Yanga ilivyotumia miaka mitatu kuifunga Simba

Muktasari:
- Lakini ilikuwa majonzi kwa mashabiki wa mnyama ambao waliamini ushindi kwenye mchezo ule ungerahisisha mbio zao za kutetea ubingwa wa ligi.
JUZI Machi 19 ilikuwa furaha kwa mashabiki wa Yanga Princess baada ya kumfunga mtani wao, Simba Queens bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Lakini ilikuwa majonzi kwa mashabiki wa mnyama ambao waliamini ushindi kwenye mchezo ule ungerahisisha mbio zao za kutetea ubingwa wa ligi.
Mchezo huo wa dabi ya wanawake ulipigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam na bao hilo pekee lilifungwa na Jeaninne Mukandasyenga dakika ya 48 aliyepokea pasi kutoka kwa Adebis Ameerat.
Mzunguko wa kwanza zilipokutana, Yanga ikiwa mwenyeji ilipoteza kwa bao 1-0 baada ya beki wa timu hiyo kujifunga kutokana na presha kutoka kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Vivian Corazone katika lango la wananchi.
Mchezo ulikuwa ni wa 13 kukutana tangu mwaka 2019, Yanga ikishinda mara mbili, sare mbili na kupoteza tisa huku Simba ikishinda tisa, kupoteza miwili na sare mbili, huku yakifungwa mabao 44,Simba ikifunga 35 na Yanga tisa.

Kwenye mabao hayo 35 ya Simba, 10 yamefungwa na mshambuliaji mkongwe Mwanahamis Omary 'Gaucho' akiweka rekodi ya kuwa mwanadada wa kwanza kufunga hat-trick kwenye dabi.
MIAKA MITATU
Yanga Princess hadi juzi imetumia miaka mitatu kuifunga Simba ambayo imekuwa ikitoa vichapo kila wanapokutana kwenye ligi na mashindano mengine kama Ngao ya Jamii.
Mara ya mwisho Yanga kuifunga Simba ilikuwa Aprili 24 mwaka 2022 mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0 la Clara Luvanga aliyetimkia Al Nassr ya Saudia.
Kumbukumbu mbaya kwenye mchezo ule Simba ilipata kadi nyekundu ya mapema dakika ya nne baada ya beki Julietha Singano kumchezea faulo Luvanga na kucheza wakiwa pungufu.
Baadae dakika ya 44 Luvanga alipiga shuti kali ambalo lilionekana halina madhara kwa kipa Gelwa Yona mpira ambao ulimponyoka na kuingia moja kwa moja kambani, bao lililodumu kwa dakika zote 90.

Msimu uliofuata zilipokutana tena zilitoshana nguvu kwa sare ya 1-1, huku msimu uliopita Yanga ikapoteza tena nyumbani na ugenini kwa jumla ya mabao 6-2, ikifungwa 3-1 kila mzunguko.
Tangu hapo Yanga iliendelea kupokea vichapo kutoka kwa Simba ikiwavuruga mabosi wa wananchi hao kuendelea kuwa 'wateja' kwa watani zao.
EDNA LEMA TENA
Kama kuna usajili bora wa benchi la ufundi walilofanya Yanga msimu huu ni kumrejesha Kocha Edna Lema 'Mourinho' anayelifahamu vyema soka la wanawake na timu hiyo kwani alifundisha kwa vipindi tofauti.
Kocha huyo alirejeshwa kikosini msimu huu akitokea Biashara United inayoshiriki Championship akihudumu kama kocha msaidizi.
Mourinho ameendelea kuweka rekodi ya kuifunga Simba mara mbili baada ya msimu 2022/23 na juzi akisimama kama kocha mkuu.
Kikosini hapo wamepita baadhi ya makocha Sebastian Nkoma, Mzambia Charles Haalubono ambao hawakuwahi kuifunga timu hiyo iliyobeba ubingwa wa ligi mara nne.
Hiyo ni dabi ya 10 kwa kocha huyo wa zamani wa Twiga Stars akipata ushindi mara mbili, sare mbili na kupoteza mechi sita.

Hii inakuwa mara ya pili kwa Mourinho kuifunga Simba na hadi sasa timu hiyo haina nafasi ya kuchukua ubingwa lakini kama itashinda mechi tano zilizosalia inayo nafasi ya kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi msimu huu na huenda Edna akarudia msimu 2021 alipomaliza namba mbili.
ZILIPOKUTANA
13/01/2029 Yanga 0-7 Simba
22/04/2019 Simba 5-1 Yanga
12/12/2019 Simba 3-1 Yanga
10/07/2020 Yanga 1-5 Simba

12/12/2020 Simba 0-0 Yanga
05/03/2021 Yanga 0-3 Simba
08/01/2022 Yanga 1-4 Simba
24/04/2022 Simba 0-1 Yanga
22/03/2023 Yanga 1-1 Simba
03/01/2024 Simba 3-1 Yanga
25/04/2024 Yanga 1-3 Simba
13/11/2025 Yanga 0-1 Simba
18/03/2025 Simba 0-1 Yanga

MSIKIE MOURINHO
Akizungumza baada ya ushindi Mourinho alisema "Nilikuwa na deni kubwa kwa mashabiki, wanaamini mimi ni mtu pekee ninayeweza kuifunga Simba, hatukuwa vizuri kipindi cha kwanza lakini nilifanya mabadiliko ya kumtoa nahodha na kumuingiza Adebisi kile nilichomwelekeza amefanya tukapata bao."
Msimamo Ligi Kuu Wanawake (WPL)
P W D L F A PTS
1.JKT Queens 13 11 2 0 51 3 35
2.Simba Queens 13 11 1 1 43 8 34
3.Yanga Princess 13 8 3 2 27 9 27
4.Mashujaa Queens 13 5 3 5 21 16 18
5.Ceasiaa Queens 11 4 1 6 15 24 13
6.Alliance Girls 12 3 3 6 16 23 12
7.Fountain Gate Prince 11 3 2 6 18 18 11
8.Bunda Queens 11 2 3 6 11 20 9
9.Get Program 11 2 3 6 9 30 9
10.Mlandizi Queens 12 0 1 11 5 64 1
4- Idadi ya mataji ya Ligi Kuu iliyobeba Simba huku Yanga ikiwa haijabeba hata moja
10 - Idadi ya mabao aliyofunga Mwanahamis Omary 'Gaucho' katika dabi
1 - Hat trick pekee iliyofungwa kwenye dabi na Mwanahamis Omary 'Gaucho' wa Simba
13 - Idadi ya dabi zilizokutana Simba Queens na Yanga Princes tangu mara ya kwanza msimu wa 2019/20
44- Idadi ya mabao yaliyofungwa kwenye dabi, huku Simba ikifunga 35 na Yanga tisa