Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo saba Dabi ya Kariakoo Kwa Mkapa

MAMBO Pict

LILE pambano lililokuwa linapiga danadana hatimaye lilifanyika juzi kwenye Uwanja wa Mkapa pale Temeke.


Katika mechi hiyo ya kiporo kilichoahirishwa mara mbili Machi 8 na Juni 15 Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 ya Pacome Zouzoua aliyefunga kwa penalti na baadae kutoa pasi kwa Clement Mzize aliyetupia chuma cha pili na Yanga kubeba ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo na taji la 31 la Ligi.



Nimegundua mambo saba baada ya kutulia katika televisheni nyumbani kwangu.


YANGA BORA KULIKO SIMBA

Kivuli ambacho mashabiki na viongozi wa Simba walijaribu kujificha ni pale Simba walipofika fainali za Shirikisho Afrika, huku Yanga wakishindwa kufika robo fainali za Ligi ya Mabingwa.

Lakini baada ya kufungwa mechi ya tano mfululizo na watani wao, mashabiki wengi wa Simba walijitokeza katika vipaza sauti vinavyozagaa nje ya uwanja wa taifa na kukiri Yanga ni bora kuliko wao.

Ndiyo, Yanga walikuwa wepesi. Walipasiana kwa haraka. Walikwenda mbele kwa haraka. Walikuwa bora wakati wakiwa na mpira na wakiwa hawana mpira.

Hata kama penalti ya Pacome Zouzoua isingetokea, hata kama Clement Mzize asingekimbia nyuma ya mabeki na kufunga, hata kama mpira ungeisha sare, Yanga walikuwa bora kuliko Simba.

MAMB 06

MPANZU NA SIMBA YAKE KILA MMOJA NA LAKE

Ilitajwa mtu tishio kwa Yanga alikuwa Ellie Mpanzu. Hakuwa na uhatari wowote ule. Zaidi ya kila kitu aliwakilisha alama ya mpira wa sasa wa Simba. Anao anao. Wachezaji wengi wa Simba eneo la mbele kila mchezaji alikuwa anacheza kivyake.

Wakati Yanga walikuwa wanacheza mpira rahisi, Simba walikuwa wanacheza mpira mgumu. Kila mtu alikuwa anajaribu kucheza kivyake.

Yanga walikuwa wamejaza viungo watatu mbele ya mabeki wao. Khalid Aucho, Mudathir Yahaya na Dube Abuya lakini bado Mpanzu alikuwa anajaribu kukatiza mbele yao na sio kupiga pasi rahisi ili apokee tena mbele.

MAMB 03

HAKUNA AZIZ KI, KUNA PACOME, CHAMA BENCHI

Simba inahitaji kukifumua kikosi chao. Nawafahamu mabosi wao ambao walimdharau Injinia Hersi Said wakati akijiingiza Yanga. walimdharau akiwa katika kamati, kisha akaenda kuwa Rais. Simba ina viongozi wakongwe kuliko Yanga.

Huwa wanaleta dharau huku wakikumbushana historia yao. Lakini Yanga wana Hersi. Mechi ya juzi Aziz Ki alikuwa Marekani akiwa bado hajamaliza msimu na Yanga lakini bado benchi kulikuwa na Mzize na Chama.

Wachezaji wenye ubora mkubwa ambao walistahili kuanza mechi. Simba wanahitaji ubora huu ndani na nje ya uwanja.

Msingi wa ubora huu ndiyo ambao umesababisha Yanga kumfunga Simba mara tano mfululizo.

Pacome aliichukua mechi akaiweka mfukoni. Alifanya alichojisikia huku Aziz akiwa Marekani na Chama akiwa benchi.

Mashabiki wa Simba waliokuwa katika vipaza sauti baada ya mechi kumalizika walisikika wakisema ‘Yanga hatuwawezi’ .Walikuwa sahihi.

MAMB 02
MAMB 02

WAARABU WAMETUMIWA NAULI KIHALALI

Mwamuzi Amin Mohamed Amin na genge lake walihalalisha maamuzi ya bodi ya ligi kuwatumia nauli waje kuchezesha Dabi ya Dar es salaam.

