kifahari.
Hapa tunakuletea nyota 10 wa soka ambao maisha yao ya utotoni yaligubikwa na umasikini wa hali ya juu kwa maana familia zao zilishindwa hata kumudu gharama za chakula na leo hii ni mabosi. Wametoboa kimaisha na wamebadilisha maisha yao na ndugu zao kutokana na soka kwa kile wanachovuna kuanzia pesa za usajili, mishahara na bonasi zao.
Zlatan Ibrahimovic
Alizaliwa katika eneo la Rosengård, Malmo, Sweden ambalo lilikuwa na ukata mkubwa kwa wakati huo.
Alizaliwa katika familia ya mama Mcroatia na baba raia wa Bonsia Jurka Gravic ambaye alikuwa mlevi kupindukia.
Wazazi wake walikuwa ni wahamiaji na walikutana Sweden ambako walianzisha mahusiano na kumpata Zlatan.

Hata hivyo, mambo yalikuwa magumu kwa staa huyu baada ya wazazi wake kutengana akiwa na umri wa miaka miwili tu.
Zlatan ambaye aliishi na mama yake alilazimika hata kwenda kuiba mara kwa mara ili kupata chakula pale mama yake alipokosa cha kuwalisha.
Luis Suarez
Unaweza kumwita, Luis Alberto Suarez Diaz. Ni mmoja wa wachezaji wengi kutoka Amerika ya Kusini na Kaskazini waliopitia maisha magumu katika ukuaji wao.
Suarez hakuwa hata na viatu wakati anacheza soka akiwa mdogo hadi kufikia miaka sita huko mitaa ya Salto, mji ulio kando ya Mto Uruguay.
Alizaliwa katika familia ya watoto saba na baada ya baba yake kuona maisha yamezidi kuwa magumu katika mji huo, alihamisha familia kwenda Montevideo, ambako pia mambo yaliendelea kuwa magumu.
Suarez alikulia katikakatika mitaa ambayo ilisifika kwa uhalifu wa aina mbalimbali.
Hata hivyo, hakuacha kucheza soka na akiwa na umri wa miaka tisa alionekana na skauti wa Nacional baada ya kufunga hat-trick alipokuwa akiichezea timu yake ya mtaani.
Cristiano Ronaldo
Mmoja wa wachezaji bora wa soka wa wakati wote, Cristiano Ronaldo aliishi katika umaskini wa kutupwa akiwa na mama yake na dada zake wawili.
Maisha ya familia yake yalikuwa magumu kiasi hata chakula tu ilikuwa changamoto na katika moja mahojiano yake aliwahi kusema kuna wakati walikuwa wakienda mgahawani kuchukua mabaki ya chakula.

Kutokana na umaskini, ilimlazimu kulala chumba kimoja na mama yake na dada zake. Alifukuzwa shuleni akiwa na umri wa miaka 14 kwa kumtupia kiti mwalimu aliye mdhihaki.
Alikuwa karibu kuachana na soka ili kufanya kazi ambayo itampa pesa aitunze familia yake lakini mama yake alimkataza na kumsisitiza apambane na kuwekeza nguvu katika soka.
Alianza kuonekana kipaji chake akiwa na miaka minane alipokuwa anaichezea Andorinha na baba yake alikuwa ni mtunza vifaa. Baba mzazi wa staa huyu alifariki kutokana na unywaji wa pombe kupitiliza mwaka 2005.
Alexis Sanchez
Pia anajulikana kama El Nino Maravilla, alizaliwa katika Jiji la Tocopilla, Chile. Baba yake aliitelekeza familia Sanchez alipokuwa mdogo sana na kwa asilimia kubwa alilelewa na mama yake ambaye alikuwa akifanya kazi ya usafi katika shule ambayo staa huyu alikuwa akisoma.
Licha ya uwezo wake wa kucheza soka, kutokana na hali ngumu, staa huyu wa zamani wa Arsenal alilazimika kufanya kazi mbalimbali kama kuosha magari ili kuhakikisha anaisaidia familia iliyokuwa inapitia kipindi kigumu cha umaskini.

