LEMA: Beki wa Nabi anayesotea namba Pamba

Muktasari:
- Hata hivyo, licha ya kukosa nafasi kwenye mechi za Ligi Kuu, Lema amekuwa akitumiwa na kikosi hicho kwenye mechi za kirafiki na Kombe la Shirikisho (FA), ambako kwenye Shirikisho alianza katika ushindi dhidi ya Mashujaa FC (1-0) na Kiluvya United (3-0). Pia amekiwasha kwenye mechi tatu za kirafiki dhidi ya Alliance FC (4-0), Geita Gold (1-2) na Stand United ambayo kikosi hicho kilishinda 2-0 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
KIKOSI cha Pamba Jiji ya Mwanza kimeshacheza mechi 24 za Ligi Kuu Bara, lakini katika zote beki wake wa kulia, Yunus Lema hajaonja hata dakika moja akiishia benchini ama jukwaani kutokana na ushindani mkali wa namba kutoka kwa mabeki wazoefu, Mwaita Gereza na Keneth Kunambi, ambao wamekuwa wakipishana mara kwa mara.
Hata hivyo, licha ya kukosa nafasi kwenye mechi za Ligi Kuu, Lema amekuwa akitumiwa na kikosi hicho kwenye mechi za kirafiki na Kombe la Shirikisho (FA), ambako kwenye Shirikisho alianza katika ushindi dhidi ya Mashujaa FC (1-0) na Kiluvya United (3-0). Pia amekiwasha kwenye mechi tatu za kirafiki dhidi ya Alliance FC (4-0), Geita Gold (1-2) na Stand United ambayo kikosi hicho kilishinda 2-0 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Lema ambaye bado anasotea walau dakika moja ya kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, alijiunga na Pamba Jiji msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Mbuni ya Arusha, ambako alikuwa miongoni mwa vipaji vya kutazamwa kwa karibu. Licha ya Pamba Jiji kuongozwa na makocha wawili msimu huu ikianza na Goran Kopunovic na baadaye Fredy Felix ‘Minziro’, beki huyo ambaye ni zao la Future Star Academy ya Arusha ameshindwa kupata namba.
Mchezaji huyo alikaribia kujiunga na Yanga 2022/2023 baada ya kumkosha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasredine Nabi na Rais wa Yanga, Hersi Said ambao walifanya naye mazungumzo baada ya mchezo wa kirafiki kati ya Mbuni na Yanga Januari 19, 2022 jijini Arusha.
Mwanaspoti limefanya mazungumzo na beki huyo aliyeeleza mambo mengi ikiwamo dili la kwenda Yanga lilivyotibuka na kinachoendelea kwa sasa, huku akifunguka kuwa anaamini uamuzi wa kujiunga na Pamba Jiji bado ni sahihi kwake.
DILI LA YANGA
Lema ambaye alikiwasha katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga Januari 19, 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha licha ya Yanga kushinda mabao 2-0 lakini kocha Nabi na Rais wa Yanga, Eng. Hersi walimfuata na kumpongeza wakiahidi kuanza mazungumzo ya kumsajili.
Anasema dili hilo lilikwama baada ya Nabi kuondoka Yanga lakini ana matumaini kuwa uwezekano wa mpango huo kuendelea upo kwani bado ana uhusiano mzuri na viongozi wa Yanga.
“Baada ya mechi Nabi alinifuata akaniuliza umri wangu na kuniambia nina kipaji na kila kitu na anataka nije kwenye timu yake, alishuka pia Rais wa Yanga, Eng. Hersi ikawa ni mpango wa kwenda,” anasema Lema na kuongeza;
“Bahati mbaya msimu ulipoisha Nabi aliomba kuondoka japokuwa huo haukuwa mwisho mpaka sasa siwezi kuweka wazi ila bado kuna mipango inaendelea,” anasema.
