Vichwa 10 vinavyochuana jino kwa jino kiatu cha dhahabu Ulaya

Muktasari:
- Straika wa Bayern Munich, Harry Kane alibeba tuzo hiyo msimu wa 2023-24, wakati alipofunga mabao 36, alifuatiwa na Serhou Guirassy na mabao yake 28 kwenye nafasi ya pili, wakati Erling Haaland na Kylian Mbappe walifungana kwenye nafasi ya tatu baada ya kila mmoja kufunga mabao 27.
LONDON, ENGLAND: MAMBO ni moto. Ndicho unachoweza kusema kuhusu vita ya kuwania Kiatu cha Dhahabu Ulaya.
Straika wa Bayern Munich, Harry Kane alibeba tuzo hiyo msimu wa 2023-24, wakati alipofunga mabao 36, alifuatiwa na Serhou Guirassy na mabao yake 28 kwenye nafasi ya pili, wakati Erling Haaland na Kylian Mbappe walifungana kwenye nafasi ya tatu baada ya kila mmoja kufunga mabao 27.
Sapraizi ipo msimu huu, ambapo vita ya kuwania tuzo hiyo ya ufungaji bora kwenye ligi za Ulaya umekuwa mkali katika kila mechi inayochezwa. Moto unawaka.
Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya mastaa 10 wanaofukuzia Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya msimu huu. Na orodha hii inawahusu wachezaji wanaoongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu tano bora za Ulaya, ambazo ni Premier League, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1, ambapo kila bao linalofungwa lina thamani ya pointi mbili.
10. Serhou Guirassy – mabao 20, pointi 40
Supastaa wa kimataifa wa Guinea aliwaduwaza wengi msimu uliopita alipofunga mabao 28 katika mechi 28 Bundesliga na kusaidia Stuttgart kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi, juu ya Bayern Munich. Guirassy ameendelea na makali yake ya kufunga hata baada ya kuhamia Borussia Dortmund, ambapo msimu huu hadi sasa ameshafunga mara 20, huku mabao yake yakiwa na msada mkubwa kwenye kikosi cha Dortmund katika mchakamchaka wa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
9. Erling Haaland – mabao 21, pointi 42
Straika Haaland alishinda tuzo yake ya kwanza ya Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya katika msimu wake wa kwanza Manchester City, wakati alipofunga mabao 52 kwenye michuano yote, huku akiweka rekodi ya kufunga mara 36 Ligi Kuu England. Msimu uliopita haikuwa bora kwake, lakini bado alifunga mabao 27 na kufanikiwa kutetea tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England na kushika namba tatu kwenye tuzo ya Kiatu cha Ulaya. Msimu huu hadi sasa ameshafunga 21.
8. Omar Marmoush – mabao 21, pointi 42
Baada ya kuanza msimu akionyesha kiwango bora kabisa katika kikosi cha Eintracht Frankfurt, Manchester City ilivutiwa na kutoa Pauni 59 milioni kunasa huduma yake ili akakipige kwenye Ligi Kuu England. Na baada ya kutua kwenye kikosi hicho cha Pep Guardiola ameonyesha ubora mkubwa, akifunga hat-trick dhidi ya Newcastle United huku akifikisha mabao 21 kwenye ligi na kuingia kwenye mchakamchaka wa kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya na timu yake ikiwamo kwenye Top Four.
7. Ousmane Dembele – mabao 21, pointi 42
Dembele amekuwa kwenye kiwango bora Paris Saint-Germain chini ya kocha Luis Enrique, akifunga mabao 21 kwenye Ligue 1. Mabao 13 kati ya hayo aliyofunga Ligue 1 amefunga katika mechi tisa tangu ulipoanza mwaka huu. Ameendeleza ubora pia hadi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuibeba timu yake kufika fainali ya michuano hiyo. Lakini, kinachovutia kuhusu Dembele ni kwamba ameanzishwa kwenye mechi 19 za ligi, lakini ana mabao 21.
