Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RUPIA: Straika wa boli asiye na bahati ya penalti

RUPIA Pict

Muktasari:

  • Rupia anashika nafasi ya pili kwa nyota wa kikosi hicho waliofunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu Bara, baada ya kuweka kambani 10, akizidiwa bao moja na mshambuliaji mwenzake raia wa Ghana, Jonathan Sowah aliyefunga 11 hadi sasa kikosini.

UNAPOTAJA washambuliaji watano bora katika Ligi Kuu Bara msimu huu, hutoacha kulitaja jina la mshambuliaji nyota wa Singida Black Stars, Mkenya Elvis Rupia kutokana na kiwango kizuri anachoendelea kukionyesha tangu atue hapa nchini.

Rupia anashika nafasi ya pili kwa nyota wa kikosi hicho waliofunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu Bara, baada ya kuweka kambani 10, akizidiwa bao moja na mshambuliaji mwenzake raia wa Ghana, Jonathan Sowah aliyefunga 11 hadi sasa kikosini.

Rupia amezidiwa pia na Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 12, sambamba na Prince Dube wa Yanga, huku kinara wa ufungaji hadi sasa ni Clement Mzize pia wa Yanga aliyetupia kambani 13.

Licha ya ujio wa Sowah aliyejiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Januari 2025, ila Rupia ameendelea kuonyesha kiwango kizuri kwa muda anaocheza, jambo linalomtofautisha na baadhi ya washambuliaji wanaoshindwa kupambania nafasi.

Rupia alijiunga na kikosi hicho msimu wa 2023-2024 akitokea Police FC ya Kenya na alifunga mabao 27 na kuivunja rekodi iliyochukua miaka 47, katika Ligi Kuu ya Kenya ya Maurice Ochieng aliyefunga 26 mwaka 1976 akiwa na Gor Mahia.

RUPI 01

Katika msimu wa kwanza, Rupia alichezea timu mbili tofauti akianza Singida Fountain Gate kisha dirisha dogo akatua Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na kwa msimu mzima alifunga jumla ya mabao sita akiwa na klabu zote mbili.

Katika misimu yote tangu atue hapa nchini, huu ndiyo msimu bora kwa Rupia Ligi Kuu Bara kutokana na idadi kubwa ya mabao aliyofunga na kijumla amechangia 12, baada ya kufunga 10 na kuasisti mawili kati ya 40 ya timu hiyo nzima.

Uwepo wa Sowah na Rupia umewafanya nyota hao kuunda safu bora ya ushambuliaji kikosini humo na kijumla wamechangia mabao 23 kati ya 40 ya timu hiyo nzima, hali inayoonyesha wazi ni miongoni mwa washambuliaji bora msimu huu katika ligi.

RUPI 02

NUKSI YA PENALTI

Licha ya ubora wa kufumania nyavu kwa nyota huyo, ila amekuwa na gundu la kukosa penalti msimu huu, kwani kati ya nane ambazo kikosi hicho imezipata, imekosa mbili tu pekee, ambazo zote ni za Rupia katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara.

Katika penalti hizo, Rupia alianza kukosa katika mechi dhidi ya KenGold, Desemba 24, 2024, Singida iliposhinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida, ingawa alifunga bao moja huku lingine likifungwa na kiungo, Josephat Arthur Bada.

Penalti nyingine, ni ile ya kichapo ilichokipata Singida cha 2-0 kutoka kwa KMC, yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Oscar Paul aliyefunga dakika ya 35 na 40, mechi ikipigwa Uwanja wa KMC Complex Mwenge, Februari 10, 2025.

Wengine waliopata ni Marouf Tchakei katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0, dhidi ya Namungo FC, Oktoba 20, 2024, kisha akafunga tena nyingine kwenye sare ya 2-2, mbele ya Kagera Sugar, Februari 7, 2025.

Nyota pekee aliyefunga penalti nyingi kikosini humo ni Jonathan Sowah aliyefunga nne kati ya nane, akianza na ya sare ya 2-2 dhidi ya Pamba Jiji Februari 23, 2025, kisha akafunga walipoichapa Mashujaa FC 3-0, Februari 26, 2025.

Nyingine aliyofunga ni ya kichapo ilichokutana nacho Singida cha kuchapwa mabao 2-1, dhidi ya Coastal Union, Aprili 10, 2025, kisha akafunga tena wakati kikosi hicho kilipoibuka na ushindi wa 3-0, mbele ya Tabora United, Aprili 19, 2025.   

RUPI 03

MGAWANYO WA MABAO

Katika mabao 10 aliyofunga ya Ligi Kuu Bara hadi sasa nyota huyo, timu tatu amezifunga sita ambazo ni KenGold, Azam FC na Dodoma Jiji ambazo amefunga mawili kwa kila mmoja, huku KMC, JKT Tanzania, Tabora United na Mashujaa FC akifunga moja moja.

Rupia alianza kuifunga KenGold katika mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo Singida ilishinda mabao 3-1, Agosti 18, 2024, kisha akaifunga tena raundi ya pili zilipokutana kwenye Uwanja wa Liti Singida, iliposhinda pia 2-1, Desemba 24, 2024.

Timu nyingine aliyoifunga mara mbili ni Azam FC akianza katika kichapo cha Singida ilichokutana nacho cha kuchapwa mabao 2-1, Novemba 28, 2024, kisha akalipa kisasi tena kwa kuifunga bao 1-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Aprili 6, 2025.

Nyingine ni Dodoma Jiji aliyoifunga mabao yote mawili ya dakika ya 8 na 15 ya ushindi ilioupata Singida wa 2-1, Desemba 12, 2024, kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida, huku la 'Walima Zabibu', likifungwa na nyota, Yassin Mgaza dakika ya 58.


MSIKIE OUMA

Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma anasema ujio wa Sowah umeongeza ushindani katika kikosi hicho, licha ya kukiri kuna wakati ni mgumu pia kufanya kazi na jopo la wachezaji bora kwa sababu huwezi kumridhisha kila mmoja wao.

"Unapokuwa katika timu yenye malengo makubwa ni lazima kama mkuu wa benchi la ufundi ukubaliane na hali iliyopo, Sowah na Rupia wameonyesha ubora mkubwa, ingawa sio wao pekee kwa sababu wanacheza kwa kushirikiana na wengine," anasema Ouma.

RUPI 04

Wasifu:

Jina: Elvis Baranga Rupia

Kuzaliwa: Apr 12, 1995

Mahali: Nakuru

Uraia: Kenya

Nafasi: Mshambuliaji

Klabu: Singida BS


Alikopita: Muhoroni, Nzoia Sugar, Power Dynamos, Wazito, AFC Leopards, Bisha, Polisi Kenya na Fountanin Gate


27 Mabao aliyofunga akiwa na Polisi Kenya na kuvunja rekodi ya miaka 47 katika Ligi Kuu Kenya.


17 Idadi ya mabao aliyowahi kufunga katika Ligi Kuu Kenya akiwa na Nzoia Sugar na AFC Leopards.


2023 Mwaka ambao straika huyo Mkenya alivuka mpaka na kuja kucheza soka nchini Singida FG.