Salah kuongoza Mafarao Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Misri ni alama ya mafanikio ya soka la Afrika. Walikuwa taifa la kwanza Afrika kucheza Kombe la Dunia mwaka 1934, wamebeba Kombe la Mataifa Afrika mara saba, wametoa magwiji wengi wa mchezo huo na sasa wanarudi tena katika michuano hiyo mikubwa zaidi wakiongozwa na mmoja wa mastaa wakubwa zaidi duniani, Mohamed Salah.
CAIRO, MISRI: KUNA mataifa ambayo hushiriki Kombe la Dunia kwa ajili ya kuongeza uzoefu lakini pia kuna mataifa yanayoingia katika mashindano yakiwa na historia nzito mabegani mwao. Misri ni moja ya mataifa hayo.
Ukisikia wanaitwa Mafarao ujue sio kwa bahati mbaya. Ni jina linalobeba historia ya utawala, mafanikio na heshima kubwa ndani ya soka la Afrika. Kwa zaidi ya miaka 100, taifa hilo limeendelea kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya Afrika.
Misri ni alama ya mafanikio ya soka la Afrika. Walikuwa taifa la kwanza Afrika kucheza Kombe la Dunia mwaka 1934, wamebeba Kombe la Mataifa Afrika mara saba, wametoa magwiji wengi wa mchezo huo na sasa wanarudi tena katika michuano hiyo mikubwa zaidi wakiongozwa na mmoja wa mastaa wakubwa zaidi duniani, Mohamed Salah.
WALIANZA MAPEMA AFRIKA
Wakati mataifa mengi ya Afrika yalikuwa bado hayajaanzisha timu za taifa, Misri tayari walikuwa wanacheza mashindano ya kimataifa. Timu yao ya taifa iliundwa rasmi mwaka 1920 kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ambayo ilifanyika Ubelgiji.
Hii ndiyo sababu Misri inatajwa kama taifa kongwe zaidi la soka Afrika. Walikuwa waanzilishi wa kuonesha kuwa Waafrika wanaweza kushindana na mataifa ya Ulaya katika mchezo huo.
Miaka 14 baadaye wakaandika historia kubwa zaidi kwa kuwa taifa la kwanza Afrika kufuzu Kombe la Dunia mwaka 1934 nchini Italia.
Katika kipindi hicho, mataifa mengi ya Afrika hayakuwa hata na ligi imara za ndani.
Katika michuano hiyo, mshambuliaji Abdulrahman Fawzi aliweka historia kwa kuwa Mwafrika wa kwanza kufunga mabao katika Kombe la Dunia baada ya kufunga mara mbili dhidi ya Hungary. Hadi leo, rekodi hiyo inabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya soka la Afrika.
UBABE HAUJAWAHI KUVUNJWA
Hakuna taifa lililowahi kutawala AFCON kama Misri. Mataji yao saba yanaifanya nchi hiyo kuwa timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Walitwaa mataji hayo 1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010. Lakini mafanikio yao makubwa zaidi yalikuja waliposhinda mataji matatu mfululizo kati ya 2006 hadi 2010.
Katika kipindi hicho, Misri ilikuwa timu iliyokamilika kila eneo. Walikuwa na safu bora ya ulinzi, viungo wenye ubunifu mkubwa pamoja na washambuliaji waliokuwa na uwezo wa kuamua mechi muda wowote.
Majina kama Mohamed Aboutrika, Ahmed Hassan, Wael Gomaa na Essam El Hadary yaliifanya Misri kuwa tishio kubwa kwa kila timu Afrika.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba walifanya hivyo bila kuwa na idadi kubwa ya mastaa waliocheza Ulaya. Nguvu yao kubwa ilitokana na mshikamano wa timu na ubora wa ligi yao ya ndani.
BABA LAO SHEHATA
Hakuna simulizi ya mafanikio ya Misri inayoweza kuandikwa bila kumtaja Hassan Shehata. Kocha huyo ndiye aliyebadili kabisa historia ya taifa hilo katika miaka ya 2000. Aliijenga Misri yenye nidhamu, moyo wa kupambana na uwezo mkubwa wa kushambulia.
Katika mikono yake, Misri ilicheza soka lililowafanya Waafrika wengi kuamini kuwa wanaweza kushindana hata na mataifa makubwa duniani.
Wakati huo, Misri iliwahi kupanda hadi nafasi ya tisa katika viwango vya FIFA mwaka 2010, ikiwa ndiyo nafasi ya juu kabisa kuwahi kufikiwa na taifa hilo.
