Simba yaitandika JKT, yachungulia ubingwa WPL

Muktasari:
- JKT ikiwa nyumbani imetandikwa mabao hayo na kushushwa kileleni ilipokuwa na pointi 37 na sasa Simba iko nafasi ya kwanza ikifikisha pointi 40.
KATIKA kuhakikisha Simba Queens inakaa kileleni na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuutetea ubingwa wa Ligi ya Wanawake imeitandika JKT Queens mabao 4-3.
JKT ikiwa nyumbani imetandikwa mabao hayo na kushushwa kileleni ilipokuwa na pointi 37 na sasa Simba iko nafasi ya kwanza ikifikisha pointi 40.
Mchezo wa kwanza zilipokutana timu hizo msimu huu Simba ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya 1-1.
JKT ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 11 likifungwa na beki Anastazia Katunzi baada ya kipa wa Simba, Janet Shija kumchezea faulo ndani ya boksi winga wa wanajeshi hao, Winifrida Gerald.
Dakika sita baadae Simba ikapata penati baada ya beki wa JKT, Janeth Pangamwene kuushika mpira ndani ya boksi.
Simba iliendelea kupeleka mashambulizi kwa wanajeshi hao na dakika 27 Shikangwa akaipa uongozi timu hiyo baada ya kumalizia krosi iliyochongwa na Asha Djafar.
Hadi mapumziko JKT ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1 lakini mabadiliko yaliyoyafanywa dakika ya 35 ya kumtoa Kija Hassan na kumuingiza Christer Bazil yaliipa ahueni timu hiyo hasa eneo la kati lililoonekana lina mapungufu.
Dakika 57 baadae Donisia Minja wa JKT alifunga bao la pili kwa shuti lililoonekana halina madhara kwa kipa Wilfrida Cedar aliyeingia kipindi cha pili baada ya Shija kuumia na kufanya mzani kuwa 2-2.
Dakika ya 70 kipa wa Simba akafanya makosa ya kutoka langoni na Jamila Rajabu akamaliza pasi iliyotolewa na Stumai Abdallah.
Mchezo huo mkali uliendelea na Simba ikijaribu kupambana kupata bao na dakika 73 Vivian Corazone akafunga bao la tatu kwa Simba.
Dakika ya 78 Shikangwa akazima matumaini ya JKT kuendelea kusalia kileleni baada ya kufunga bao la nne lililodumu kwa dakika zote 90 zilizoipa pointi tatu Simba.
Hata hivyo mchezo huo ulikuwa muhimu kwa Shikangwa ambaye yuko kwenye mbio za kuwania nafasi ya kiatu akifunga hat-trick na kumfanya afikishe mabao 22 nyuma ya Stumai mwenye mabao 26.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi, Azishi Kondo alisema wachezaji wa timu hiyo walifanya makosa na kubweteka baada ya kupata bao la tatu.
"Tulikuwa vizuri lakini ndio hivyo makosa yametugharimu, tulikuwa nyuma tukarejesha mabao baadae tukafanya makosa wenzetu wakatumia nafasi hiyo," alisema Kondo.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Yussif Basigi alisema hana kikubwa cha kusema zaidi ya kuwapongeza wachezaji wa timu hiyo.
"Mchezo ulikuwa mgumu sana lakini nawashukuru sana wachezaji wangu wamepambana hadi mwisho kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu,"