Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba katika fainali baada ya siku 11,494

SIMBA Pict

Muktasari:

  • Hii ni fainali ya kwanza kwa Simba katika michuano ya CAF tangu ilipocheza mara ya mwisho fainali ya Kombe la CAF iliyopigwa Novemba 27, 1993 dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kulala 2-0.

SIMBA inashuka uwanjani usiku wa leo ikiwa ugenini kuvaana na RS Berkane ya Morocco katika mechi ya kibabe ya fainali inayopigwa Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane, nchini humo.

Hii ni fainali ya kwanza kwa Simba katika michuano ya CAF tangu ilipocheza mara ya mwisho fainali ya Kombe la CAF iliyopigwa Novemba 27, 1993 dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kulala 2-0.

Michuano hiyo ya Kombe la CAF ilikuja kuunganishwa na Kombe la Washindi Afrika mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika ambalo Simba inacheza leo mechi ya kwanza ugenini kabla ya kurudiana nao wiki ijayo huku taji likiwa uwanjani.

Kama hujui, tangu Simba ilipocheza mechi ya mwisho ya fainali ya CAF mwaka 1993 zimepita takriban siku 11,494 sawa na miaka 31 na miezi mitano na siku 20 ndipo Wekundu wa Msimbazi hao wanatesti zali mbele ya RS Berkane, mabingwa wa michuano hiyo ya Shirikisho 2019-2020 na 2021-2022.

KIBA 02

Berkane yenye rekodi ya kubeba pia CAF Super Cup 2022, imecheza fainali zilizopita za Kombe la Shirikisho 2023-2024 na kupoteza mbele ya Zamalek ya Misri iliyotolewa robo fainali na Stellenbosch katika msimu huu. Stellenbosch ya Afrika Kusini ndiyo iliyotolewa nusu fainali na Simba.

Mechi ya leo inaleta kumbukumbu ya kusisimua kwa wachezaji, viongozi, makocha na kila Mwanasimba kwa kuzingatia kwa muda mrefu imekuwa ikikejeliwa na watani wao, Yanga iliyocheza fainali ya michuano hiyo misimu miwili iliyopita na kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria.

Yanga ilianza kwa kupoteza nyumbani kwa mabao 2-1 kisha kwenda kushinda ugenini kwa bao 1-0, hivyo matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2, lakini kanuni ya bao la ugenini likawabeba USM Alger na kutwaa ubingwa huo ikiwa kwenye ardhi ya nyumbani.

Rekodi zinaonyesha, tangu Simba irudi katika michuano ya kimataifa ya CAF mwaka 2018 ilikuwa haijawahi kuvuka hatua ya robo fainali katika misimu sita tofauti kabla ya safari hii kufanya kweli na sasa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo wanasikilizia mechi ya leo kujua wanatokaje nyumbani.

SIMB 01

Simba imecheza robo fainali nne za Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024, huku kwa Shirikisho Afrika imecheza 2021-2022 iliposhiriki baada ya kutupwa kutoka Ligi ya Mabingwa na kufika robo na kwa mara hii ya pili safari hii imejitutumua hadi hatua hiyo ya fainali.


SIO MECHI RAHISI

Licha ya morali kubwa waliyonayo wachezaji, makocha na wanasimba kwa jumla, ila kiuhalisia mechi ya leo siyo nyepesi, siyo kwa Simba tu bali hata kwa wenyeji Berkane ambao imekuwa na rekodi tamu katika michuano hiyo ikifika fainali nne, mbili ikibeba taji na mbili ikipoteza 2018-2019 na 2023-2024.

Pia ilishacheza fainali mbili za CAF Super Cup 2020 ikipoteza na ile ya 2022 ikitwaa taji, kuonyesha siyo timu nyepesi, lakini matokeo ya nyumbani kwa msimu huu na imecheza mechi sita, ikishinda zote na kufunga jumla ya mabao 18 na yenyewe kutoruhusu bao lolote.

Simba inayosaka heshima kwa mara ya kwanza baada ya kukwama 1993 katika Kombe la CAF, rekodi kwa mechi za ugenini zinaonyesha imeshinda mara moja tu dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia hatua ya makundi, lakini ikitoka sare tatu ikiwamo ile ya suluhu katika raundi ya pili dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, 1-1 katika makundi ilipoifuata Bravos ya Angola na suluhu nyingine na Stellenvbosch ya Afrika Kusini katika nusu fainali na kuchezea vichapo viwili kwa timu za Ukanda wa Afrika Kaskazini.

KIBA 04

Ilianza kwa kufungwa mabao 2-1 na CS Constantine katika hatua ya makundi, kisha kulala 2-0 kwa Al Masry zilipokutana kwenye robo fainali na leo itakuwa mechi ya saba kwa msimu huu na ya tano dhidi ya timu za ukanda huo wa Kaskazini maarufu kama Waarabu.

