Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Pasaka imepita lakini Dabi ya Kariakoo bado haijafufuka

DABI Pict

Muktasari:

  • Kila ninakopita rafiki zangu wanaoamini huenda mimi niko mbele ya muda wananiuliza kama ninajua Dabi ya Kariakoo itachezwa. Na kama itachezwa, basi itachezwa lini. Sina jibu lolote la uhakika.

MWOKOZI wetu Yesu aliteswa baada ya usaliti mkubwa wa rafiki yake, Yuda Iskariot. Akafa. Akazikwa. Akafufuka Siku ya Pasaka. Hata hivyo, Dabi ya Kariakoo ambayo ilikuwa wakati ule wa kwaresima bado haijafufuka na hatujui itafufuka lini.

Kila ninakopita rafiki zangu wanaoamini huenda mimi niko mbele ya muda wananiuliza kama ninajua Dabi ya Kariakoo itachezwa. Na kama itachezwa, basi itachezwa lini. Sina jibu lolote la uhakika.

Ilikuwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na Kwaresima. Idd Mosi ilipita, Idd pili ikapita, Pasaka ikaja ikapita, bado pambano hili hatujui litachezwa lini. Kwa Wakristo Bwana Yesu alifufuka, lakini pambano hili bado halijafufuka.

Sababu ya msingi ambayo naifahamu kwa nini dabi haijapangiwa muda ni ukweli waliokosea wanataka kwanza Yanga ibadili msimamo wake ili tarehe mpya ya dabi ipangwe.

Hawana jeuri ya kutangaza tarehe mpya ya dabi bila ya kuibembeleza Yanga.

DB 01

Wanajua wakitangaza tarehe mpya kama walivyosema mchana ule wa Machi 8 dabi itapangiwa tarehe nyingine, basi Yanga watashikilia pale pale hawachezi.

Na kama hali ikiwa hivi hivi basi Yanga hawatakwenda kweli uwanjani.

Kwa kuwa siku ile Yanga kwa makusudi kabisa walikwenda uwanjani na wakafanya ‘warm up’ hata kama mwamuzi hakuwepo, ulikuwa mtego tosha, Simba wanaweza kufanya hivyo katika tarehe nyingine, lakini hawapaswi kupewa pointi tatu.

Bahati mbaya hakuna mwamuzi anayeweza kumaliza pambano hilo na kuipa mamlaka Bodi ya Ligi kutangaza Simba anapewa pointi tatu. Haitatokea.

Ndiyo maana wanajiadhari na hali hii mapema kwa kutotangaza tarehe ya dabi.

Kwa mfano itokee watangaze tarehe ya dabi kabla ya Yanga kuafiki kucheza ni wazi maandalizi yataendelea, lakini itakapofika saa tisa na nusu bila ya dalili zozote za Yanga kuja uwanjani basi mechi itaahirishwa kama ilivyoahirishwa mechi ya siku ile.

DB 02

Ghafla tu itatoka taarifa mitandaoni pambano limeahirishwa.

Kuna ganzi kubwa katika kuzitawala Simba na Yanga.

Ni wakubwa hasa. Kigugumizi kimekaa muda mrefu kwa sababu Yanga wamesema hawachezi. Hakuna wa kuwavimbia.

Hata waziri wa wizara husika aliwaita hawa wakubwa wa Kariakoo, lakini hakutoa maamuzi yoyote kwa sababu ya ukubwa wao.

Nipo gizani sijui kinachoendelea. Nasikia Yanga wamekwenda CAS. Sidhani kama hii inawazuia Bodi ya Ligi kutotangaza tarehe ya pambano hili.

Wao wana nguvu yao ya kujipangia mambo yao bila ya kujali Yanga wamekwenda CAS. Hata hivyo, hawana ubavu wa kufanya hivyo.

DB 03

Kitu kingine ambacho sifahamu ni watu hawa waliokosea wanafanya juhudi zozote na maarifa kuwashawashi watu wa Yanga wacheze mechi hiyo.

Kwa sasa kuna ukimya mwingi na Watanzania wameachwa gizani.

Kitu ambacho bado kipo gizani zaidi ni kuhusu kanuni zinasema nini kama mechi hii haitachezwa. Kuna uwezekano isichezwe na tukapata bingwa?

Katika mazingira haya ambayo Yanga na Simba zinapishana pointi chache kama zote zitashinda mechi zote zilizosalia kuna uwezekano wa kupata bingwa bila ya pambano hili kuchezwa?

Mtu mmoja aliwahi kunipigia hesabu endapo Yanga itashinda mechi zake zote, na Simba itashinda mechi zake zote bila ya pambano hilo kuchezwa basi Yanga atakaa kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi moja tu.

DB 04

Unawezaje kumtangaza Yanga bingwa katika mazingira haya wakati Simba ana mechi ambayo anaweza kushinda na kutangazwa kuwa bingwa? Zaidi ya kila kitu ni kwa sasa Simba wapo tayari kucheza mechi yenyewe.

Sijui Elie Mpanzu amewapa jeuri au vipi, lakini najua wapo tayari kucheza kuliko ilivyokuwa siku ile.

Kwa yeyote aliyekoroga mambo lazima ajue namna ya kunywa matokeo yake. Watanzania wanaitaka tarehe ya mechi hii haraka iwezekanavyo.

Walau tarehe itajwe tu halafu tujue msimamo wa Yanga kama utaendelea kuwa vile vile au msimamo wa Simba utabadilika.

Ukimya unawavuruga zaidi Watanzania.

Tumeona mechi nyingi zikiharishwa na kisha kupangiwa tarehe haraka iwezekanavyo. Vipi kuhusu hii? Mbona kimya?

Nadhani wanazidi kuthibitisha kanuni zipo kwa ajili ya klabu nyingine 14 ambazo zinashiriki Ligi Kuu lakini siyo Simba na Yanga.

Hata Rais wetu wa mpira, Wallace Karia baada ya kutoa maneno ya nguvu siku ile akiwa uwanja wa ndege akirudi kutoka Cairo sasa hivi amepiga kimya.

Nadhani amegundua ukubwa wa Simba na Yanga linapokuja katika misimamo yao. Inabidi uongee nao kwa sauti ya upole zaidi kuliko sauti ya mamlaka.

Ambacho nakifahamu ni hata kama pambano hili litachezwa, hii haitakuwa mara ya mwisho kwa timu moja kuamua kutocheza mechi katika siku ya pambano.

DB 05

Ni kwa sababu viongozi wa timu hizi wanajua vyema namna ya kutumia nguvu za ukubwa wao.

Wanajua wenye mamlaka na mpira wataendelea kuwagwaya.

Kanuni zinaweza kuwa wazi, lakini wao wanaweza kuamua kupingana na kanuni na usiwafanye chochote.

Ambao hawafahamu ni hata mechi zao wanazopaswa kucheza na timu nyingine zinapoahirishwa au kupangiwa tarehe, kinachoafanyika ni wenye mamlaka na mpira kuwasiliana nao kwanza ili waridhie.

Ni tofauti na kina Kagera Sugar ambao wanaweza kupanguliwa tarehe zao bila ya majadiliano yoyote na Bodi ya Ligi.

Simba na Yanga ni midude mikubwa na hatujui kama kuna siku wanaweza kudhibitiwa na kanuni.

Siku hiyo ikifika mpira wa Tanzania utakuwa umepiga hatua.