Ufundi wa Kepteni Bruno

Muktasari:
- Swali hilo lilikuwa na maana ni wapi kapteni Bruno Fernandes atakwenda kufiti?
MANCHESTER, ENGLAND: WAKATI Ruben Amorim anaingia mlangoni Old Trafford, Novemba mwaka jana na kauntabuku lake la maelezo ya fomesheni ya 3-4-2-1 mkononi, maswali mengi yaliyoibuka ni kutokuwapo kwa majukumu ya Namba 10.
Swali hilo lilikuwa na maana ni wapi kapteni Bruno Fernandes atakwenda kufiti?
Baada ya dakika 68 katika mechi ya kwanza ya Kocha Amorim klabuni Manchester United katika sare ya 1-1 dhidi ya Ipswich Town, majibu yalipatikana.
Fernandes aliondolewa kwenye ile Namba 10 ya safu ya washambuliaji watatu wa mbele na kuja kucheza kwenye kiungo ya kati upande wa kushoto, eneo ambalo kocha Amorim ameamua kumtumia kwenye nafasi hiyo Mreno huyo.

Majaribio mengine ya kucheza nafasi tofauti yalifuata, lakini kwenye mechi 12 kati ya 13 za mwisho kwenye michuano yote, Fernandes amekuwa akitumika kama moyo wa safu ya kiungo ya Man United.
Mechi pekee ambayo alianza mbele ni ile ya ugenini dhidi ya Everton, kisha baadaye Fernandes alishuka chini baada ya Alejandro Garnacho kuingia kuchukua nafasi ya kiungo Casemiro kwenye dakika ya 62. Mabadiliko hayo yaliisaidia Man United kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kupata sare ya 2-2. Sasa katika kuelekea mchezo ujao wa Man United dhidi ya Nottingham Forest, kinachoonekana Fernandes si tu mchezaji aliyekuwa kwenye ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, bali pia ni moja ya wachezaji wanaokupa kila unachokitaka kwenye ligi hiyo.
Msimu wa ovyo wa Man United haushabiani kabisa na kiwango cha Fernandes. Sawa, mwanzoni alianza vibaya baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu tatu kati ya Septemba mwishoni na Boxing Day, lakini kwa sasa staa huyo ni matata kwelikweli ndani ya uwanja. Kwenye ishu ya kutawanya mipira uwanjani, Bruno ni fundi wao.

Kwa msimu huu, amepiga pasi 241 kwenye boksi la wapinzani, anashika namba moja kwenye ligi. Amepiga pasi za kupenyeza 21, anashika namba moja kwa ligi. Pasi sahihi kwenye eneo la wapinzani 469, namba mbili kwenye ligi, ametengeneza nafasi 66, namba mbili kwenye ligi, ameasisti mara tisa, namba mbili kwenye ligi, ametengeneza nafasi 45 zisizohusisha mipira ya adhabu, namba nne kwenye ligi na ametengeneza nafasi kubwa 12, namba tano kwenye ligi. Huo ni ufundi wa kapteni Bruno anapokuwa kwenye nusu ya wapinzani.
Amewapa wachezaji wa timu pinzani presha mara 599 ikiwa ni mara nyingi zaidi kwenye ligi, ambapo kwenye Ligi Kuu England hakuna mchezaji wa safu ya kiungo aliyezidi mara 475 kuwapa presha timu ya upinzani ili kupoka mpira.
Kapteni Bruno pia ni balaa anapokuwa hana mpira na takwimu zake zinabainisha wazi. Amerudisha mpira kwenye umiliki wa timu yake mara 161, akiwa namba tatu kwenye ligi, amewapata presha timu pinzani katikati ya uwanja mara 80, ambayo inamfanya ashike namba tatu kwenye eneo hilo katika ligi.
Bruno anafunga pia na kwa msimu huu ameshafunga mara 16 kwenye michuano yote. Mabao yake matatu kati ya manane aliyofunga kwenye Ligi Kuu England amefanya hivyo kwenye mechi nne zilizopita na yote amefunga nje ya boksi.
Friikiki matata kabisa dhidi ya Everton na Arsenal na kisha bao la shuti la mbali dhidi ya Leicester City.
Kwa msimu huu, amefunga mabao matano nje ya boksi, kwenye ligi anashika namba moja, amepiga mashuti 75, anashika namba tatu
kwenye ligi na amehusika kwenye mabao 17, namba tatu kwenye ligi.

Majukumu mapya
Bruno amekuwa mtamu zaidi kwenye kiungo ya kati tofauti na mwanzoni alipokuwa sehemu ya washambuliaji watatu. Na hakika, Bruno analifanyia kazi vyema kabisa eneo lake jipya la majukumu yake ya kazi. Amekuwa akifanya vizuri sana kwenye kiungo ya kati, awe amepangwa na Casemiro au Manuel Ugarte. Eneo hilo analocheza Bruno kwa sasa, amekuwa akitawala mchezo, akipiga pasi za kupenyeza nyingi kuliko mchezaji yeyote kwenye klabu hiyo.
Kwenye ishu ya kutengeneza nafasi za kufunga, Fernandes anakuwa mchezaji namba sita kwenye Ligi Kuu England kwa kuwa mzalishaji mahiri wa jambo hilo katika kipindi cha miaka 22 iliyopita. Ana wastani wa kutengeneza nafasi 2.84 kwa dakika 90, akizidiwa na mafundi wenzake wote ambao ni Kevin De Bruyne mwenye wastani wa 3.59, Mesut Ozil 3.29, David Silva 2.98, Ryan Giggs 2.90 na Cesc Fabregas 2.89.
Fernandes amecheza mechi 187 tangu alipojiunga na Man United na ndani ya muda huo, amefunga mabao 62 na asisti 50. Kwa rekodi za kuanzia Januari 2020 tangu alipotua Man United, kapteni Bruno anazidiwa na wachezaji wawili tu katika ishu ya kuhusika kwenye mabao mengi kwenye ligi, kwa maana ya kufunga na kuasisti.

Fernandes amehusika kwenye mabao 112, akifunga 62 na asisti 50, wakati wachezaji wanaomzidi ni Mohamed Salah, aliyehusika kwenye mabao 177 (amefunga 116, asisti 61) na Son Heung-min aliyehusika kwenye mabao 124, akiwa amefunga 79 na asisti 45. Kwa rekodi za miaka mitano iliyopita ni Salah na De Bruyne pekee ndiyo wanaomzidi Fernandes kwa asisti. Lakini, kwa upande wa ubunifu ndani ya uwanja, Fernandes amewapiku wote. Na kwa hesabu za kutengeneza nafasi nyingi za mashambulizi, Bruno ni namba moja kwa kuanzia Januari 2020, nafasi 513.