Msengi: Kule nje narudi ila simba, yanga nafasi ipo tu

“NAJIPANGA upya.” Ndivyo anavyoeleza mchezaji, Ally Msengi aliyerejea tena Tanzania baada ya kwenye soka la kulipwa Afrika Kusini akiitumikia Stellenbosch ya Ligi Kuu nchini humo.

Nyota huyo aliyewahi kutamba na timu kadhaa za hapa nchini zikiwamo Mbao, Pamba na KMC huku akikumbukwa zaidi katika kikosi cha Serengeti Boys (U17) kilichoshiriki fainali za Afrika nchini Gabon amesaini mwaka mmoja wa kuichezea Tanzania Prisons, lakini ni kama kaziita mezani kimtindo Simba, Yanga na Azam.

Baada ya kurudi nchini, Mwanaspoti limezungumza kwa kina na nyota huyo na kueleza safari yake ya soka Afrika Kusini huku akiweka wazi amekuja kujitafuta upya kutokana na kupitia changamoto za hapa na pale zilizomfanya kutoonekana muda mrefu.


HAKUAMINI

Licha ya mafanikio ya kuonja hali ya hewa nje ya nchi, lakini Msengi anasema hakuamini kama itatokea nafasi ya kucheza huko japo amebarikiwa kipaji.

Anasema baada ya kupata ofa aliamua kukubali akiamini kilichotokea sio bahati mbaya, bali mapenzi na mipango ya Mungu.

“Kwanza nilisikia faraja nikaamini naweza kufanya kitu kwa sababu uwezo na kipaji ninavyo, nilijua naweza kufanya kitu kwa sababu Ligi Kuu nilishaicheza nikiwa na timu mbalimbali kama vile KMC na Mbao kidogo hivyo sikuwa na hofu,” anasema.


AANZA NA MSALA

Baada ya kutua katika kikosi hicho msimu wa 2020/2021, Msengi anasema aliikuta timu hiyo imebakisha mechi tisa tu huku akisotea benchi.

Licha ya changamoto hiyo ila baadae alianza kupewa dakika chache hadi msimu ulipoisha kutokana na kujiunga kipindi cha dirisha dogo la Januari kutokana na kukutana na nyota wenye majina makubwa na wazoefu zaidi yake waliokuwa wanamuweka benchi.

“Changamoto niliokutana nao nakumbuka nilipewa mechi yangu ya kwanza dhidi ya Mamelodi Sundowns na nilipewa pasi ila kwa bahati mbaya nikajichanganya nikapokonywa mpira na kufungwa bao 1-0, kiukweli ilinipa wakati mgumu sana kisaikolojia.”


KUJITAFUTA UPYA

Nyota huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi tatu uwanjani ikiwa beki ya kulia, kati na straika, anaeleza kwa sasa ni kama anaanza tena kujitafuta kutokana na kupotea uwanjani kwa msimu mzima.

Anasema baada ya kumaliza mkataba na Stellenbosch alijiunga na Moroka Swallows ila ilifungiwa kusajili na kukosa kucheza msimu mzima wa 2022/2023 ingawa hajakata tamaa kwani anaamini kupitia timu ya Tanzania Prisons atarudisha makali yake.

“Kukaa nje msimu mzima bila ya kucheza kama mchezaji ni pigo kubwa ila nashukuru nimekuja Prisons nikiamini ni sehemu salama itakayonirudisha katika ufalme niliokuwa nao mwanzoni japo natambua ushindani ni mkubwa sana kikosini,” anasema.


AZIOTA YANGA, SIMBA

Kiraka huyo anasema hakutarajia kurudi Tanzania mapema hivi ila kutokana na changamoto hizo hakuwa na jinsi ya kufanya, hivyo anaitumia Prisons kama daraja la kumrudisha tena kucheza soka la kulipwa kwani hayo ndiyo malengo aliyojiwekea.

“Mpira ndio maisha yangu hivyo lazima nipambane kupitia Prisons ili kufungua ukurasa mwingine mpya aidha wa kucheza kwa timu kubwa za Yanga, Simba na Azam au kurudi tena kimataifa ambako kila mchezaji anatamani kuchezea huko,” anasema.


MAISHA YA AFRIKA KUSINI

Mchezaji huyo anasema maisha ya Afrika Kusini hayatofautiani sana na Tanzania haswa kwa upande wa vyakula, japo kwenye soka kuna utofauti mkubwa kwa sababu hucheza mpira wa kasi na nguvu kubwa kutokana na ubora wa wachezaji waliopo huko.

Anasema maisha mengine aliyoona ya tofauti ni kuishi kama mpangaji kwani kila mchezaji hutoka nyumbani kwake tofauti na ilivyo Tanzania.

“Wanaoishi kambini ni zile klabu kubwa, ila pale Stellenbosch ni timu ya chuo na kuna nyumba ambazo tunakaa kwa kulipia. Kama huwezi unakaa nje ya chuo na wakati wa mazoezi unatokea kwako. Timu ndogo zinakutana siku moja tu kabla ya mchezo.”