Morocco: Tishio jipya Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Safari yao kuelekea Kombe la Dunia 2026 imebeba matumaini makubwa kwa mashabiki wa Afrika na Waarabu kwa ujumla. Hii ni kwa sababu Morocco hawabebi tena jina la timu inayotafuta uzoefu, bali taifa ambalo tayari limeonyesha lina uwezo wa kuangusha mataifa makubwa duniani.
CASABLANCA, MOROCCO: Baada ya kuweka historia kubwa katika Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar na kuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia, sasa Morocco inaingia katika Fainali za 2026 kama moja ya mataifa yanayotazamwa zaidi.
Katika miaka michache iliyopita, Morocco imebadilika kutoka timu ya kawaida ya ushindani ndani ya Afrika na kuwa taifa linalotajwa sambamba na vigogo wa soka duniani. Wameonyesha uwezo mkubwa wa kiufundi, nidhamu, ubora wa benchi la ufundi pamoja na kizazi cha wachezaji wanaotikisa Ulaya.
Safari yao kuelekea Kombe la Dunia 2026 imebeba matumaini makubwa kwa mashabiki wa Afrika na Waarabu kwa ujumla. Hii ni kwa sababu Morocco hawabebi tena jina la timu inayotafuta uzoefu, bali taifa ambalo tayari limeonyesha lina uwezo wa kuangusha mataifa makubwa duniani.
Wakiwa na nyota kama Achraf Hakimi, Sofyan Amrabat, Yassine Bounou, Hakim Ziyech, Brahim Diaz pamoja na kizazi kipya cha vipaji vinavyoendelea kuchomoza Ulaya, Morocco wanaonekana kuwa moja ya timu hatari zaidi kutoka Afrika kuelekea mashindano hayo.
WALIVYOANZA KUCHOMOZA
Morocco ni miongoni mwa mataifa yenye historia kubwa ya soka ndani ya bara la Afrika. Baada ya kupata uhuru mwaka 1956, taifa hilo lilianza kuwekeza katika maendeleo ya soka na kujenga ushindani mkubwa ndani ya Afrika pamoja na kwa Waarabu.
Katika miaka ya 1960 na 1970, Morocco ilianza kujitengenezea jina kama moja ya timu bora Afrika Kaskazini. Ilitambulika kwa soka la pasi nyingi, nidhamu kubwa ya kiuchezaji pamoja na uwezo wa kiufundi.
Mwaka 1970, Morocco iliweka historia kwa kuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kufuzu Kombe la Dunia mara mbili tofauti baada ya kushiriki mashindano hayo nchini Mexico. Hilo lilikuwa jambo kubwa sana kwa kipindi hicho ambapo mataifa ya Afrika yalikuwa bado yanapigania kutambuliwa katika soka la dunia.
Miaka sita baadaye, 1976, Morocco ilitwaa ubingwa wake wa kwanza wa Mataifa ya Afrika (AFCON), mafanikio ambayo yaliiweka rasmi katika kundi la mataifa makubwa ya soka Afrika. Ubingwa huo uliifanya Morocco kuwa taifa linaloheshimiwa zaidi Afrika Kaskazini na uliweka msingi wa maendeleo ya soka yao.
HISTORIA ILIWEKWA MEXICO
Moja ya mafanikio makubwa katika historia ya Morocco yalitokea Kombe la Dunia 1986 nchini Mexico.
Katika mashindano hayo, Morocco iliandika historia kwa kuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kumaliza kinara wa kundi katika Kombe la Dunia. Ilikuwa kundi moja na England, Poland na Ureno, lakini ilionyesha kiwango kikubwa kilichowashangaza wengi duniani.
Morocco iliifunga Ureno mabao 3-1 katika moja ya ushindi mkubwa kwa taifa la Afrika katika Kombe la Dunia. Baada ya kufuzu hatua ya 16 bora, ilikutana na Ujerumani Magharibi na kupoteza kwa bao la dakika za mwisho, lakini ilikuwa tayari imeweka historia kubwa kwa bara la Afrika.
MIAKA YA CHANGAMOTO
Baada ya mafanikio ya miaka ya 1980, Morocco ilipitia vipindi vya kupanda na kushuka. Kulikuwa na nyakati ilizokosa mashindano makubwa na kushindwa kufikia matarajio ya mashabiki wake.
