Tumuunge mkono Kocha Mkwasa
Muktasari:
- Ni mwendelezo wa mwitikio chanya ambao Watanzania tumeanza kuwa nao juu ya soka la vijana ambalo limekuwa chachu ya kuzalisha wachezaji bora.
Kocha Boniface Mkwasa ameonekana amefungua kituo cha soka kwa vijana wadogo.
Ni mwendelezo wa mwitikio chanya ambao Watanzania tumeanza kuwa nao juu ya soka la vijana ambalo limekuwa chachu ya kuzalisha wachezaji bora.
Inapotokea mtu kama Mkwasa anafungua kituo cha soka ambacho kinawaandaa wachezaji wa siku za usoni, basi tunapaswa kumuunga mkono.
Kuna faida mbili ambazo watoto watakaoenda katika kituo hicho kilicho chini ya Mkwasa watazipata na watanufaika nazo kwa muda mrefu.
Faida ya kwanza ni kupata maandalizi bora zaidi ya kimbinu na kiufundi pia kiakili, ambavyo ni vitu muhimu vinavyohitajika kwa mchezaji wa kisasa anayecheza soka la kulipwa.
Nadhani wengi tunakubaliana Mkwasa ni miongoni mwa makocha bora kuwahi kutokea hapa nchini na ana uzoefu mkubwa wa kufundisha soka katika ngazi ya klabu na timu za taifa za umri tofauti za Tanzania.
Lakini faida ya pili ni watoto kupata hamasa na ushawishi mkubwa wa kucheza soka kutokana mvuto ambao wataupata kwa wasifu wa Mkwasa akiwa mchezaji mkongwe.
Kuwahi kuichezea Taifa Stars na klabu kubwa nchini kama Yanga, kunatosha kuwa ushawishi kwa watoto ambao anawalea kisoka kwenye kituo chake.