Hata hivyo, kipaji chake kilimwokoa na kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji walikuwa wakipata mshahara mkubwa sana EPL alipokuwa anaichezea Manchester United.
Dani Alves
Fundi huyu alizaliwa Mei 6, 1983, huko Juazeiro, Brazil, kwa baba yake, Domingos na mama yake, Dona Lucia. Mama yake alikuwa hana kazi wakati baba yake akihudumu kama mkulima, ambaye Alvez alilazimika kumsaidia.
Beki huyu aliamka mapema saa 10 asubuhi ili kwenda na baba yake shambani na alitembea kilomita 30 kila siku.
Hata hivyo, mashamba katika eneo ambalo walikuwa wakilima hayakuwa yakizalisha kiasi kikubwa cha mazao, hivyo haikuwasaidia kuondokana na hali ngumu.
Licha ya kumsaidia baba yake kazi za shambani, staa huyu bado alipata nafasi ya kucheza soka alipokuwa akirudi nyumbani na hatimaye alionekana na Juazeiro SC na safari yake ilianzia hapo.
Angel Di Maria
Ni mmoja wa watoto watatu waliozaliwa katika familia ya Miguel na Diana, Angel Di Maria alikulia katika jiji la Pedriel huko Mendoza, magharibi mwa Argentina. Alikuwa mtundu sana alipokuwa na umri mdogo na hiyo ilisababisha aanguke kwenye kisima wakati fulani lakini akaokolewa.
Alikuwa akisaidia wazazi wake kufanya kazi katika kiwanda cha makaa ya mawe kilichopatikana kwenye mtaa waliokuwa wanaishi ili kuongeza kipato.
Licha ya kuwa na kipaji cha soka tangu utotoni, wazazi wake walikuwa maskini na hata wakashindwa kumnunulia viatu vya kuchezea.
Akiwa anacheza Torito, maskauti kutoka Rosario Central walimwona na inaelezwa ada yake ya kwanza ya uhamisho ilikuwa ni mipira 35 iliyotolewa kwenda kwenye timu yake aliyokuwa anaichezea.
Roberto Firmino
Kama wachezaji wengi wa Amerika Kusini, Firmino pia alikulia katika umasikini. Kwake, soka lilikuwa si tu shauku au starehe, bali pia njia ya kubadilisha maisha ya familia yake.
Jina lake kamili ni Roberto Firmino Barbosa de Oliveira. Alizaliwa na kukulia Maceio, jiji la Pwani ya Mashariki mwa Brazil.
Jiji hili linajulikana kwa fukwe zake nzuri na vitongoji vyenye uhalifu mwingi.
Firmino alizaliwa katika familia maskini, iliyopata tabu hata kwenye chakula.
Sadio Mane
Hadithi yake imekuwa ni maarufu sana. Alikulia Bambali, mji mdogo katika eneo la Sedhiou huko Senegal. Kwa sababu ya historia ya familia yao ya kiuchumi, Mane hakuwahi kwenda shule. Baba yake alimkataza kucheza soka, kwani alitaka ajikite katika dini.

Hata hivyo, Mane aliamua kuondoka kijijini kwenda Dakar kwa ajili ya kupambania ndoto yake ambako alionekana na wakala kutoka Ufaransa aliyempeleka Metz na tangu hapo maisha yake yameendelea kuwa bora siku zote.
Kutokana na umaskini wa familia yake na kijiji chake, Mane amekuwa akisaidia miradi mbalimbali kama shule na Hospitali pamoja na kusaidia familia zinazoishi eneo hilo.
Diego Armando Maradona
Ubora wake unajulikana duniani kote hata kwa wale ambao hawakuwahi kumshuhudia akicheza, jina lake limekuwa katika vichwa vyao kutokana na rekodi alizowahi kuziweka.
Maradona alizaliwa katika eneo la Villa Fiorito, Oktoba 30, 1961. Aliishi katika vitongoji vigumu vya Villa Fiorito nje ya Jiji la Buenos Aires.

Ukubwa wa familia yao iliyokuwa na watoto saba ilikuwa changamoto kwa baba yake ambaye alikuwa na kipato kidogo kutokana na kazi yake ya uchoraji. Kulala na njaa na watoto wote kulala chumba kimoja ilikuwa ndiyo staili ya maisha ya staa huyu.
Maradona bado alijitahidi uwanjani na alisaini mkataba wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 15 na akaendelea kusaidia familia yake tangu hapo. Maradona alifariki dunia Novemba 2020 akiwa na umri wa miaka 60 kutokana na matatizo ya moyo.
ENDRICK
Baada ya staa huyu kusajiliwa na Real Madrid, siku ya utambulisho baba yake alionekana akilia sana na katika mahojiano alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini alikuwa akimwaga machozi alisema, mchezaji huyo alipokuwa na umri mdogo siku moja alikuwa amekaa sebuleni, kisha Endrick akaja na kumwambia 'baba pesa ya kununulia chakula', baada ya kumwambia hiyo mzee huyo alianza kuangusha machozi kisha akamwambia mwanawe, Endrick sina pesa mfukoni.
Endrick akamkumbatia baba yake na kumwambia ipo siku atakuwa mchezaji mkubwa na ataiondoa familia yake katika umaskini na sasa anaishi ahadi hiyo aliyoiweka kwa baba yake wakati akiwa mdogo.