Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndo DR Congo ya Fiston Mayele Kombe la Dunia

DR CONGO Pict

Muktasari:

  • Shirikisho lao la soka (FECOFA) lilianzishwa tangu 1919, kabla hata ya nchi kupata uhuru wake. Hii inaonyesha jinsi soka lilivyokuwa sehemu ya maisha ya jamii kwa muda mrefu. Baada ya kujiunga na FIFA 1962 na CAF 1963.

KINSHASA,  DR CONGO: WAKATI joto la Fainali za Kombe la Dunia 2026 likianza kupanda taratibu, macho ya wengi yakielekezwa Marekani, Canada na Mexico, msisimko wa soka unaanza kujijenga mapema kabla ya kipute chenyewe, ikiwa zimesalia siku 41.

Haya ni mashindano ambayo huleta pamoja mataifa bora, vipaji na hadithi zisizosahaulika kila baada ya miaka minne.

Katika kukupa uhondo wa fainali hizo, Mwanaspoti tunakuletea mfululizo maalum zenye uchambuzi, tukianza kwa kuyatazama kwa undani mataifa yote 48 yatakayoshiriki fainali hizo kutoka mabara yote sita yanayotambuliwa na FIFA ambayo ni Afrika (CAF), Ulaya (UEFA), Amerika Kusini (CONMEBOL), Asia (AFC), Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) pamoja na Oceania (OFC).

Tukichambua historia, walivyofuzu, nafasi yao katika michuano hiyo na mastaa waliobeba matumaini ya mataifa hayo.

Katika mfululizo huu, tunaanzia Afrika na moja kwa moja hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) maarufu kama Les Leopards,  timu yenye historia ndefu, mafanikio na safari ya kusisimua ya kurejea kwenye Kombe la Dunia baada ya miaka 52.

DR 01

NGUVU YA LES LEOPARDS

DR Congo ambayo ina mchezaji aliyewahi kutamba Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele akiwa na Yanga ni moja ya timu zenye hadhi kubwa katika soka la Afrika, ikiwa na utambulisho uliojengwa kwa miongo mingi.

Shirikisho lao la soka (FECOFA) lilianzishwa tangu 1919, kabla hata ya nchi kupata uhuru wake. Hii inaonyesha jinsi soka lilivyokuwa sehemu ya maisha ya jamii kwa muda mrefu. Baada ya kujiunga na FIFA 1962 na CAF 1963.

Uwanja wao wa nyumbani, Stade des Martyrs, umekuwa ngome muhimu kwa timu hiyo, ukibeba historia ya ushindi na presha kubwa kwa wapinzani wanaocheza mbele ya mashabiki wao. Kwa sasa, DR Congo wanashika nafasi ya 46 kwenye viwango vya FIFA.

DR 02

HISTORIA YA MAFANIKIO

Katika historia ya soka la Afrika, DR Congo ni moja ya mataifa yaliyowahi kutawala. Ushindi wao wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 1968 ulikuwa mwanzo wa enzi ya mafanikio ambapo walionesha kuwa wanaweza kushindana na timu bora barani humo.

Miaka michache baadaye 1974, walipata tena mafanikio hayo kwa kutwaa ubingwa wa pili wa AFCON. Katika fainali hiyo, walilazimika kurudia mechi baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Zambia, kabla ya kushinda marudiano kwa mabao 2-0.

Sababu ya fainali kurudiwa ilikuwa ni kanuni za mashindano ya wakati huo hakukuwa na mfumo wa mikwaju ya penalti kuamua mshindi, ilibidi mechi irudiwe siku mbili baadaye.

Mshambuliaji wao Ndaye Mulamba aliweka rekodi ya kufunga mabao tisa kwenye mashindano hayo rekodi ambayo bado haijavunjwa hadi leo.

Mbali na AFCON, DR Congo pia wamefanikiwa katika michuano ya CHAN, wakitwaa ubingwa mara mbili (2009 na 2016), jambo linaloonyesha kuwa hata vipaji vya ndani vina mchango mkubwa katika mafanikio yao.

DR 03

KOMBE LA DUNIA

DR Congo iliweka historia 1974 walipofuzu Kombe la Dunia wakiwa taifa la kwanza kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara kufanikisha hilo. Ushiriki huo ulikuwa hatua kubwa kwa soka la Afrika kwa ujumla.

Hata hivyo, mashindano hayo yalikuwa magumu sana kwao. Walipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi na kushindwa kufunga hata bao moja. Kipigo cha mabao 9-0 dhidi ya Yugoslavia kilibaki kuwa moja ya matokeo mabaya zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.

Licha ya matokeo hayo, uzoefu huo uliwapa somo kubwa na kuweka msingi wa maendeleo ya soka lao. Tatizo lilikuwa si vipaji, bali ni maandalizi, usimamizi na mifumo ya kisoka ambayo haikuwa imara wakati huo.

DR 04

WALIVYOPOROMOKA NA KUREJEA

Baada ya mafanikio ya miaka ya 1970, DR Congo walipitia kipindi kigumu kufuatia kushindwa kufuzu mashindano makubwa. Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1970 hadi 1990, walishindwa kurudi kwenye kiwango chao cha awali.

