ZUGO: Bondia aliyetakiwa na Mayweather Sauzi, ngoma ikabuma

Muktasari:
- Zugo ni miongoni mwa mabondia wanne pekee nchini waliofikia nyota nne tangu taifa hili lipate uhuru kutokana na mipango na mikakati yake kwenye mchezo huo inavyokwenda.
UKIWATAJA mabondia wa Tanzania waliofikia rekodi ya hadhi ya nyota nne, basi jina la mtoto wa Zena Kipingu, mke wa Kanali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idd Kipingu ambaye ni maarufu kama Mama Zugo, basi jina la kijana wake, Abeid Keisy Kassy Zugo litakuwepo.
Zugo ni miongoni mwa mabondia wanne pekee nchini waliofikia nyota nne tangu taifa hili lipate uhuru kutokana na mipango na mikakati yake kwenye mchezo huo inavyokwenda.
Bondia huyo wa uzani wa light amekuwa hatajwi sana, lakini amekuwa na rekodi bora katika mtandao wa Boxrec chini ya usimamizi wa manejimenti inayomsimamia ya Kemmon Sports.
Kwa mujibu wa mtandao huo, bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 16 akiwa amefanikiwa kushinda 15 kati ya hayo 13 ni kwa Knockout na amepigwa pambano moja pekee kwa knockout mpaka sasa.
Licha ya kuwahi kufikisha hadhi ya nyota nne na kushika nafasi ya pili kati-ka mabondia wote bora wa Tanzania maarufu kama pound for pound, lakini ameshuka na kuwa na hadhi ya nyota mbili na nusu huku akiwa bondia wa 113 kati ya mabondia 2488 duniani katika uzito wake wakati nchini akiwa wa pili katika mabondia 114.
Lakini, kwa upande wa 'pound for pound' ya mabondia bora wa Tanzania kutoka katika kilo zote, Zugo ameporomoka hadi nafasi ya 10 kwa sasa.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na bondia huyo ambaye ameeleza mam-bo mbalimbali aliyokutana nayo kwenye safari yake ya mchezo wa ngumi.
Zugo anasema anatokea kwenye familia ya wapenda michezo kutokana na mama yake kuwahi kuwa bondia huko nyuma kabla ya kuwa promota sasa, lakini kaka yake Selemani Zugo na watu wengine wamechangia yeye kuwa bondia.
"Sikuwahi kuwa na ndoto ya kuwa mpiganaji kwa maana ya ubondia katika mchezo huu, lakini mazingira yamechangia sehemu kubwa sana kuweza ku-fika hapa," anasema.

"Unajua zamani nilikuwa napenda sana mpira na nilikuwa nacheza, lakini wakati fulani nikiwa nyumbani naona watu wakifanya mazoezi ya ngumi kwetu. Nakumbuka wakati huo gym ilikuwa nyumbani pale Kituo Kipya (Dar), makocha wengi walikuwa wakitoka jeshini. Tulikuwa naye kocha mmoja anaitwa Nyagawa alikuwa mwanajeshi wa JKT sasa marehemu ndiyo alikuwa akitufundisha na wengine akiwemo kocha Maneno.
"Sasa kitendo cha kuona watu wakifanya mazoezi kila siku ndiyo nikata-mani ila sikutegemea wala kukusudia wakati huo ilikuwa katika miaka 2007 hivi."
SWALI: Sasa shule na michezo ilikuwaje upande wako?
JIBU: "Unajua uzuri nimesoma katika shule za michezo maana nimesoma Jamii Nulhiya na Lord Barden ambazo zote zilikuwa za michezo ingawa haukuwepo mchezo wa ngumi, tukawa tunacheza karate.
Lakini ikawa ndiyo watu wa kwanza kucheza shuleni kwa sababu ya kuweza kuutambulisha kwa shule."

SWALI: Ilikuchukua muda gani kuingia kwenye ngumi za kulipwa?
JIBU: "Unajua wakati naendelea kupigana ikatokea pambano la Chaurembo Palasa na Venance Mponji na promota alikuwa Kaike Siraji, nikachomekwa nicheze ingawa upande wangu sikuchukulia uzito kabisa wa hilo pambano, niliamini ni sehemu ya kujifurahisha.
"Lakini katika hali ya kushangaza Chaurembo Palasa baada ya kupima uzito alikamatwa na polisi, akalala ndani halafu akatoka siku ya pambano na kwa hasira yeye aligoma kupigana kwa sababu hawezi kutoka polisi halafu akapigane basi ikabidi pambano langu ndiyo liwe kuu.
"Baada ya hapo kocha Mbaruku Heri ndiyo aliniweka chini na kunieleza namna faida iliopo kwenye mchezo kama nitaweka nguvu na maarifa yangu katika huu mchezo na ndiyo leo hii nimefikia hapa."
SWALI: Uliwahi kushinda mashindano ya kuhifadhi Qur-an ilikuaje kwa maana michezo na masomo ya dini?
JIBU: "Kiukweli ngumi kwangu ilikuwa kama ni sehemu ya kujifurahisha, niliwekeza sana kwenye kusoma zaidi, nimesoma kwenye shule za bweni hivyo michezo mara nyingi sana ilikuwa nikirudi nyumbani.
Ukiangalia hata shule ya msingi, nimesoma ya kiislam kwa hiyo kusoma Quran na kuhifadhi ilikuwa ni jambo la lazima katika kila siku za maisha yangu, nilikuwa shekhe mzuri sana (anacheka....).

