Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu avujisha meseji za Orlando, Tshabalala naye kumekucha

Muktasari:

  • Timu hiyo imefuzu fainali mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipoasisiwa 2004 kwa kuunganishwa Kombe la CAF na la Washindi, na imepangwa kukutana na RS Berkane kati Mei 17 na 25 ambapo mshindi wa jumla atabeba taji hilo lililotemwa na Zamalek ya Misri.

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amefichua ujumbe alioupokea kutoka kwa mmoja wa maofisa wa juu wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini baada ya kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hiyo imefuzu fainali mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipoasisiwa 2004 kwa kuunganishwa Kombe la CAF na la Washindi, na imepangwa kukutana na RS Berkane kati Mei 17 na 25 ambapo mshindi wa jumla atabeba taji hilo lililotemwa na Zamalek ya Misri.

Simba itaanzia ugenini kabla ya kumalizia nyumbani Mei 25 ikiwa na kazi ya kulipa kisasi dhidi ya timu hiyo ya Morocco iliyowahi kukutana nayo katika makundi ya michuano hiyo msimu wa 2021-2022 na kila moja kushinda mechi ya nyumbani.

Simba ilitinga fainali baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, na Fadlu ameliambia Mwanaspoti kuwa amepokea ujumbe wa kusisimua kutoka kwa kigogo wa Orlando.

Kocha huyo alifichua maneno yenye hisia kutoka kwa ofisa huyo aliyemkumbusha kumbukumbu ya machungu ya 2022. Hata hivyo, Fadlu hakumtaja kigogo huyo aliyemzindua. “Nilipokea ujumbe kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu Orlando Pirates. Ujumbe ulisema, “kumbuka ni Berkane waliotufunga kwa mikwaju ya penalti.” Fadlu alisema.

Kauli hiyo iligusa hisia za kocha huyo kwa vile Fadlu alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Orlando Pirates lililofungwa na RS Berkane katika fainali ya michuano hiyo 2022, baada ya pambano kali lililomalizika kwa penalti, baada ya Orlando kuifunga Simba robo fainali.

“Mchezo ule bado unanikumbusha maumivu. Tuliifunga Simba katika robo fainali. Tukaitoa Al Ahli Tripoli halafu tukapoteza kwa penalti dhidi ya Berkane. Ni timu ambayo imeimarika sana. Na kocha wao, Mouin Chaabani tulishamkabili msimu uliopita akiwa na Raja Casablanca,”  aliongeza Fadlu.

Kocha huyo alisema ujumbe huo ulienda sambamba na kukumbushwa kujiandaa kwa mechi ya ugenini dhidi ya timu hiyo ya Morocco ambayo haijapoteza mchezo wowote msimu huu katika michuano ya CAF, ikifunga mabao 18 bila kuruhusu bao nyumbani.

Rekodi zinaonyesha katika mechi sita za nyumbani msimu huu kuanzia raundi ya pili, Berkane imeshinda zote ikianza kuifunga Dadje ya Benin 5-0 kisha makundi ikatoa vichapo kwa CD Luanda ya Angola 2-0, ikaizaba Stade Malien ya Mali 1-0 na kuinyoa Stellenbosch 5-0. Hatua ya robo fainali iliifunga Aserc Mimosas ya Ivory Coast kwa bao 1-0 na nusu fainali ikaifunga CS Constantine ya Algeria kwa mabao 4-1.

Wakati kwa mechi za ugenini, mabingwa mara wa michuano hiyo walicheza pia sita na kushinda nne wakipoteza moja na kutoka sare moja, wakifunga mabao matano na kufungwa mawili kuonyesha sio timu nyepesi na Fadlu na mastaa wa Simba wana kazi kubwa ya kufanya ili kubeba ubingwa.

Kwa mechi ya raundi ya pili, Berkane ilianza ugenini ikaifunga Dadje mabao 2-0 kisha makundi iliilaza Stellenbosch 3-1, ikailaza Stade Malien 1-0, huku ikilazimishwa suluhu na CD Luanda, wakati hatua ya robo fainali iliishinda Asec 1-0 na nusu fainali ndipo ikalala 1-0 kwa Constantine.

Hivyo, Fadlu anajua anakutana na timu ngumu na anapaswa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini na hata kama watapoteza isiwe mabao mengi.

“Tunajua kuna kazi kubwa mbele ya Berkane, lakini ujumbe nilioupata kwa bosi wangu wa zamani wa Orlando umenikumbusha kitu cha kuhakikisha tunafanya kila kitu kupata matokeo mazuri - zaidi ugenini ili mechi ya marudiano nyumbani isiwe ngumu,” alisema Fadlu ambaye hii ni nafasi nzuri kwake kulipiza kisasi kwa Berkane na kuandika historia mpya ya kuipa Simba ubingwa wa Afrika.

Ingawa Simba imepata mafanikio makubwa kimataifa, Fadlu hajapoteza mwelekeo katika mbio za Ligi Kuu Bara anaochuana na Yanga, lakini pia akiiwezesha Simba kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ikijiandaa kuvaana na Singida Black Stars.


TSHABALALA NA KAIZER

Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imefufua tena nia ya kumsajili beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ikiwa ni mpango mbadala endapo itashindwa kumalizana na chaguo lake la kwanza, Fawaaz Basadien kutoka Stellenbosch.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, Chiefs bado inamtambua Basadien kama lengo kuu, lakini sintofahamu kuhusu upatikanaji wake imeilazimu kuangalia machaguo mengine, huku uzoefu wa Hussein katika mashindano ya Afrika ukiivutia.

Hatua hiyo inaendana na mkakati wa Kaizer Chiefs kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hasa safu ya ulinzi upande wa kushoto. Hussein ameonyesha kiwango bora akiwa na Simba katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, na mchango wake umeisaidia timu hiyo kuichapa Stellenbosch timu anayochezea Basadien.

“Kaizer Chiefs wanataka Tshabalala aungane na kocha Nasreddine Nabi. Wanamtaka awe suluhisho la tatizo lao la beki wa kushoto, kwani Bradley Cross haonekani kama suluhisho la muda mrefu,” chanzo kiliongeza.

Iwapo Chiefs itafanikiwa kumsajili beki mpya wa kushoto huenda ikaachana na baadhi ya wachezaji waliopo katika nafasi hiyo. Majina ya Edmilson Dove na Zitha Kwinika yanatajwa kuwa miongoni mwa wanaoweza kuachwa. Kwa sasa, Kaizer Chiefs inaonekana kuwa na dhamira ya dhati kupata beki wa kushoto mwenye uzoefu na anayekidhi viwango vya ushindani wa kimataifa. Iwe ni Basadien au Tshabalala mabadiliko makubwa yanatarajiwa msimu ujao.