PUMZI YA MOTO: Mpira unapoitia siasa majaribuni

Muktasari:
- Kwa kufanya hivyo, Iran linakuwa taifa la sita kujikatia tiketi yake baada ya Japan na New Zealand kupitia mchakato wa kawaida wa kufuzu, na Marekani, Canada na Mexico kama waandaaji. Hiyo inakuwa mara ya nne mfululizo kwao na ya saba kwa ujumla kufuzu Kombe la Dunia.
IRAN limekuwa taifa la sita kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kufuatia sare ya nyumbani ya mabao 2-2 dhidi ya Uzbekistan, Jumanne iliyopita.
Kwa kufanya hivyo, Iran linakuwa taifa la sita kujikatia tiketi yake baada ya Japan na New Zealand kupitia mchakato wa kawaida wa kufuzu, na Marekani, Canada na Mexico kama waandaaji. Hiyo inakuwa mara ya nne mfululizo kwao na ya saba kwa ujumla kufuzu Kombe la Dunia.

Kufuzu Kombe la Dunia ni kazi ngumu sana na ndiyo maana tangu mashindano hayo yaanze 1930 ni Brazil pekee ndiyo wamefuzu mara zote na angalau Ujerumani ambao walikosa mara moja, lakini siyo kwa sababu ya kushindwa kufuzu, bali siasa.
Ujerumani haikuruhusiwa kushiriki Kombe la Dunia 1950 kama adhabu ya kuleta chokochoko zilizosababisha Vita Kuu vya Pili vya Dunia.
Lakini kwa Iran kufuzu hakujawa kugumu kwao, lakini ugumu upo kwenye kushiriki mashindano yenyewe. Hii inatokana na ukweli kwamba mashindano hayo yanakuja katika wakati ambao ni mgumu kisiasa kuanzia kwa waandaaji hadi timu shiriki kama Iran. Kufuzu kwa Iran kunakwenda kuongeza chumvi kwenye kidonda cha siasa ambacho tayari kina pilipili.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na mmoja wa waandaaji, Marekani, siyo mzuri tangu 1979 pale utawala wa Kiislamu chini ya Ayatollah Khomenei ulipoindua serikali ya Mfalme Shah ambayo ilikuwa kipenzi cha Marekani. Lakini hata hivyo, sasa mataifa hayo yameingia kwenye sura mpya ya uhusiano mbaya.

Rais Donald Trump ameonekana kuwa na msimamo mkali zaidi dhidi ya Iran juu ya mipango ya nchi hiyo kuzalisha mabomu ya nyuklia. Rais Trump anaelekea kuwapiga marufuku raia wa Iran kuingia Marekani kama sehemu ya vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya Bara la Asia.
Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni na utawala wa Trump, Iran imeorodheshwa miongoni mwa mataifa 10 yakiwemo Afghanistan, Syria, Cuba na Korea Kaskazini ambayo yako hatarini kuzuiwa kabisa raia wake kuingia Marekani. Hii ina maana kwamba timu ya taifa ya Iran iko hatarini kutocheza mechi zake za hatua ya makundi nchini Marekani.
Wanaweza kupangiwa kucheza Canada au Mexico. Lakini endapo watavuka hatua hiyo hawatakuwa na namna nyingine zaidi ya kuingia Marekani kwa sababu ndiko mechi zote za baada ya makundi zitafanyika. Sasa itakuwaje hapo?

Huu ni mtihani wa kwanza unaomkuta ndugu yetu siasa kutoka kwa ndugu yetu mpira. Wakati hilo likiwatatiza wengi, kuna mtihani mwingine uko hapo. Huu ni mvutano mkubwa wa kisiasa baina ya waandaaji yaani Marekani, Canada na Mexico.
Marekani ipo kwenye uhusiano mbaya zaidi kihistoria na majirani zake hao.
Rais Trump ambaye ndiye kinara wa mtafaruku wote huu ameonyesha nia ya kuichukua Canada na kuifanya kuwa sehemu ya Marekani. Hii imewakera sana Canada na kujikuta wakiingia kwenye vita vya maneno na Marekani.
Juu ya hilo kuna vita nyingine kubwa ya ushuru wa forodha ambao Marekani imeuweka dhidi ya bidhaa zote kutoka Mexico na Canada kuingia nchini humo. Ushuru huo umewakera viongozi wa mataifa hayo na kujikuta wakichanganyikiwa. Lakini licha ya hali hiyo tete, bado mataifa hayo yanatakiwa kuweka kando tofauti zao na kuandaa Kombe la Dunia kwa pamoja huku wakilazimika kuwapokea watu wasiowapenda kama Iran kwa Marekani.

Hapo ndipo nguvu ya mpira inapojidhihirisha bayana na kuishinda siasa. Lazima Kombe la Dunia litafanyika na lazima Iran watakwenda. Na kama wataenda na kuvuka hatua ya makundi, maana yake ni lazima watacheza Marekani. Na kama itakuwa hivyo maana yake ni lazima Marekani watoe visa (ruhusa ya kuingia) kwa watu wote kutoka Iran watakaokuja kwenye mashindano wakiwemo wachezaji, makocha viongozi na hata mashabiki.
Na hii ikitokea maana yake siasa itakuwa imezidiwa nguvu na mpira...usichezee nguvu ya mpira hata kidogo. Mpira ulisimamisha vita 2010 kule Ivory Coast. Ulisimamisha vita 1996 nchini Liberia. Ulisimamisha vita vya Biafra 1969 nchini Nigeria. Huu ndiyo mpira.