Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Jona Mkude amenikumbusha mbali, mwaka 1947

Muktasari:

  • Hata hivyo, baada ya mkataba wake kumalizika na Simba kutoonyesha nia ya kumuongezea mkataba mpya, Yanga walionyesha nia ya kumchukua na wakampa mkataba. Nadhani walikuwa na lengo la kutimiza ndoto yao ya kumuona Jonas akiwa amevaa jezi ya Yanga.

 KUNA wakati unaiacha ndoto mpaka mwisho ufike. Usiikatishe. Ukiikatisha maisha yanakuja na mvurugano wa ajabu. Kama Jonas Mkude angemalizia maisha yake Simba huenda lingekuwa jambo jema zaidi.

Hata hivyo, baada ya mkataba wake kumalizika na Simba kutoonyesha nia ya kumuongezea mkataba mpya, Yanga walionyesha nia ya kumchukua na wakampa mkataba. Nadhani walikuwa na lengo la kutimiza ndoto yao ya kumuona Jonas akiwa amevaa jezi ya Yanga.

Huwa inatokea. Kuna wakati hapa nchini mchezaji fulani wa mtani anahusishwa kila mara kwenda kwa mtani au huwa inasemwa na watu wake wa karibu kwamba mapenzi yake yapo kwa mtani. Ghafla inatokea dhamira kwamba lazima acheze timu ambayo amehusishwa nayo kwa muda mrefu.

Kama ilivyomtokea Mkude, basi imewahi kutokea sana katika siku za nyuma. Tatizo ni kwamba kama ndoto ya mtani ikitimia basi maisha hayawi kama zamani. Maisha hayawi kama yalivyokadiriwa. Wengi huwa wanacheza kwa mtani mwingine kwa kipindi kifupi na kuvuruga historia ndefu ambayo uliandika ukiwa katika klabu yako.

Zamani wakati huo mpira ukiwa haupo mitandaoni kama siku hizi tulikuwa tunaambiwa kwamba staa mkubwa wa Simba, Zamoyoni Mogella alikuwa na mapenzi makubwa na Yanga utotoni. Hatuna uhakika. Zilikuwa simulizi tu ambazo tulizisikia katika vijiwe vya kahawa tukiwasikiliza wazee - watu wazima, huku tukiwa tumeshika madaftari yetu baada ya kutoroka shule.

Baada ya kucheza Simba kwa jina kubwa na historia kubwa hatimaye mwaka 1993, Yanga chini ya tajiri wa Kihindi, Abbas Gulamali walifanikiwa kumsajili Mogella akitokea zake Uarabuni. Mogella alifanikiwa kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati akiwa na Yanga pale Kampala, lakini hakuweza kucheza Yanga kwa muda mrefu. Alicheza msimu huo kisha akastaafu soka.

Ilikuwa ni ndoto kwa watu wa Yanga kumuona Mogella akivaa jezi yao. Hadithi ikaishia hapo. Tatizo tuna watu wana nongwa. Kuna watu wa Simba mpaka kesho inawaumiza kwanini Mogella alikwenda kucheza Yanga. Hawajawahi kupona maumivu haya.

Edibily Lunyamila na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ walicheza Yanga kwa mafanikio makubwa. Walikuwa roho ya Yanga. Kwa nyakati tofauti walijikuta wameangukia Simba kwa kucheza kwa msimu mmoja tu. Mwisho mwisho wa maisha yao ya soka.

Bahati nzuri kwao walifanikiwa kurudi tena kumalizia mpira Yanga. Hata hivyo historia zao zilikuwa zimeingia doa kwa kiasi kikubwa kwa kwenda kucheza kwa mtani. Kuna wazee wangu nawafahamu huwa wana nongwa iliyopitiliza. Sidhani kama wamesahau kwamba hawa jamaa walikwenda kucheza Simba.

