Prime
Yanga, Azam vita yenu ndo heshima Bara
MECHI za kufungia hatua ya makundi kwa michuano ya CAF kwa msimu wa 2025-2026 zinapigwa wikiendi hii, huku macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa kwa Yanga na Azam FC.
Wawakilishi hao wawili ndio waliobeba matumaini ya Tanzania kuingiza angalau timu moja katika robo fainali baada ya Simba na Singida Black Stars kuchemka mapema katika mechi zao za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Tanzania ilibahatika kuingia katika vitabu vya historia vya soka la Afrika kwa kuingiza klabu nne kwa mpigo, zikiwa Simba na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC na Singida BS zikishiriki kwa mara ya kwanza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, kuna dalili huenda timu hizo nne zikaaga michuano hiyo na kushindwa kwenda robo fainali, iwapo Yanga iliyopo Kundi B itashindwa kufanya maajabu mbele ya As FAR Rabat ya Morocco inayochuana nao kuwania tiketi moja ya robo fainali ikiungana na Al Ahly ya Misri.
Azam, iliyopo Kundi B la Kombe la Shirikisho nayo ina mtihani mbele ya AS Maniema ya DR Congo ili kuandika rekodi nyingine ya kucheza makundi mara ya kwanza na kuvuka hadi robo fainali.
Katika kundi ililopo, Azam imefungana pointi na Maniema kila moja ikiwa na tisa baada ya mechi tano, nyuma ya Wydad AC ya Morocco iliyofuzu kwenda robo na kuziachia msala timu hizo, huku Nairobi United ya Kenya ikiwa kama wasindikizaji tu kwani haijapata pointi yoyote hadi sasa.
Yanga ipo nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kucheza na JS Kabylie ya Algeria, huku ikisikilizia pambano la Al Ahly ya Misri na As FAR Rabat zitakazokuwa uwanjani Cairo.
Yanga ina pointi tano na inahitaji ushindi ili kufikisha pointi nane kama ilizonazo AS FAR ambayo sare ya aina yoyote inawapeleka robo kwani tayari ina pointi nane mkononi kwa sasa.
Azam yenyewe ipo ugenini kuvaana na Wydad iliyofuzu, lakini ambayo haijapoteza mechi yoyote ya nyumbani, ila Wanalambalamba wakisikilizian matokeo ya Maniema na Nairobi United, kwani ushindi wowote utawahakikishia Wakongomani kuungana na vinara wa Kundi B.
Simba yenyewe itakuwa uwanjani kesho kukamilisha ratiba dhidi ya Stade Malien ya Mali, ikisaka ushindi wa kwanza nyumbani katika michuano ya CAF msimu huu, lakini ikiweza kuchupa kutoka mkiani mwa kundi hadi nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi tano hata kama haivuki kwenda robo.
Singida BS yenyewe ipo ugenini ikiifuata Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa mechi ya kukamilisha ratiba kwani imeshajiengua katika mbio za kusaka tiketi ya robo fainali katika Kundi C kwa pointi ilizonazo hadi sasa kwani inazo nne na ikishinda itafikisha saba zilizopitwa na CR Belouizdad ya Algeria na Otoho d’Oyo ya Congo Brazzaville zilizopenya mapema robo fainali kwa pointi ilizonazo.
Kifupi ni kwamba Tanzania ilikuwa na msimu bora zaidi wa Ligi Kuu Bara kwa Afrika kwa kuingiza timu nne hatua ya makundi kwani, haya ni mafanikio tuliyozoea kwa miaka mingi kwa Ligi za nchi kama ya Misri, Morocco na hata Tunisia na Algeria kama sio Afrika Kusini ambazo zimekuwa zikiingiza timu nne hatua ya makundi.
Kwa kuangalia kwa namna tumezoea kutazama vitu ki-kawaida kana kwamba hakuna lolote ni bahati tu tunaweza kulidogosha jambo hili ila sio jambo dogo ni mafanikio, kwani DR Congo mbali na kuwa na TP Mazembe iliyokuwa ikitikisa Afrika walihangaika kupeleka timu nne makundi.
Hivyo hatua tuliyofikia msimu huu, kwetu ni jambo chanya kwa ligi kupata mafanikio yanayofaa kujengewa misingi imara na yawe na muendelezo ili kuyageuza kuwa daraja la ligi yetu kwa misimu ijayo. Lakini ni muhimu wawakilishi wa Tanzania wakomae angalau kupata timu moja hatua ya robo.
Hadithi tamu ya mafanikio tunayoendelea kufurahia ni kuombea tukimaliza mechi za makundi kuvusha angalau timu moja. Itakuwa aibu kama timu zote zitatoka na kushindwa kwenda robo fainali wikiendi hii.
Yanga na Azam zinapaswa kufanya kitu wikiendi hii kuhakikisha zote au moja inaenda robo fainali kulinda heshima ya Tanzania ili kuondoka dhana kwamba kufuzu na kuingiza timu nne ilikuwa ni kubahatisha na sio ubora wa Ligi Kuu Bara iliyo katika nafasi ya sita kwa sasa Afrika.
Ni kweli kufuzu kwa timu hizo kunategemea zaidi vikokotoo vya mechi zao binafsi za zile za wapinzani waliopo katika makundi yao, lakini ni afadhali kuliko kuanguka kwa Simba na Singida BS mapema ambao zinaenda kukamilisha ratiba tu kwa msimu huu wa 2025-2026.
Vinginevyo tutarudi katika hali ya majonzi kwa kubaki watazamaji wa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu Afrika.
Sitaki kuamini kuporomoka kwa wawakilishi wetu Afrika kunatokana na kushuka kwa ubora wa Ligi Kuu Bara iliyoporomoka kutoka nafasi ya nne iliyokuwa inashikilia kwa miaka miwili iliyopita hadi kuwa ya sita kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu na Historia ya Soka (IFFHS).
Hapa kuna somo tunalipata tukijaaliwa afya wakati mwingine tutaliangalia hili. Kwa leo tuendelee kuziombea dua zile timu ambazo bado calculator inawaka na kuzimika. Usimkatie tamaa mwanadamu. ungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Yanga na Azam.