Kibadeni: Haikuwa rahisi kufika fainali 1993

Muktasari:
- Mechi hiyo ya kwanza ya fainali inapigwa kuanzia saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane, kabla ya kurudiana wikiendi ijayo Uwanja wa New Amaan, Zanzibar huku Kombe likiwa uwanjani.
TAKRIBAN miaka 32 imepita tangu Simba ilipocheza fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 wakati ambao Kocha Mkuu alikuwa Abdallah Kibadeni ‘King’, wakati timu hiyo leo itashuka tena uwanjani kucheza fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Mechi hiyo ya kwanza ya fainali inapigwa kuanzia saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane, kabla ya kurudiana wikiendi ijayo Uwanja wa New Amaan, Zanzibar huku Kombe likiwa uwanjani.
Wanasimba kwa jumla wamehamasika kwa rekodi hiyo iliyorudiwa na kikosi cha sasa kucheza fainali nyingine ya CAF, huku baadhi ya nyota na kocha waliopoteza katika fainali ya 1993 mbele ya Stella Abdijan ya Ivory Coast wametoa maoni yao juu ya mechi hizo za msimu huu.
Wameeleza namna wenyewe walikosea na kulikosa Kombe mbele ya ardhi ya nyumbani wakati huo Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipolazimika kuwakabidhi taji wageni walioshinda kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).
Kibadeni ambaye mbali ya kuwa kocha wa Simba, pia amewahi kuichezea timu hiyo, akishikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga hat trick katika Dabi ya Kariakoo akifanya hivyo Julai 19, 1977 wakati Wekundu hao wakiishindilia Yanga kwa mabao 6-0. Rekodi hiyo haijavunjwa hadi leo ikiwa ni takribani miaka 48.

Kitendo cha Simba kufika tena fainali katika mashindano ya CAF, imekuwa furaha kubwa kwa Kibadeni ambaye anasema:
"Najisikia furaha sana kuona historia inajirudia na mimi bado nipo, tuwaombee Simba na wachezaji wake waweze kutufikisha katika rekodi ambayo hatujawahi kuifikia.
"Ni miaka mingi sana imepita, vijana wana jukumu la kuhakikisha wanatupa furaha tuliyoikosa wakati ule kwani wana kikosi bora sana."
SIMBA IFANYE HIVI
Kibadeni anasema wakati wao wanacheza fainali mwaka 1993, ilikuwa ngumu sana kumsoma mpinzani kwa sababu huwezi kuona mechi za wapinzani au mbinu zao jambo ambalo liliwafanya kuwa wageni katika michezo ya kimataifa, lakini sasa teknolojia imekua, hivyo ni faida kwa Simba.
"Simba kitakachowaokoa sasa ni utandawazi ambao umekuwepo miaka ya hivi karibu, kocha Fadlu Davids na wachezaji kwa jumla wamepata muda wa kumsoma mpinzani vyema katika mechi zake zote kwa sababu wako mubashara.

"Faida nyingine ni kwamba Simba imekuwa na kocha toka mwanzo wa msimu, hivyo anajua kupanga kikosi chake vyema, wakati ule hata mimi sikuwa na shida kwa sababu ukiwajua wachezaji ni rahisi kama mwalimu kujua unaanza na yupi.
"RS Berkane ni timu nzuri sio ya kuidharau, nimeiona, ila Simba inaweza kupata matokeo mazuri kwani kanda zao zote wanazo wamewaona hivi karibuni kwenye michezo iliyopita," anasema Kibadeni na kuongeza;
"Kwa upana wa kikosi cha Simba wanachotakiwa ni kuipigania timu na sio kingine, wachezaji wa sasa ni tofauti na zamani, hawa wanapambana kujiuza wenyewe ndiyo maana utaona mtu anakomalia kufunga mpaka anakosa bao."
Mkongwe huyo anasema ni lazima Simba iwe makini katika fainali hiyo ya leo na hata mchezo wa marudiano, ili kutumia kila nafasi watakazotengeneza, pia kuzuia kwa akili na nidhamu.

"Wawe makini hasa kwenye kumalizia na kwenye kuzuia, unajua fainali hasa ni huo mchezo waliokwenda kuucheza ndiyo utatupa picha nzuri ya kuona tunafanyaje marudiano. Wajitambue na wajue kiu ya serikali, wanachama, viongozi wenyewe, mama mwenyewe amewapa mpaka ndege iwapeleke, sasa bado mtu unakwenda kuzubaa? Zamani tulikuwa tunasafiri mapema ili mkazoee hali ya hewa, nataka kombe hapa nyumbani, nchi inataka mafanikio makubwa.
"Tunachotaka na sisi tujulikane kama mabingwa wa Afrika, wenzetu walishapata ila sisi tulikuwa hatujapata, tunafika tu robo fainali au nusu fainali."
UJUMBE MUHIMU
Kibadeni anasema kwa mechi ya ugenini kuna kila sababu ya Simba kucheza kwa umakini kama walivyofanya mwaka 1993 kwa kutoka suluhu, lakini ikawa bahati mbaya kwa kupoteza nyumbani na kombe kuchukuliwa na wageni.