Anasema kuwa Hersi alimtia moyo kuwa anaweza kucheza mpira kama akikubali kupata uangalizi mzuri na kijituma, basi Nabi angempenda na kumpa nafasi kwani alikuwa muumini wa vijana chipukizi akimtolea mfano wa Denis Nkane.
“Mpaka sasa nawasiliana naye (Eng. Hersi) na tunaongea mambo mengi, kwa sasa wacha tuone muda utaongea. Viongozi wa Mbuni walinisihi kuendeleza nidhamu ndani na nje ya uwanja na waliamini Yanga ingekuwa sehemu sahihi kwangu kuonyesha Watanzania kile nilichonacho,” anasema beki huyo.
KUTOCHEZA
Akizungumzia changamoto ya kutopangwa katika mechi zaidi ya 20 za Pamba Jiji tangu alipojiunga nayo Julai, mwaka jana anasema bado anaamini muda utafika wa kucheza na kuisaidia timu hiyo pale atakapohitajika.
“Ni kweli ni changamoto na mimi ni kijana mdogo nina malengo, kitu kikubwa ninachokiamini ni utafika muda wangu nitapata nafasi nitacheza na nitahakikisha nafanya vyema na kuipigania nembo ya klabu hii,” anasema Lema na kuongeza;
“Ndiyo mara ya kwanza naenda kujiunga na timu inayohusisha wachezaji wa kigeni nilihisi itakuwa ngumu kwa upande wangu ila nimekuja naona hakuna changamoto kuishi nao ukizingatia nafahamu Kiingereza kwahiyo hakuna changamoto kubwa,” anasema.
Beki huyo ambaye alianzia safari yake ya soka mwaka 2014 katika kituo cha Future Star cha jijini Arusha na baadaye kujiunga na Mbuni FC ambayo mwaka 2022 aliipandisha Ligi ya Championship, anasema licha ya kupata ofa sehemu mbalimbali lakini aliamini Pamba Jiji ndiyo sehemu sahihi kwake.
“Nilipata ofa Championship kama mbili na Ligi Kuu timu tatu ikiwamo Pamba naamini ni chaguo sahihi kwa kulinda kipaji changu. Ilikuwa faraja na furaha kwangu na nilihisi malengo yanaenda kutimia kwamba msimu huu lazima nicheze Ligi Kuu, kwahiyo ilinifanya nihamasike.”
MINZIRO HANA UTANI
Lema aliyedumu Mbuni tangu akiwa na miaka 16, anasema baada ya kutua Pamba Jiji amekuwa chini ya makocha tofauti, lakini Minziro ni tofauti kwani hapendi utani na mizaha.
“Hakuna utofauti mkubwa wa Goran Kopunovic na Minziro wote ni makocha bora na kila mtu amekuja kufanya kazi kwa nafasi yake. Minziro ni kocha mzuri hapendi utani wala mzaha mazoezini kwa sababu kila mtu yuko kazini ila nje ya uwanja ni baba mlezi na mshauri mzuri hata kwa Goran ilikuwa hivyo pia.”
KAPOMBE, CHILAMBO
Beki huyo wa kulia ambaye malengo yake ni kuifanya soka iwe sehemu ya maisha yake na kusaidia familia anasema anakoshwa na uwezo wa mabeki wenzake wazawa Shomari Kapombe wa Simba, Nathaniel Chilambo wa Azam na Mwaita Gereza wa Pamba Jiji.
“Wachezaji wanaonivutia binafsi na napenda wanavyocheza ni Shomari Kapombe, Mwaita Gereza na Nathael Chilambo hao ndiyo watu wanaonivutia wanavyocheza uwanjani,” anasema Lema.
KUIPANDISHA MBUNI
Lema anasema kati ya matukio ya kukumbukwa katika maisha yake ni Aprili 23, 2022 alipoipandisha daraja Mbuni kupitia Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, katika fainali ya nane bora ya First League dhidi ya Copco na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo wakipanda Ligi ya Championship.