Hawa jamaa ndo kiboko ya nyavu za uwanjani tangu mwaka 2000

Muktasari:
- Na kwenye hilo la kufunga mabao, kuna mastaa hao wamejipambanua vyema kabisa kwa kuwa hodari kwenye kupasia mipira nyavuni, walipoonyesha uhodari huo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000.
LONDON, ENGLAND: RAHA ya mechi bao, wanasema. Ndivyo ilivyo na ndio maana kwenye mchezo wa soka kila siku kumekuwa na marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuona mechi zinakuwa na mvuto hasa kwenye ishu ya mabao kufungwa.
Na kwenye hilo la kufunga mabao, kuna mastaa hao wamejipambanua vyema kabisa kwa kuwa hodari kwenye kupasia mipira nyavuni, walipoonyesha uhodari huo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000.
Hii hapa orodha ya masupastaa 10 wanaoongoza kwa kufunga mabao kwenye timu zao za taifa na klabu kwa kuanzia mwaka 2000.
10. Hulk - mabao 441
Hakika si jina ambalo wengi wangelifikiria linapokuja suala la wafungaji mahiri kwenye mchezo wa soka, lakini Hulk amekuwa na rekodi za kibabe kabisa anapokuwa mbele ya goli la wapinzani. Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 38 bado yupo imara kwenye kikosi cha Atletico Mineiro, ambako amefunga mabao 125 katika kipindi cha miaka minne na nusu. Kwa kufikisha idadi ya mabao 441 kuanzia mwaka 2000, hiyo ina maana Hulk amefunga mara nyingi kuzidi Wayne Rooney, Sergio Aguero na David Villa.

9. Neymar - mabao 450
Kwasasa, supastaa Neymar amefunga mabao tisa zaidi ya aliyofunga Hulk na ndiye kinara wa mabao kwa wachezaji wa Kibrazili kwenye karne ya 21. Katika mabao 450 aliyofunga, 79 alifanya hivyo akiwa na kikosi cha Brazil.
Mwaka 2023, aliipiku rekodi ya mabao ya Pele ya kuwa kinara wa mabao wa muda wote wa Brazil, lakini majeraha yamekuwa yakimtibulia maisha yake ya soka tangu wakati huo.
Kwa sasa Wabrazili wanapiga dua ili kuona supastaa wao anakuwa fiti kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2026, zitakazofanyika Marekani.

8. Edinson Cavani - mabao 458
Bado anaonyesha kiwango bora kabisa akiwa na kikosi cha Boca Juniors pamoja na kuwa na umri wa miaka 38, Cavani ameweka jina lake kwenye orodha ya mastraika bora kabisa kwenye kizazi chake.
Alifurahia kiwango chake bora kabisa wakati anakipiga Napoli na PSG, ambako alifunga asilimia 66 ya mabao yake katika maisha ya soka. Cavani yupo kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu linaloendelea huko Marekani, ambako anatazamiwa kuongeza idadi yake ya mabao kabla ya kutundika daruga zake.
7. Harry Kane - mabao 479
Yupo kwenye kiwango chake bora cha kupachika mabao, bila shaka straika Harry Kane, atakuwa kwenye namba za juu kabisa za utikisaji wa mabao hadi kitakapofika kipindi cha kustaafu soka lake.
Kinachovutia ni kwamba tayari ameshavuka idadi ya mabao ambayo supastaa, Wayne Rooney amefunga kwenye klabu na nchi yake, kwa umri wa miaka 31 alionao na rekodi ya kufunga mabao 82 katika mechi 91 alizochezea Bayern Munich, straika huyo bado ana mengi ya kufanya kwenye soka lake. Yupo na kikosi chake cha Bayern kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.
6. Karim Benzema - mabao 498
Wakati akiwa si kwenye ubora wake mkubwa wa kupachika mabao kama ambavyo amekuwa akifahamika, straika Karim Benzema bado amekuwa na nafasi ya kuongeza idadi yake ya mabao katika kikosi cha Al-Ittihad anachokitumikia huko Saudi Arabia.
Nyakati ambazo staa huyo Mfaransa alikuwa kwenye kiwango bora cha maisha yake ya soka ni alipokuwa Real Madrid, ambako alifunga mabao 354 katika mechi 648.
Licha ya kwamba hajaichezea Ufaransa kati ya 2016 na 2020, amekuwa na rekodi nzuri pia ya kufunga kwenye soka la kimataifa, akiwa na mabao 37 katika mechi 97 alizotumikia kikosi cha Ufaransa kinachofahamika kama Les Bleus.

