Ihefu yazivizia Yanga, Azam

KOCHA wa Ihefu, Zubery Katwila amesema ana nafasi tano za kuongeza wachezaji wapya kupitia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa jana na tayari kuna vifaa viwili kutoka Azam FC vinatarajiwa kutua kwa wageni hao wa Ligi Kuu Bara, huku pia wakivizia wachezaji wenginge kutoka Yanga akiwamo kiungo Juma Mahadhi.

Katwila alisema watakuwepo baadhi ya wachezaji ambao watawachukua kwa mkopo kutoka katika timu kadhaa nchini ikiwemo Yanga na Azam kutokana na uzoefu wao ili kukiongezea makali kikosi chao kwa duru la pili la ligi hiyo waliyoianza na mguu mbaya tangu mechi yao ya kwanza.

Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa kwenye mipango ya timu hiyo kutoka Azam ni beki Oscar Masai na mshambuliaji, Andrew Simchimba, huku ikielezwa hata beki kisiki David Mwantika anaweza kuibukia huko, ingawa bado dili halijakamilika.
“Kuhusu Juma Mahadhi kutoka Yanga siwezi kueleza lolote mpaka hapo nitakapokuwa naye katika timu kwani naweza kumzungumzia wakati huu kumbe akabadilisha uamuzi juu kwa juu na akaenda kucheza timu nyingine,” alisema Katwila.
Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria alisema ni kweli mamepokea maombi ya timu nyingi kutoka kwenye ligi zikiwahitaji wachezaji wao kwa mkopo na Ihefu ikiwa ni moja wapo lakini bado hawajafanya uamuzi kwa vile kocha wao, George Lwandamina ametaka kuwaona wachezaji zaidi ili aamue nani atoke na yupi abaki kikosini.
“Tumeyaona maombi ya Ihefu na kuna baadhi ya wachezaji wanawataka kutokea kwetu lakini si wao tu bali kuna Biashara United, Mwadui na nyinginezo wametuma maombi ya kutaka wachezaji wetu lakini Lwandamina ndio mwenye kauli ya mwisho,” alisema Zakaria na kuongeza;

“Lwandamina ameomba tumpatia muda kidogo na kabla ya dirisha kufungwa ndio atoe tathmini yake wachezaji wa kubaki nao na atakaokubali kuwaachia kwa mkopo.”