6. Alexander Isak – mabao 23, pointi 46
Mmoja wa washambuliaji walipo kwenye kiwango bora kabisa Ulaya kwa sasa. Isak amesaidia Newcastle kuwamo kwenye Top Four ya Ligi Kuu England akifunga mabao 23 katika mechi 32 alizocheza katika ligi hiyo. Kiwango chake kinamfanya kuwamo kwenye orodha ya wachezaji wanaowindwa sana katika kuelekea dirisha la usajili wa majira ya kiangazi. Arsenal na Liverpool zinamtaka, lakini shida ipo kwenye ada yake ya usajili kuwa juu sana. Mabao yake yanamwingiza kwenye vita ya kuwania Kiatu cha Ulaya.
5. Mateo Retegui – mabao 24, pointi 48
Atalanta imefanikiwa kuwa na mchezaji katika vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya baada ya mkali wake, Mateo Retegui kufunga mabao 24 kwenye Serie A hadi sasa. Msimu uliopita, kikosi chao kilikuwa na mkali Gianluca Scamacca aliyekuwa moto, ambapo alifunga mabao 19 katika misimu yote. Kikosi hicho kinachonolewa na Gian Piero Gasperini kwa sababu kwenye kikosi chao kuna staa Retegui, ambaye amefunga mabao 24 katika mechi 33 alizochezea Atalanta kwenye Serie A.
4. Robert Lewandowski – mabao 25, pointi 50
Straika gwiji wa Poland, Lewandowski amefanikiwa kucheza chini ya makocha mahiri sana katika zama hizi kuanzia kwa Jurgen Klopp hadi kwa Carlo Ancelotti, lakini chini ya Hansi Flick ameonyesha kiwango bora kabisa, ikiwamo kufunga mabao 48 katika michuano yote wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich msimu wa 2020-21. Kwa sasa yupo Barcelona na anaendeleza makali, akifunga mabao 25 kwenye La Liga huku akifukuzia tuzo ya tatu ya Kiatu cha Dhahabu Ulaya.
3. Harry Kane – mabao 25, pointi 50
Straika Kane alishinda Kiatu cha Dhahabu kwenye Bundesliga msimu uliopita na yupo kwenye nafasi nzuri ya kushinda tena tuzo hiyo ya ufungaji bora kwa Ujerumani msimu huu. Staa huyo wa England amefunga mabao 25 katika mechi 30 za ligi na kwenye Bundesliga msimu huu, amefunga hat-trick mara tatu. Lakini, kwenye ishu ya kutetea Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya kwa msimu huu, hilo linaonekana kuwa jambo zito kwa Kane na kwamba amebakiza mechi moja tu, dhidi ya Hoffenheim.
2. Kylian Mbappe – mabao 27, pointi 64
Licha ya kuanza maisha yake Madrid kwa kasi hafifu, straika Mbappe amekuwa kwenye kiwango bora kabisa siku za karibuni. Hakuna mchezaji wa kutoka Ligi Kuu tano bora za Ulaya aliyefunga mara nyingi tangu mwaka 2025 uingie kumzidi Mbappe. Jumapili iliyopita alipiga hat-trick kwenye kipute cha El Clasico na hivyo kujiweka imara kabisa katika mbio za kusaka Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, ambapo itakuwa mara yake ya kwanza kukibeba katika maisha yake ya soka.
1. Mohamed Salah – mabao 28, pointi 68
Si tu staa huyo wa Liverpool anaongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu tano bora za Ulaya, bali pia ni kinara wa asisti pia. Salah alikuwa matata kwelikweli kwenye kufunga mabao mwanzoni mwa msimu na kati, lakini mabao yake yamekauka siku za karibuni. Amefunga mara moja tu katika mechi saba za mwisho kwenye Ligi Kuu England, lakini bado ana nafasi ya kuongeza mabao yake kwenye mechi mbili zilizobaki za timu yake dhidi ya Brighton na Crystal Palace. Ndiye kinara wa mabao kwa sasa.