"Kwa kuwa timu inakwenda ugenini, tusiseme tunakwenda kujilinda ilimradi tuje kushinda nyumbani, hapana, mimi nafikiri mpango wa kwanza kila mmoja aambiwe jukumu lake analotakiwa afanye, asizidishe mambo, akizidisha anaweza kuvuruga, kwa hiyo kila mmoja anajua anapokuwa na mpira au timu yake inapokuwa na mpira kazi anayotakiwa kufanya ni kushambulia kutafuta nafasi na kufunga, sasa isifike wakati nafasi zinatafutwa halafu mtu anapoteza. Utulivu unatakiwa, kila mmoja atimize wajibu wake.
"Sisi tunataka kushinda kulekule kwao, Mungu atujalie tupate hata bao mbili au tatu, tukija hapa tutakuwa na njia nyepesi ya kulinda zile bao zetu na mashabiki tuliokuwa nao, uwanja tutaujaza, kwa hiyo ni suala tu la kuwaambia wachezaji na wao wamuombe sana Mwenyezi Mungu.
KINA MASATU NA WENZAO
Kibadeni katika kikosi alichokiongoza mwaka 1993, kilikuwa na wachezaji wengi mahiri, miongoni mwao ni George Masatu ambaye anasema anguko lao kubwa katika fainali waliyocheza ni kulewa sifa kulikowafanya kuona kama mechi wameshaimaliza baada ya ugenini kutoka 0-0.
"Ujue sisi tuliona matokeo ya ugenini yanatupa faida ya kuchukua kombe, kumbe mambo hayakuwa mepesi, wapinzani wakatubadilikia kwetu, tukakosa kombe.
"Wachezaji wa Simba nawasihi wacheze kama hawajafunga bao hata kama watakuwa wamewaburuza wapinzani, mabeki wazungumze kwani wao ndio wanaoiona timu nzima na kipa.

"Pia wasifunguke sana ugenini, ila wacheze kwa akili kubwa ya kujilinda na kuhakikisha Mwarabu hapiti, waache mambo ya kukaa mbali, kila mtu awe na kazi ya kumkaba mpinzani mmoja.
"Zamani tulikuwa tunasafiri kwa shida kidogo, kwa kutumia treni, hali ambayo ilikuwa ikiongeza uchovu wa safari, lakini hata maandalizi hayakuwa makubwa kiasi hiki.
"Kitu pekee ambacho mabeki wa Simba wanatakiwa kuwa nacho ni kuongea, sijui shida yao hasa ni nini kwani huwa hawana mawasiliano jambo linalowagharimu.
"Kipa anatakiwa kuongea na mabeki ili kuwajulisha na wengine kuhusu mbinu za wapinzani, kwa sababu wao ndio wanaowaona jinsi wanavyowashambulia na kusogea langoni.
Malota Soma alikuwepo katika kikosi hicho akicheza eneo la ushambuliaji, anasema: "Kwa sasa timu ina wachezaji wa kigeni wengi tofauti na sisi wakati wetu tulikuwa wazawa kwa hiyo tulikuwa tunacheza kutokana na uzalendo na mapenzi ya timu.
"Hakukuwa na mambo ya kuweka rekodi ili kupata jina la kujiuza mkataba unapomalizika kwenye timu husika, ndiyo maana kuna muda wananyimana pasi uwanjani, sio kwa sababu ya chuki ila ni mambo kama hayo.
"Tulipitia kipindi kigumu wakati tunacheza mashindano ya CAF, mechi ya kwanza tulicheza Msumbiji tukafunga bao la ugenini na pasi nilitoa mimi, baada ya kutoka hapo, ndipo tukafika fainali, wachezaji pia walikuwa wapya kama hivi sasa.
"Tulijitoa sana kwa sababu ya bonasi alizokuwa akitupa bosi wetu Azzim Dewji, tulifanya makosa madogo madogo ambayo yalitukosesha kubeba ubingwa.
"Kwa Simba ya sasa, wachezaji kwanza waende kwa kujituma zaidi wahakikishe hawapotezi mchezo wa kwanza kama sisi, pia wasijiamini kupitiliza jambo ambalo tunalijutia hadi hivi leo kwa sababu lilitupoteza.
"Kupangwa kwa mechi mchana kulituharibu, jua lilikuwa kali sana, kwa hiyo hawa vijana wetu waliopata nafasi ya kwenda kucheza fainali ninachowaomba kwanza wajitume hasa safu ya ushambuliaji.
"Simba kocha anacholalamika ni kutokutumia nafasi, wanapata nafasi 10 wanatumia mbili tu, ukiangalia ni mashindano ya kutaka kufunga, wakiacha ubinafsi watavunja historia yetu."
Beki wa zamani aliyeichezea Yanga na Simba, Godwin Aswile 'Scania' naye alikuwepo mwaka 1993, anasema, kipindi chao huduma ilikuwa ndogo kulinganisha na sasa wachezaji wanapata kila kinachotakiwa.
"Zamani wachezaji walifanikiwa kwa juhudi zao binafsi, kuhamasishana kufanya mazoezi kwa nguvu zote, lakini suala la ahadi hazikuwa zinatimia.
"Sijui wanashindwa wapi mastaa wa sasa, ila nina uhakika Simba sasa iko imara sana, huenda wakatuletea kombe ambalo sisi tulilikosa, kinachotakiwa ni wao kuwa watulivu tu.
"Mechi ya fainali 1993 tulijiamini sana na baadae tukakata tamaa na wapinzani wakatupiga, kukosa ushindi katika mechi ile ndiyo kitu pekee kilichowahi kuniumiza kwenye maisha yangu ya soka.
"Kila mchezaji alichanganyikiwa tulivyofungwa bao la kwanza, kwa sababu kila mtu alishapiga hesabu ya zawadi ambazo tuliahidiwa ya gari aina ya KIA, lakini Simba ijitume ifute aibu."