Hata hivyo, taifa hilo halikuacha kuwekeza katika maendeleo ya soka. Serikali, shirikisho la soka pamoja na akademi mbalimbali ziliendelea kuzalisha vipaji vipya. Miundombinu ya kisasa ilijengwa, vituo vya mafunzo vikaimarishwa na mfumo wa kuendeleza vijana ukawekwa katika kiwango cha juu.
Hatua hizi zilianza kuzaa matunda taratibu huku wachezaji wengi wa Morocco wakianza kucheza katika ligi kubwa za Ulaya.
WALIVYOTIKISA DUNIA
Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar liligeuka kuwa moja ya hadithi kubwa zaidi katika historia ya soka la Afrika.
Morocco iliingia bila kutajwa sana miongoni mwa timu zinazoweza kufika mbali, lakini ilibadilisha mtazamo wa wengi. Chini ya kocha Walid Regragui, ilicheza soka lenye nidhamu, mshikamano na moyo wa kupambana.
Katika hatua ya makundi, iliifunga Ubelgiji 2-0, Canada 2-1 na kutoa suluhu na Croatia, hivyo kumaliza ikiwa kinara kwa pointi saba. Baadaye iliiondoa Hispania kwa penalti 3-0 hatua ya 16 bora kabla ya kuifunga Ureno 1-0 robo fainali.
Hilo liliifanya Morocco kuwa taifa la kwanza Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia. Licha ya kupoteza 2-0 dhidi ya Ufaransa, iliondoka Qatar ikiwa imeandika historia.
MASTAA WA MOROCCO
Kikosi cha sasa kimejengwa juu ya wachezaji wenye uzoefu mkubwa Ulaya. Achraf Hakimi amekuwa sura ya timu kutokana na kasi na uongozi wake.
Yassine Bounou amejidhihirisha kama mmoja wa makipa bora duniani. Sofyan Amrabat amekuwa injini ya kiungo, huku Hakim Ziyech akibaki na ubunifu mkubwa.
Brahim Diaz naye ameongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji akiwa na ubora wa kufunga na kutengeneza mabao. Wengine ni Noussair Mazraoui, Nayef Aguerd, Azzedine Ounahi, Bilal El Khannouss, Youssef En-Nesyri na Ayoub El Kaabi.
SIRI YA MAFANIKIO
Moja ya sababu kubwa ya mafanikio ya Morocco ni uwekezaji katika akademi ya Mohammed VI Football Academy. Akademi hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha vipaji.
Pia kuna maboresho ya ligi ya ndani, miundombinu na mafunzo ya makocha, jambo lililoinua kiwango cha soka nchini humo.
TISHIO JIPYA
Tofauti na miaka ya nyuma, Morocco sasa inaingia Kombe la Dunia kama timu inayoheshimika duniani. Ina uwezo wa kudhibiti wapinzani wakubwa na kucheza kwa nidhamu kubwa.
Katika Kombe la Dunia 2026, Morocco inaingia ikiwa na ndoto ya kwenda mbali zaidi kuliko Qatar. Kundi lake lina Brazil, Scotland na Haiti.
NGUVU YA MASHABIKI
Mashabiki wa Morocco walikuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya 2022 kwa kujaa viwanjani na kutoa sapoti kubwa.
Katika 2026, wanatarajiwa tena kuwa na nguvu kubwa pamoja na sapoti ya Waafrika wengi duniani.
Morocco yapewa muda kuchagua kambi
Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limepewa muda wa ziada na FIFA kukamilisha maamuzi ya kambi rasmi ya timu ya taifa kuelekea Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Hatua hiyo imekuja wakati Morocco ikiwa na hesabu za mchezo wake wa kwanza dhidi ya Brazil utakaochezwa Juni 13, 2026, kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey.
Viongozi wa FRMF na benchi la ufundi la Walid Regragui wanaendelea kutathmini vituo mbalimbali vya mazoezi nchini Marekani kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Miongoni mwa mambo yanayoangaliwa ni umbali wa safari, hali ya hewa, ubora wa viwanja, vifaa vya tiba na kiwango cha faragha. Morocco inataka mazingira kama yale ya Qatar 2022 ambako walifika nusu fainali.
Katika maandalizi hayo, Morocco inaamini utulivu wa kambi utakuwa silaha muhimu, hasa ikizingatiwa watakutana na Brazil mapema kwenye hatua ya makundi.