5. Zlatan Ibrahimovic - mabao 564
Linapokuja suala la kudumu kwenye soka la kiwango cha juu kwa muda mrefu, si wanasoka wengi wanaweza kushindana na straika Zlatan Ibrahimovic na hakika alikuwa bora kwelikweli ndani ya uwanja. Kwa ujumla wake, alifunga mabao 564 tangu mwaka 2000 na alivunja rekodi mbalimbali ndani ya muda huo.
Na kinachovutia zaidi, kwenye mabao hayo 564 aliyofunga, 341 alitikisa nyavu baada ya kutimiza umri wa miaka 30. Straika huyo mwenye majivuno mengi amejiweka pazuri kwa kuwa mmoja wa wachezaji waliotikisa nyavu mara nyingi tangu mwaka 2000.

4. Luis Suarez - mabao 575
Pengine hayupo kwenye makali yake kama ya zamani ya kuwa na kasi kubwa ndani ya uwanja, lakini straika Luis Suarez bado anafahamu namna bora ya kuhakikisha mipira inatinga kwenye nyavu za timu pinzani.
Tangu alipoachana na soka la Ulaya, Suarez aliendelea kufunga mabao kwenye timu za Nacional, Gremio na sasa Inter Miami.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 38 ni kiboko ya mabao kwenye timu ya taifa ya Uruguay, akifunga mara 68 kwenye soka la kimataifa na bado anaendelea na kazi yake ya kutikisa nyavu kwenye MLS. Kuna uwezekano mkubwa wa kufikisha idadi ya mabao 600 kabla ya kufikia kipindi cha kutundika daruga.
3. Robert Lewandowski -mabao 694
Msimu baada ya msimu, straika Robert Lewandowski amekuwa akifunga mabao kwa kadri anavyopenda. Fowadi huyo wa Poland sasa amefunga zaidi ya mabao 20 katika kipindi cha misimu 14 mfululizo kwenye ngazi ya klabu na bado kina kitu kikubwa miguu yake inaweza kukifanya ndani ya uwanja.
Alihitimisha msimu wa 2024-25 kwa kufunga mabao 42 kwenye michuano yote aliyotumikia Barcelona, ikiwa ni mabao mengi kwa kuzingatia alivyokuwa akifanya kwenye timu yake ya zamani ya Bayern Munich. Lewandowski pia ni kinara wa mabao wa muda wote wa Poland, akifunga mara 85 katika mechi 158 alizocheza kwenye soka la kimataifa.
2. Lionel Messi - mabao 865
Anaendelea kufanya maajabu yake ndani ya uwanja licha ya kuwa na umri wa miaka 37, hakika supastaa Lionel Messi bado ni mchezaji anayevutia kutazama.
Akiwa staa hodari wa kukokota mpira, supastaa huyo wa Kiargentina pia ni mmoja wa wamaliziaji bora kabisa iliyopata kutokea kwenye mchezo wa soka duniani. Kwa kuzingatia idadi ya mechi ambazo Messi alicheza kwenye maisha yake ya soka, hakuna pingamizi kwamba ni mchezaji bora kabisa kitakwimu katika kizazi chake.
Baada ya kutamba na vikosi vya Barcelona na Paris Saint-Germain kwa sasa mkali huyo anakipiga katika kikosi cha Inter Miami ya Marekani, ambayo inashiriki pia fainali za Kombe la Dunia la Klabu 2025.

1. Cristiano Ronaldo - mabao 938
Kwenye namba moja ya mastaa waliofunga mabao mengi kwa kuanzia mwaka 2000, lipo jina la mkali Cristiano Ronaldo.
Staa huyo wa Kireno aliweka wazi dhamira yake ya kufukuzia rekodi ya kufikia mabao 1,000 na hadi kufikia sasa, amebakiza mabao 62 tu kufikia idadi hiyo.
Wakati wanasoka wengi wakiwa wameshastaafu wanapofika umri wa miaka 40, Ronaldo yeye bado yupo moto uwanjani na ana njaa ya kufunga mabao mengi.
Kwa kitendo chake cha kubaki kwenye kikosi cha Al-Nassr, mchezaji huyo kuna uwezekano mkubwa wa kufikisha idadi ya mabao 1,000 ndani ya misimu miwili ijayo.