KenGold yaipeleka Simba Ruvuma

Muktasari:
- Sababu za timu hiyo kusaka makazi mapya, ni kutokana na Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambao kikosi hicho hutumia kwa mechi zake za nyumbani kutumika pia Juni 18, kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Yanga.
KENGOLD iliyoshuka mapema hadi Championship kutoka Ligi Kuu Bara iliyoicheza kwa mara ya kwanza msimu huu, imepanga kuipeleka mechi dhidi ya Simba iliyopangwa kupigwa Juni 18 Uwanja wa Majimaji, Songea, mkoani Ruvuma, endapo taratibu za ukaguzi uwanjani hapo zitakamilika mapema.
Sababu za timu hiyo kusaka makazi mapya, ni kutokana na Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambao kikosi hicho hutumia kwa mechi zake za nyumbani kutumika pia Juni 18, kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa KenGold, Joseph Mkoko alisema kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala la uwanja wa mechi na Simba, japo taratibu bado zinaendelea na zitakapokamilika watatoa taarifa ya sehemu watakapocheza siku hiyo.
“Kwa sasa tunaendelea na maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Pamba Jiji tutakayocheza Mei 13, kisha baada ya hapo tutakuwa na wigo mpana wa kuzungumzia uwanja tutakaotumia dhidi ya Simba, kwa sasa tuvute subra na mambo yatakapokamilika tutaweka wazi,” alisema Mkoko.
Wakati Mkoko akizungumzia hayo, taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata ni viongozi wa timu hiyo wanafanya juhudi ili kutumia uwanja huo, ambao kwa sasa unatumiwa na Songea United ya Ruvuma inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu.
Kwa upande wa Kocha wa KenGold, Omary Kapilima alisema licha ya timu hiyo kushuka daraja ila wanachokifanya kwa sasa ni kucheza kwa heshima, ingawa anatambua kasi yao ya mwanzo na ya sasa siyo sawa kutokana na wachezaji kupoteza morali.
Kikosi hicho kinaburuza mkiani na pointi zake 16, baada ya kushinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 17 kati ya 27 iliyocheza na imesaliwa na mechi tatu za kufungia msimu kabla ya kuanza maisha mapya Ligi ya Championshilp ambao walibeba ubingwa msimu uliopita na kupanda Ligi Kuu sambamba na Pamba Jiji iliyorejea katika ligi hiyo baada ya msoto wa miaka 23 tangu iliposhuka 2001.