Prime
JICHO LA MWEWE: Yakoub Suleiman anaweza kuwa Tanzania One kwa muda mrefu

Muktasari:
- Sio kwamba Watanzania wanamfahamu sana Yakoub. Hapana. Ni wachache ndio wanaomfahamu na kumfuatilia. Wanaomfuatilia wanakwambia ni bonge la kipa katika lango la JKT Tanzania. Wengi tunawafuatilia zaidi wachezaji wa Simba na Yanga.
ALIKUWEPO kipa mpya katika macho ya Watanzania walio wengi katika pambano la Morocco dhidi ya Taifa Stars pale Oujda, Kaskazini Magharibi mwa Morocco. Hakuna aliyeshangaa sana kumwona Yakoub Suleiman akikaa katika lango la Taifa Stars katikati ya wiki hii.
Sio kwamba Watanzania wanamfahamu sana Yakoub. Hapana. Ni wachache ndio wanaomfahamu na kumfuatilia. Wanaomfuatilia wanakwambia ni bonge la kipa katika lango la JKT Tanzania. Wengi tunawafuatilia zaidi wachezaji wa Simba na Yanga.
Wachache huwa wanatenga muda wao kufuatilia mechi ya JKT dhidi ya Mashujaa kule Kigoma au pambano la Coastal Union dhidi ya Kagera Sugar kule Kaitaba, Bukoba. Wanaoweza kufuatilia pambano la JKT mahala, ndio ambao hawakushangaa sana kumuona Yakoub akiwa langoni kule Morocco.
Ni kipa mzuri. Ana umbo kubwa. Utabiri wangu wa hali ya hewa unanionyesha anaweza kuwa ‘Tanzania one’ kwa muda mrefu ujao kama akijisikia kuwa hivyo. Wakati mwingine hatima ya wachezaji wa Tanzania huwa inaamuliwa zaidi na wao wenyewe.

Katika pambano dhidi ya Morocco alikuwa na matatizo mawili ya msingi ambayo yanaeleweka. Kwanza kabisa alikuwa na wasiwasi mkubwa na mechi husika. Pambano lake la kwanza halafu unacheza dhidi ya Morocco ugenini.
Morocco wenyewe walikuwa wamekamia kushinda mechi ili kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwakani. Safu ya mbele ilitisha. Ilikuwa inaongozwa na Brahim Diaz anayecheza Real Madrid. ilikuwa lazima awe na wasiwasi mkubwa.
Bao la kwanza lilitokana na wasiwasi huu. Yakoub alikuwa na ‘timing’ nzuri ya mipira ya juu lakini kuna wakati alikuwa anaamua kupangua mipira ambayo kama ingekuwa inapigwa na Yanga au Kagera Sugar angeweza kuidaka. Sidhani kama aliandaliwa kisaikolojia kuhimili mambo haya kwa mara yake ya kwanza katika jezi ya Taifa Stars.

Alipangua mpira ambao angeweza kuudaka kama lingekuwa pambano la Ligi Kuu. Ikapigwa kona ambayo ilizaa bao la kwanza la Morocco. Ni kitu kilichotazamiwa kwa kipa kama yeye ambaye naambiwa miezi michache iliyopita hakuwa hata na Pasipoti ya kusafiria. Hakujiandaa kwa mazingira haya.
Kitu cha pili, alikuwa na wasiwasi na mipira ya kuanzia nyuma. Katika mazingira kama yale hofu ilimshika na akajikuta anapiga mipira mbele ovyo huku kina Dickson Job wakiwa wamefungua nafasi wapasiwe.
Kina Job na Ibrahim Bacca wamezoea kucheza hivi na Djigui Diarra. Kina Mohamed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe wamezoea kucheza hivi na Moussa Camara. Yakoub alikuwa na wasiwasi mwingi kwa sababu labda huwa hachezi hivyo na walinzi wa JKT, pia labda huenda anacheza hivyo na walinzi wake wa JKT lakini siku ile wasiwasi ulimzidi. Hakutaka kusikia habari yoyote kuhusu pasi za kuanzia nyuma.

