Prime
Kwa nini ‘Cleen Sheet’ tuzo apewe kipa?

MAGOLIKIPA wengi duniani wameshinda Tuzo ya Golikipa Bora wa mashindano kwa kigezo kikubwa cha kuwa na 'clean sheet' nyingi.
Kama huelewi ‘Cleen Sheet’, basi ni kitendo cha timu kucheza mechi na kumaliza bila kuruhusu bao, kwa hiyo mwisho wa mashindano huangaliwa ni kipa gani ameshiriki michezo mingi bila kuruhusu wavu wake kutikiswa ndiye anaibuka Kipa Bora wa michuano husika.
Kigezo hicho kinachoendelea kutumiwa katika mashindano mbalimbali ya soka kwangu hili sikubaliani nalo.
Kwanini sikubaliani nalo? Sababu zangu ni rahisi kabisa, tuzo binafsi zimekuwa zikizingatia kile mchezaji anachokifanya na sio timu yake inafanyaje? Mfano mfungaji bora anapatikana kwa idadi ya mabao aliyofunga na sio mashambulizi aliyofanya. Hapo huja dakika alizocheza ikiwa watalingana kwa idadi japo hapa kwetu bao la penalti limepunguziwa thamani japo wako wanaokosoa.
Kuna mtengenezaji bora nafasi nyingi zaidi katika michuano na si timu imetengeneza nafasi ngapi kwa maana hii hata tuzo ya kipa bora inapaswa kupimwa kwa kile alichokifanya binafsi na sio timu.

Hapo naweza kuwaacha baadhi na maswali, namaanisha nini ninaposema kipa asipewe tuzo binafsi kwa matukio ya timu ni hivi; Utaratibu wa timu kuzuia unaanza na washambuliaji, kisha viungo halafu mabeki na kipa akiwa kwenye hilo kundi la mabeki. Kama kutokuruhusu bao kunahusisha idara zote tatu kiwanjani kwa nini tuzo iende kwa kipa pekee na sio timu kwa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao?
Kwa kukumbusha tu huwa kuna tuzo ya beki bora ambayo huangalia nini anafanya binafsi katika kujilinda na kuandaa mashambulizi na sio safu nzima inafanya nini.

Hivyo basi badala ya shuka jeupe kuwa tuzo ya kipa inapaswa kuwa ya timu kwa kujilinda vema na kipa apimwe kwa idadi ya nafasi za mabao anazookoa kwa msimu.
Kwa nini nafasi anazookoa? Kwa sababu hii ni tuzo binafsi inamhusu yeye, hakuna kiungo, beki wala mshambuliaji anayeweza kumsaidia bali inamhitaji yeye peke yake.

Mfano rahisi kuelewa kipa wa Simba, Yanga au Azam ana nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo kuliko wa timu nyingine kwa sababu, ili Simba au Yanga imalize bila kuruhusu bao inamhitaji kipa kuokoa wastani wa nafasi tatu, huku kipa wa Kagera Sugar anahitajika kuokoa nafasi saba hadi kumi timu ipate shuka jeupe, ili utoe tuzo binafsi hiyo mechi utampa golikipa wa timu ipi ikiwa mechi itaisha bilabila.

Inawezekana wakati clean sheet kwa timu inafanywa tuzo ya kipa, kulikuwa hakuna uwezo wa kiteknolijia kuliko sasa bali tulipofikia tunaweza kuwapima kwa kuokoa na sio kutokuruhusu bao kisha kukawa na maksi kulingana na aina ya walizookoa kwa maana kuzipa maksi sevu au kuzigawa kwa madaraja kulingana na asilimia za nafasi husika kuwa bao.
Mfano msimu uliopita alichukua kipa wa Coastal Union kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao, ungerudi katika mashuti aliyookoa alishika namba mbili nyuma ya kipa wa Tanzania Prisons na hiyo aliipata baada ya kipa wa Yanga kukosa baadhi ya mcehi.

Dunia ikiwemo na sisi tunaweza kuangalia upya tuzo hii na kuifanya ya timu kutokana na mabadiliko ya mechi, ulinzi kuwa jukumu la timu kimbinu hivyo ikitokea timu imecheza michezo mingi bila kuruhusu bao iwe ni tuzo ya timu kama ilivyo tuzo ya timu yenye nidhamu, lakini kipa bora apimwe kwa kuokoa iwe kuokoa kwa kutoka nje ya boksi na kutumia miguu au ndani ya boksi kwa kutumia mikono, lakini anashiriki vipi kwanye ujenzi wa mashambulizi kwani mpira wa kisasa unamuhesabu kipa kama mlinzi pindi timu inapokuwa kwenye umiliki wa mpira.