Maamuzi yao yalikuwa sahihi muda wote. Kwa waamuzi wetu, ile kadi ya njano aliyopewa Pacome kwa kujaribu kuiba penalti ingeweza kuwekwa penalti.

Na ile penalti ambayo Moussa Camara alimvamia Pacome basi mwamuzi wetu angeweza kupeta na kudanganya wachezaji walikuwa wamegongana.

Ilikuwa penalti halali. Pacome alivyouvusha tu mpira Camara hakupaswa kucheza na mwili wake.

Nilipenda pia jinsi Amin alivyokuwa anatoa ufafanuzi wa penalti yake kwa kina Tshabalala ambao walikuwa wanapinga. Tukiachana na hilo waamuzi wasaidizi walifurahisha zaidi namna walivyokuwa wanajua kucheza na mistari ya mtu wa mwisho lilipokuja suala la ‘offside’.

MAMB 05

SIMBA HAWATAMPENDA AHOUA KAMWE

Mpira wetu kivyetuvyetu. Siku hizi wachambuzi na mashabiki wameanza kujadili sana suala la namba za mchezaji. Mabao yake au pasi zake za mwisho.

Hapa ndipo Jean Charles Ahoua anapowachanganya mashabiki wa Simba. Ana namba nzuri lakini Simba wanahitaji kiungo mshambuliaji kama Fei Toto au kama Pacome.

Ambaye anaonekana anautawala mpira. Juzi Ahoua ameendelea kudhihirisha yeye ni kiungo mwenye namba nzuri lakini sio mtawala.

Simba inapitia sana pembeni kwa Mohamed Hussein na Shomari Kapombe. Juzi hawakupanda sana kwa sababu Yanga walikuwa wanatumia sana winga zao kutengeneza mashambulizi. Na hapo ndipo mashambulizi ya Simba yakafa.

Simba haimtegemei Ahoua katika kutawala mechi na kutengeneza mashambulizi. Tangu baada ya kumpoteza Chama haijapata kiungo wa mbele mwenye kuutawala mchezo na kutengeneza mashambulizi. Wamempata kiungo mwenye namba nzuri tu halafu basi.

MAMB 01
MAMB 01

MZIZE LAZIMA ANAWACHANGANYA AKILI MABOSI

Mzize lazima anawachanganya akili mabosi wake wa Yanga. Tazama namna alivyokimbia nyuma ya mabeki, tazama alivyoutuliza ule mpira, tazama alivyotupia mpira katika nyavu za Camara.

Kwa washambuliaji wa ndani wanaocheza nchini hakuna kama yeye. Alipoingia tu kipindi cha pili akaanza kuwapa shida Simba. Namna anavyokimbia kwa kasi, na namna anavyoimarika katika kumalizia.

Nasikia Yanga wanaweza kumuuza ili ampishe Jonathan Sowah wa Singida Black Stars. Ni biashara inayochanganya.

Unatoa mshambuliaji mzuri unaingiza mshambuliaji mzuri. Kama kila mtu akibakia alipo Yanga haiwezi kuathirika kwa lolote lile.

MAMB 06 (1)

MPIRA UMESHINDA, DABI ILIKUWA NA MVUTO

Mpira umeshinda. Raha ya mpira ni kuchezwa. Raha ya mpira ni mwamuzi kupuliza filimbi mpira uchezwe. Simba ilipoingia kupasha misuli moto, kisha Yanga nao wakaingia kufanya hivyo, ile ndiyo raha ya mpira. Mwarabu alipopuliza fimbi mpira uchezwe, ile ndiyo raha ya mpira.

Mpira hauchezwi katika ‘Tangazo kwa Umma’ pale Instagram. Simba amefungwa, Yanga bingwa, maisha yanasonga mbele.

Siku nyingi Yanga itafungwa na Simba itachukua ubingwa na maisha yatasonga. Kwani haijawahi kutokea huko nyuma? Imetokea mara kadhaa. Kilichotokea nje ya uwanja katika dabi hii kisirudiwe tena. Wanyarwanda walikuwa na msemo wao baada ya mauaji ya kimbari. ‘Never again’.

Ndiyo, kuanzia sasa na kuendelea tusilete tena habari ya mechi inayochezwa Dar es Salaam kuamuliwa na kikao cha Dodoma.