Ilimtokea pia Juma Kaseja. Baada ya kutamba kwa muda mrefu katika lango la Simba hatimaye tajiri mwingine wa Kihindi pale Yanga, Yusuf Manji alifanya kama vile ambavyo Gulamali alifanya kwa Mogella. Naye akamshawishi Kaseja kwenda Yanga.

Mama mmoja shabiki wa Simba pale Kariakoo aliangua kilio hadharani kama vile kuna msiba akilia kwa kitendo cha Kaseja kwenda Yanga. Alikuwa na uchungu mkubwa moyoni. Iliumiza wengi. Hata hivyo baada ya msimu mmoja Kaseja alirudi Simba.

Siamini kama yule mama pamoja na baadhi ya mashabiki wa Simba kama wamemsamehe Kaseja kwa kwenda kucheza Yanga. Hivi ndivyo watani walivyo. Hakuna masuala ya kuwa mchezaji wa kulipwa na mwenye uweledi linapokuja suala la kuhama kutoka Jangwani kwenda Msimbazi au kutoka Msimbazi kwenda Jangwani.

Jonas ameingia katika kundi hili. Bahati mbaya kwake ni kwamba licha ya kuwa ameingia katika kundi la Yanga yenye mafanikio, lakini amekaa nje zaidi kuliko hata wenzake. Fikiria katika pambano la juzi la Kombe la FA kati ya Yanga dhidi ya Songea United bado Jonas alikaa nje. Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alianza katika nafasi yake.

Sina uhakika nafsi yake inasemaje kuhusu hili. Huenda amefurahia kupata kitita cha mwisho mwisho katika soka, lakini lazima atakuwa na majuto fulani katika kuhamia Yanga. kitu kibaya zaidi ni kwamba sioni tena nafasi yake ya kurudi Simba na kurekebisha makosa.

Kama angecheza Yanga kwa mafanikio walau angekuwa katika nafasi nzuri ya kuwafanya viongozi wa Simba wawakomoe Yanga kwa kumrudisha tena klabuni hapo. Lakini ukizingatia kwamba aliondoka baada ya wao kuamua kuachana naye, huku baadaye akishindwa kutamba pale Yanga ni wazi kwamba hana nafasi ya kucheza tena Simba.

Hapo ndipo unapotamani walau ungeondoka zako Simba na kutotibua kile ambacho ulikitengeneza kwa miaka mingi. Kama ingekuwa ameondoka zake na kwenda Singida Black Stars au Namungo pengine heshima yake ingeendelea kuwa kubwa zaidi kwa Wanasimba. Hili la kwenda Yanga huwa linatia dosari kama ilivyo kwa Mogella enzi zake.

Wanasoka wanaofaidi kuhama hizi timu ni wale ambao walihama wakiwa katika ubora wao na sio katika siku za mwisho mwisho za maisha yao ya soka. Kina Method Mogella, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’ hawa ni aina ya wachezaji ambao hawakuwa na majuto kwa sababu walikokwenda walikwenda kutamba kwa muda mrefu kidogo.

Hawa ambao wametengeneza jina kubwa kwa muda mrefu katika klabu moja halafu wakahamia kwa mtani katika dakika za majeruhi nadhani kuna namna huwa wanajuta na wanakiri katika mioyo yao kwamba ni bora tu wasingeenda kwa mtani ili wabakie wanaheshimika jumla katika klabu zao walizokaa kwa muda mrefu.

Hawa wageni kina Clatous Chama na Benard Morrison au Emmanuel Okwi huwa hawana mambo mengi ya kujilaumu kwa sababu walikuja kutembea tu katika klabu hizi. Huwa wanatuachia machungu yetu na kurudi makwao. Hawana muda sana wa kujuta. Tatizo ni wachezaji wetu wazawa ambao tunashinda nao katika vijiwe vya kahawa. Lazima huwa wanajuta. Mkude amenikumbusha mambo ya kina Mogella na Lunyamila.