Hata hivyo, Simba nao haipo kinyonge kwa mechi sita za nyumbani, imeshinda zote kama ilivyo kwa Berkane, lakini ikifunga mabao 11 na kufungwa mawili tu kuanzia raundi ya pili, kitu kinachotoa ishara mechi ijayo haitakuwa ya kitoto kama ilivyo ya leo huko mjini Berkane.

Simba ilianza kwa kushinda 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, kisha ilipotinga makundi iliinyuka Bravos ya Angola bao 1-0, ikaipokea CS Sfaxien na kuifunga 2-1 na baadae kuizima CS Constantine kwa mabao 2-0 na kuichapa Al Masry pia 2-0 hatua ya robo fainali kisha kuing'oa kwa penalti na kuitungua Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa bao 1-0 kwenye nusu fainali mechi ikipigwa Zanzibar.


MAAJABU YA SIMBA

Tofauti na misimu mingine yote ambayo Simba imeshiriki michuano ya CAF, safari hii kwa mara ya kwanza imejikuta ikivaana na timu za nchi tano za Ukanda wa Afrika Kaskazini ikiwa na maajabu mengine ya Wekundu hao.

Kama hujui, ukanda huo unaundwa na nchi tano ambazo ni Morocco, Misri, Tunisia, Libya na Algeria, huku Simba ikivaana na timu zote za nchi hizo ikiwamo leo inapojiandaa kuvaana na RS Berkane ya Morocco.

SIMB 02

Kabla ya hapo ilianza kukutana na Al Ahli Tripoli ya Libya katika mechi ya raundi ya pili na kutoka suluhu ugenini kabla ya kushinda nyumbani mabao 31 na kutinga makundi na ilikutana na CS Constantine ya Algeria na kupoteza kwa mabao 2-1 ugenini kabla ya kushinda nyumbani 2-0.

Baada ya hapo ikaikaribisha CS Sfaxen ya Tunisia Kwa Mkapa na kushinda 2-1, kisha kurudiana nao mjini Tunis na kushinda 1-0 na kutinga robo fainali ilipoangukia mikononi mwa Al Masrya Misri ambao iliwafumua ugenini kwa mabao 2-0 kabla ya kulipa kisasi nyumbani kwa idadi kama hiyo.

Kwa vile matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 2-2, ilifuata mkono wa kupigiana penalti na Smba ikashindwa kwa mikwaju 4-1 na kutinga nusu fainali na sasa katika fainali inakutana na RS Berkane waliowahi kukutana katika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Shirikisho msimu wa 2021-2022.

Katika mechi hizo, Berkane ilianza kwa kushinda nyumbani kwa mabao 2-0 kisha kupoteza ugenini 1-0, hii ikiwa ni mechi ya tatu kwa leo kwa timu hizo kukutana, lakini ni mara ya kwanza kwao kuvaana fainali, huku kila moja ikipiga hesabu za ubingwa mapema kabla ya kurudiana wiki ijayo mjini Unguja.

SIMB 03

VITA NYINGINE

Ukiacha kila timu kuupigia hesabu ubingwa uliotemwa mapema na Zamalek ya Misri iliyotolewa nishai na Stellenbosch ya Afrika Kusini, lakini mechi hii ya fainali ya leo na ile ya marudiano wiki ijayo zote zina vita nyingine ya mastaa wa timu hizo wanaowania kumaliza vinara wa mabao msimu huu.

Oussama Lamlioui wa Berkane anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji kwa sasa akiwa na mabao manne akilingana na Ifeanyi Ihemekwele wa Enyimba ambaye timu yake ilitolewa makundi wanaomfukuzia kinara Ismail Belkacemi wa USM Alger ambao nao walitolewa mapema michuanoni.

Katika orodha hiyo wapo nyota wengine watatu wa Berkane, Issoufou Dayo, Youssef Zghoudi na Paul Bassene wenye mabao matatu kama waliyonayo Jean Charles Ahoua na Kibu Denis ambao wote hao leo watakuwepo uwanjani kuzipigania timu hizo katika mechi hiyo ya fainali ili kuona wanatokaje.

Mastaa wote hao kila wana dakika 180 za kujitetea kuanzia mechi ya fainali ya leo na ile ya marudiano ili kumaliza kama wababe wa kutupia kumpiku Ismail Belkacemi wa USM Alger anayemiliki matano, huku nafasi kubwa akiwa nayo Lamlioui mwenye mabao manne.

Nini kitakachotokea usiku wa leo? Bila shaka na kusubiri kuona simu 11,494 za Simba kurudi katika mechi nyingine ya fainali ya CAF mambo yatakuwaje!