MFALME SALAH
Leo hii dunia ikiisikia Misri, jina la kwanza linalotajwa ni Mohamed Salah. Nyota huyo sio tu nahodha wa taifa hilo, bali ni moja ya sura kubwa zaidi za soka la Afrika duniani.
Umaarufu wake akiwa Ulaya umeifanya Misri kuwa taifa lenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka.
Salah tayari amefunga mabao 67 akiwa na timu ya taifa na bado mabao mawili tu kuifikia rekodi ya kocha wake wa sasa Hossam Hassan mwenye mabao 69.
Kilichomfanya Salah kuwa muhimu zaidi ni uwezo wake wa kubeba matumaini ya taifa zima. Wakati Misri ilipofuzu Kombe la Dunia 2018, karibu nchi nzima ilisimama nyuma yake.
Hata sasa kuelekea 2026, macho yote yatakuwa kwake.
HOSSAM, GWIJI SASA KOCHA
Kitu kinachowapa Wamisri matumaini zaidi ni uwepo wa Hossam Hassan kwenye benchi lao la ufundi.
Huyu ni mtu aliyewahi kuibeba Misri kwa miaka zaidi ya 20 akiwa mchezaji. Ana mechi 176 za kimataifa na ndiye mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo.
Anafahamu vizuri presha ya mashindano makubwa, anajua maana ya kuvaa jezi ya taifa hilo na anajua nini mashabiki wanahitaji kuona kutoka kwa timu yao.
Wengi wanaamini kuwa anaweza kuirejesha Misri kwenye ubora wa zamani.
KIKOSI CHAO
Mbali na Salah, Misri ya sasa ina wachezaji wengi wanaocheza kwenye ligi kubwa duniani.
Yupo Omar Marmoush ambaye kasi yake imekuwa tishio kubwa kwa mabeki wengi Ulaya akiwa na Manchester City. Yupo Mostafa Mohamed mwenye nguvu kubwa eneo la ushambuliaji pamoja na Trézéguet ambaye uzoefu wake bado ni muhimu ndani ya kikosi.
Katikati ya uwanja, kina Emam Ashour na Hamdy Fathy wamekuwa injini ya timu hiyo kutokana na uwezo wao wa kukaba na kuanzisha mashambulizi.
Safu ya ulinzi nayo imekuwa imara kutokana na uwepo wa Mohamed Abdelmonem huku langoni wakimtegemea sana Mohamed El Shenawy.
WALIVYOFUZU KOMBE LA DUNIA
Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026, Misri ilionyesha ubora mkubwa.
Walicheza mechi 10 bila kupoteza hata mmoja, wakishinda nane na kutoka sare mbili. Wamefunga mabao 20 huku wakiruhusu mabao mawili pekee.
Rekodi hiyo inaonesha wazi kuwa timu hiyo imeimarika zaidi kiulinzi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Misri ilimaliza kinara wa kundi A katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia ikiwa na pointi 26.
KUNDI GUMU, LAKINI
Kombe la Dunia 2026 litakuwa na ushindani mkubwa zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya timu. Misri imepangwa kundi moja (G) na Ubelgiji, Iran pamoja na New Zealand.
Ubelgiji ndiyo wanaopewa nafasi kubwa zaidi kutokana na uzoefu wao Ulaya, lakini Misri wanaamini wanaweza kupambana nao.
Dhidi ya Iran, mchezo huo tayari umeanza kutajwa kama moja ya mechi zitakazovuta hisia za wengi kutokana na ukubwa wa mataifa hayo mawili katika ukanda wa Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.
New Zealand kwa upande mwingine wanaonekana kuwa timu ambayo Misri wanapaswa kushinda kama wanataka kufuzu hatua inayofuata.
NINI WANAKITAFUTA 2026?
Kwa miaka mingi, mafanikio makubwa ya Misri yamekuwa Afrika. Lakini sasa wanataka kufanya kitu kikubwa duniani.
Katika historia yao yote ya Kombe la Dunia, hawajawahi kuvuka hatua ya awali kwa mfumo wa sasa wa mashindano. Hiyo ndiyo ndoto yao kubwa kwa sasa.
Mashabiki wa taifa hilo wanaamini kizazi hiki kinaweza kufanya jambo maalum kutokana na uzoefu wa wachezaji wao wengi wanaocheza Ulaya.
Pia wanaamini huu unaweza kuwa mwisho wa safari ya Kombe la Dunia kwa Salah, hivyo kila mchezaji ndani ya kikosi anataka kuhakikisha wanaandika historia mpya.