Hata hivyo, miaka ya 1990 ilileta matumaini mapya, walipofika robo fainali mara tatu katika AFCON (1992, 1994, 1996). Mwaka 1998 walimaliza nafasi ya tatu mafanikio makubwa kwa kizazi cha wakati huo.

Katika miaka ya karibuni, chini ya makocha tofauti, walijaribu kujijenga upya. Kipindi cha kocha Florent Ibenge ambaye kwa sasa ni kocha wa Azam FC kilileta mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kumaliza nafasi ya tatu AFCON 2015 na kufanya vizuri katika kufuzu Kombe la Dunia 2018 ingawa walikosa tiketi kwa tofauti ndogo sana.

DR 06

MAPAMBANO YA KIHISTORIA

Safari ya DR Congo kuelekea Kombe la Dunia 2026 ilikuwa ya kipekee na yenye presha kubwa. Walianza vizuri katika hatua ya makundi, wakishinda mechi muhimu dhidi ya timu kama Sudan, Togo na Sudan Kusin.

Hata hivyo, walikumbana na changamoto kutoka kwa Senegal, waliomaliza juu ya kundi hilo. Kumaliza nafasi ya pili kuliwalazimu kupambana zaidi kupitia hatua ya mtoano.

Katika hatua ya pili, walikutana na Cameroon na Nigeria timu zenye historia kubwa Afrika. Ushindi wao dhidi ya Nigeria kwa penalti ulikuwa moja ya matukio muhimu zaidi katika safari yao.

Hatua ya mwisho ilikuwa dhidi ya Jamaica katika mchujo. Mechi hiyo ilikuwa ngumu lakini walikushinda kwa bao 1-0 katika muda wa ziada, ushindi uliowapeleka moja kwa moja Kombe la Dunia.

DR 07

KIKOSI CHAO

Kikosi cha DR Congo kinachonolewa na Sébastien Desabre, raia wa Ufaransa ambaye alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo 2022, kinaonyesha wazi kuwa taifa hili lina hazina kubwa ya vipaji.  Wachezaji wengi wanacheza katika ligi za mataifa makubwa ya soka huko barani  Ulaya, jambo linaloongeza kiwango cha ushindani wa timu hiyo.

Lionel Mpasi (Le Havre), Timothy Fayulu (Noah), Matthieu Epolo (Standard Liège), Aaron Wan-Bissaka (West Ham United), Steve Kapuadi (Widzew Šódź), Axel Tuanzebe (Burnley), Arthur Masuaku (Lens), Joris Kayembe (Genk).

Rocky Bushiri (Hibernian), Chancel Mbemba (Lille), Dylan Batubinsika (AEL), Brian Bayeye (Villefranche), Edo Kayembe (Watford), Ngal’ayel Mukau (Lille), Nathanaël Mbuku (Montpellier), Samuel Moutoussamy (Atromitos), Brian Cipenga (Castellón), Theo Bongonda (Spartak Moscow), Meschack Elia (Alanyaspor).

Wengine ni Noah Sadiki (Sunderland), Charles Pickel (Espanyol), Grady Diangana (Elche), Cédric Bakambu (Real Betis), Fiston Mayele (Pyramids), Yoane Wissa (Newcastle United) pamoja na Simon Banza (Al Jazira).


TAKWIMU NA REKODI

DR Congo wana rekodi nyingi za kuvutia katika historia. Nahodha wao Chancel Mbemba ndiye mchezaji aliyewahi kuichezea timu ya taifa mechi nyingi zaidi, akiwa na zaidi ya mechi 100 za kimataifa (107), huku Dieumerci Mbokani akibaki kuwa kinara wa mabao wa muda wote wa taifa hilo akiwa amefunga mabao 22.

Timu pia ina historia ya ushindi mkubwa (10-1 dhidi ya Zambia) na uzoefu wa mashindano makubwa ya Afrika.

DR 08

MTIHANI MKUBWA

DR Congo wamepangwa katika kundi gumu pamoja na Ureno, Colombia na Uzbekistan. Hili ni kundi lenye changamoto kubwa kutokana na uwepo wa timu zenye uzoefu mkubwa wa Kombe la Dunia. Hata hivyo, hii ni fursa kwa DR Congo kupima kiwango chao dhidi ya waliobora duniani na kuonyesha kuwa wanaweza kushindana katika kiwango cha juu. Kwa ujumla, DR Congo wanaenda kwenye Kombe la Dunia 2026 wakiwa na historia kubwa, uzoefu wa changamoto na matumaini mapya.

Ni taifa lililowahi kutawala Afrika, likapotea kwa muda na sasa limerejea likiwa na kizazi kipya cha wachezaji wenye vipaji na njaa ya mafanikio.

Kwa Mwanaspoti, huu ni mwanzo tu wa ‘countdown’ yetu kuelekea Kombe la Dunia 2026. Tutaendelea kuchambua timu nyingine zote kwa undani, tukikuletea kila kitu muhimu kabla ya mashindano hayo kuanza Juni 11, 2026. Swali kubwa linabaki, Je, DR Congo wataishia kushiriki pekee au wataandika historia mpya ya kushtua dunia? Endelea kuwa nasi kwa uchambuzi zaidi.