Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkwabi, Rage wafunguka Simba SC

Dar es Salaam. Vigogo wa zamani wa klabu ya Simba, Swedi Mkwabi na Ismail Aden Rage wamefunguka kuhusishwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa klabu hiyo kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Februari 7, mwakani.

Rage na Mkwabi waliowahi kuwa wenyeviti wa klabu ya Simba kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili jana kwamba licha ya baadhi ya wanachama kuwaomba wafanye hivyo, lakini hawana mpango huo.

Mkwabi ambaye alijiuzulu nafasi yake alisema,kurudi kugombea uongozi wa Simba ni mpaka mfumo wa klabu utakapobadilika.

“Ni kweli wanachama baadhi walinifuata kuomba nirudi, nikawaambia wangetaka nirudi wangehoji kwenye mkutano mkuu kwanini niliondoka na sio sasa, siwezi kurudi tena kwa kuwa sikujiuzulu kwa bahati mbaya.

“Hata mwenyekiti ajaye naamini atakuwa na kazi ngumu kama mfumo wa klabu hautabadilika, kwani kuongoza Simba tangu nimeingia mfumo haukuwa rafiki, unakuwa mwenyekiti usiye na nguvu, ni kama kuwa rais halafu hauna nguvu kwenye baraza la mawaziri,” alisema Mkwabi.

“Sijapaga kabisa kurudi kugombea tena uenyekiti wa klabu ya Simba na ninaamini mwenyekiti ajaye atakutana na changamoto ambazo zilisababisha nijiuzulu, bado vitu vingi haviko sawa.

“Katiba ya Simba haimpi nguvu mwenyekiti ndiyo sababu nikatolea mfano, ni kama kuwa rais halafu huna nguvu kwenye baraza la mawaziri, ni ngumu, mwenyekiti ajaye ajiandae kukutana na hilo na kukabiliana nalo.”

Simba itafanya uchaguzi mdogo kuziba nafasi ya Mkwabi Februari 7 na tayari fomu za kugombea nafasi hiyo zimeanza kutolewa makao makuu ya klabu jijini Dar es Salaam hadi Desemba 24, ingawa mpaka jana saa 5:30 asubuhi hakuna mwanachana aliyekuwa amejitokeza kuchukua fomu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Boniface Lihamwike alisema bado mwitikio wa kuchukua fomu ni mdogo ingawa alisisitiza kuwa wengi wa wagombea huwa na utamaduni wa kusubiri siku ya mwisho, hivyo bado wana muda.

Wakati wanachama wakitegeana kuchukua fomu za kugombea, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ambaye tangu mchakato wa uchaguzi mdogo ulipotangazwa amekuwa akihusishwa kutaka kumrithi Mkwabi alisema hana mpango wa kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, Rage alisema hawazii wala hana nia ya kujitosa kugombea uenyekiti wa klabu hiyo kwani hataki kuingia kwenye kile alichodai kuwa ni matatizo.

“Watu wana matatizo yao halafu na mimi niingie kwenye matatizo, siwezi na isitoshe sijawahi kuwaza kugombea, na hata kama ningetaka kugombea ningetangaza mwenyewe bila woga kwa kuwa najiamini,” alisema Rage.

Alisema ambacho anaweza kukifanya kwa sasa ni kuwa mshauri pekee, lakini sio kujitosa kuongoza klabu hiyo ambayo iko kwenye mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji kutoka kwa wanachama kuwa kampuni.

Ingawa mchakato huo umeibua sintofahamu baada ya Simba kueleza unacheleweshwa na Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC), Simba nayo ilijibu haijakamilisha taratibu zilizotakiwa kufanyika.