Simba yatuma jeshi Harare

SIMBA haipoi haiboi. Katika kuthibitisha azma yao ya kufanya makubwa kwenye ligi ya ndani na kimataifa, Wekundu wa Msimbazi, wametuma jeshi jijini Harare, Zimbabwe kwa ajili kuandaa mipango ya kuwamaliza FC Platinum katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jeshi la Simba likiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez limeelekea nchini Zimbabwe kwa ajili ya kuweka mambo sawa kwa ajili ya mechi yao ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum itakayochezwa Desemba 23, 2020.
Mbali na Barbara kuondoka jana Jumanne mchana, Mwanaspoti inajua kwamba wengine akiwemo Mratibu wao, Abbas Selemani pamoja na mpishi Samuel Cyprian watafuata kabla ya timu kuondoka.
Jeshi lililotangulizwa ni kwa kazi maalum ya kuandaa mazingira ambayo yataifaa timu kufikia ikiwamo hoteli, uwanja wa mazoezi, usafiri na mambo mengineyo ya msingi.
Simba walitunga hatua ya pili ya mtoano ya michuano hiyo baada ya kuwatoa Plateau United ya Nigeria, ilishinda mechi ya ugenini bao 1-0 kabla ya kutoka sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.