Licha ya hayo, pia hakuwa na makosa mengine. Kama angekuwa nayo nadhani mashabiki wangejazana mitandaoni kulaumu kwa nini kipa wa JKT Tanzania alipangwa katika pambano dhidi ya Morocco na sio Ally Salim wa Simba ambaye ameshawahi kudaka katika mechi za kimataifa za Taifa Stars na klabu yake ya Simba.
Sasa naamini Yakoub anaweza kuwa kipa namba moja wa Taifa Stars kama akijisikia kuwa hivyo. Baada ya mechi hii dhidi ya Morocco atakuwa ameondoa uoga.
Kuanzia sasa anaweza kudaka mechi nyingine za Taifa Stars na akaona maisha ni ya kawaida tu. Hapo atatuonyesha kipaji chake.
Pia najaribu kuangalia namna ambavyo anaweza kujitanua katika lango la Taifa Stars kupitia sera zetu mpya za timu kubwa.
Hawa rafiki zetu wa Kariakoo kwa sasa hawana imani na makipa wazawa. Makipa wao kwa sasa ni lazima wawe wageni. Halafu makipa wa pili ndio wanakuwa wazawa.

Kwa taifa kama letu ambalo linategemea zaidi wachezaji wa Taifa Stars kutoka Simba, Yanga na Azam inaweza kuwa rahisi kwa Yakoub kwa sababu wakubwa wameamua kwenda na makipa wa kigeni zaidi na ndiyo maana haikushangaza kuona mashabiki wa Simba na Yanga hawakulalamika kuona Yakoub yupo langoni.
Walifahamu wao wenyewe ndiyo chanzo cha kuwa na kipa wa JKT langoni.
Hawakushangaa pia kwa sababu wanafahamu kuwa nafasi ya kipa wa pili katika klabu zao kwenda moja kwa moja katika lango la Taifa Stars sio lazima sana.
Ndiyo maana hawakupiga kelele kwa Abuutwalib Mshery kutoitwa Stars au Ally Salim kutopangwa katika pambano hilo.
Tatizo kubwa la Yakoub linaweza kuwa kwa Aishi Manula kama akienda Azam kama inavyosemwa. Mkataba wa Aishi na Simba unakaribia mwisho na inadaiwa wamekubaliana kuachana mwishoni mwa msimu baada ya Aishi kuonekana kuwa Kirusi kwa watu wa Simba.
Aishi ambaye kwa muda sasa amekuwa ‘Tanzania one’ anaweza kurudi katika lango la Stars kama akirudi zake Azam na kuchanganya akili yake upya.

Huyu ndio tishio kwa Yakoub katika mazingira ya sasa ya mpira wetu. vinginevyo kama Azam inaweza kusajili kipa mwingine ambaye atakuwa mzuri kwa Aishi basi Yakoub anaweza kuwa Tanzania One kwa muda mrefu ujao.
Uzanzibar wake vipi? Sidhani kama kuna tatizo. Leo nataka kuwakumbusha Wazanzibar namna ambavyo wakileta bidhaa nzuri huku bara basi haibaguliwi kama ambavyo hapo katika miaka ya katikati walikuwa wanadhania hivyo.
Achilia mbali kocha mkuu, Hemed Morocco kuwa Mzanzibar lakini kulikuwa na wachezaji wanne kutoka Zanzibar katika kikosi dhidi ya Morocco ambao walianza mechi na hakuna ambaye alipangwa kwa sababu ya Uzanzibar wake. Kipa, Yakoub, Fei Toto, Ibrahim Bacca na Mudathir Yahaya.
Imenikumbusha wakati ule Zanzibar ilikuwa inaleta mafundi wengi katika timu ya taifa. Lakini hata lilipokuja suala la makipa kulikuwa na makipa kama Ally Bushiri na Riffat Said ambao walikuwa wanadakia Taifa Stars kutokana na uhodari wao na si Uzanzibar wao.
Eneo la ndani kulikuwa na akina Amour Aziz, Nassor Mwinyi Bwanga, Juma Bakari Kidishi, Seif Bausi na wengineo wengi ambao walitamba katika kikosi cha Taifa Stars kutokana nna uhodari wao na si upendeleo maalumu kwa sababu ya asili yao.