SWALI: Mbona unacheka sasa?
JIBU: "Nacheka kwa sababu wakati mwingine mazingira yanakubadilisha ingawa Afrika Kusini ndiyo iliniharibu (anaendelea kucheka). Lakini kuhusu mashindano ukiondoa shule, nyumbani nilikuwa nasoma madrasa ya Shekhe Hussein (marehemu kwa sasa) ipo Kariakoo katika mtaa wa Jangwani na Amani inaitwa Shifaa.
"Wakati nasoma yakafanyika mashindano ya Quran ya madrasa za Dar es Salaam ndiyo nilifanikiwa kushinda kwa kushika nafasi ya kwanza ingawa mwaka sikumbuki vizuri kwa kuwa nilikuwa mdogo sana. Katika yale mashindano mgeni rasmi nadhani alikuwa naibu waziri wa ulinzi wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete, nikapata nafasi mbili za ufadhili wa masomo kwenda Afrika Kusini na Uingereza.
"Lakini kwa bahati mbaya wazazi hawakuwa tayari mimi kwenda kusoma nje kutokana na umri wangu kuwa mdogo zaidi wakaomba baada ya miaka miwili au mitatu baadaye ndiyo niweze kwenda."
SWALI: Hujawahi kuzijutia hizo nafasi baada ya mwenyewe kukua?
JIBU: "Sikujutia sana kwa sababu ni Mungu ambaye nikilikusudia jambo huwaga ananipaga fursa ndiyo maana nimekuwa mtu ambaye nasafiri sana.
"Lakini kuna upande nilijuta ila Mungu akanipa nyingine baadaye ingawa kwa sasa nikisafiri nafanya kwa gharama zangu. Pengine ile nafasi ingekuwepo kuna mambo yangeweza kupungua upande wa gharama, hivyo kama siyo wazazi huenda ningekuwa msomi mkubwa."

SWALI: Kitu gani kilikuunganisha Afrika Kusini?
JIBU: "Kule tuna familia yetu ndiyo inaishi na wao ndiyo waliniita kwa ajili ya kwenda kukuza kipaji kwenye ngumi ambapo niliweza kusaini mkataba na gym ya Wonder Boy Boxing Club na nilisaini mkataba wa miaka miwili. Lakini nilipata changamoto ya kibari cha kazi kutokana na maombi yangu kutumwa kwenye anuani tofauti na kupelekea nikae mwaka mzima bila ya kibari na hata nilivyopata muda ukawa umeenda sana.
"Sikuwa na kibali ila nilikuwa barua ambayo ilikuwa inaonyesha kwamba nasubiria kibali ila nikawa siruhusiwi kufanya kazi yoyote maana hata nil-ivyopata fursa ya pambano kubwa sikuweza kupigana kwa sababu mamlaka zilizuia kupigana kwa kuwa sikuwa na kibali.
"Lakini hata alivyokuja Flody Mayweather Afrika Kusini na timu yake nilipata nafasi ya kuonyesha uwezo wangu. Jamaa walinikubali wakataka tuondoke wote (kwenda) Marekani, lakini nafasi sikuweza kupata kwa sababu hayo mambo ni pamoja na mkataba na menejimenti yangu kule."
SWALI: Uliwahi kupata mchongo gani mkubwa wa pesa nyingi kwenye ngumi ukapoteza?
JIBU: "Kusema ukweli mimi dili huwa nazipata nyingi hasa mwaka jana na mwaka juzi zimenitembelea nyingi sana kama unavyojua nipo chini ya menejimenti yangu ya Kemmon Sports huwa siwezi kufanya uamuzi wa peke yangu kutokana na watu wanaonipa sapoti.
"Ukiangalia sisi vijana mara nyingi tukipata dili za maana huwa hata wale ambao wametupa sapoti hatuna tena muda nao, lakini kwangu ni tofauti kwa sababu walionishika mkono siwezi kuwatupa kivyovyote. Niliwahi ku-pata dili kwenda Ujerumani kukaa miaka miwili kwa mkataba halafu ikato-kea nyingine miaka minne Marekani ambayo alisimamia promota wangu mwenyewe ila walishindwana kwenye maslahi ikashindikana.
"Lakini nilipata pambano nikiwa na nyota mbili na nusu ambayo ilitakiwa ifanyike Mexico ambayo ofa yake ilikuwa milioni 175 halafu ilikuja ofa nyingine ambayo nilitakiwa nikapigane na Connor Benn, Uingereza ambayo ofa yake ilikuwa milioni 200.
"Hii ya Uingereza nilitakiwa nikacheze kilo 69 halafu mimi hata nile kiasi gani siwezi kufika kilo 69, niliomba angalau iwe kilo 63, wazungu walikataa na menejimenti ikashauri tuachane nayo.
"Binafsi moja kati ya nafasi niliyokuwa najutia ni hiyo kwa sababu Connor Benn ni bondia mkubwa mno, naamini ingenisogeza mbali kwa sababu ya ukubwa wake halafu wakati huo nilikuwa nimefikia nyota nne."