Serikali yajivua lawama ‘Kariakoo Derby’

Muktasari:
- Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kanuni zinamfunga mikono kulisemea jambo la mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga ‘Kariakoo Derby’ hadharani wakati yeye si mtoa maamuzi.
Serikali imejiweka kando kwenye Dabi ya Simba na Yanga ikisema haiwezi kuingilia mipango ya mpira kwa kuwa inakiuka sheria za ligi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi wakati akihitimisha hoja yake ya maombi ya fedha kwa mwaka 2025/26 ambapo ameomba Sh519.66 bilioni.
Awali wabunge walipokuwa wkaichangia bajeti hiyo walionyesha hisia za kutaka kujua nini kilichojificha nyuma ya pazia kuanzia mazungumzo na uamuzi ambapo walimtaja Waziri Kabudi kuwa, alishiriki vikao vya mapatanisho lakini hajawahi kusema chochote.
Kukataliwa kwa hoja hiyo kulianzia katika mchango wa Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali alipokuwa akichangia kuhusu jambo hilo, ambapo Naibu Spika Mussa Zungu alizuia akisema jambo hilo, lipo mahakamani.
“Mheshimiwa Gulamali, nakuomba ujielekeza katika mambo ya kisera, kanuni ya 81 inakuzuia kusema jambo ambalo linasubiri uamuzi wake na kama utabisha nitakuingiza kwenye kanuni ya 84 halafu unajikuta huna hata sifa za kugombea,” amesema Zungu.
Aliposimama Waziri alizungumza kwa ufupi akasema; “Suala la dabi siwezi kulizungumzia hapa, jambo hilo liko mahakamani na kanuni zinanifunga hapa.”
Hata hivyo, kwenye upitishaji wa vifungu jambo hilo liliibuka na kuzua mvutano tena baada ya Wabunge Costantine Kanyasu (Gaita Mjini) na Joseph Msukuma (Geita Vijijini) waliibua tena, lakini Naibu Spika aliwazuia akisema hakuna mwenye mamlaka ya kuzungumzia.
Hata hivyo, Msukuma alimuuliza Naibu Spika kwamba Waziri na Naibu wake, Hamis Mwinjuma walikwenda kufanya nini katika kikao ikiwa wanakingiwa kifua wasiulizwe, wakati hawakuwa wachezaji wala viongozi wa michezo kama haitakiwi kuulizwa mbele ya kadamnasi.
Dabi ya Kariakoo ilishindwa kuchezwa Machi 8 baada ya kuahirishwa saa chace na Bodi ya Ligi, ikiwa muda mchache tangu Simba ilipotangaza isingechezwa kwa kuzuiwa kufanya mazoezi na wanaodaiwa makomandoo wa Yanga, siku moja kabla ya mechi.
Hata hivyo, jana Bodi ilitangaza tarehe mpya ya mechi kuwa itapigwa Juni 15, huku Yanga ikitishia kutocheza kwa kutokuwa na imani na mabosi wa TFF na Bodi kwa walichokidai wana viashiria vya upendeleo uliowafanya wakimbilie CAS iliyowarudisha katika mamlaka za ndani kwanza.