Penalti ya utata yaibeba Simba kwa KMC

MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na KMC umemalizika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilionekana kuwa ngumu kwa timu zote mbili kwani zilimalizika pasi kuwa na bao lolote lililofungwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kocha wa Simba Sven Vandenbroeck kuwatoa golikipa Aishi Manula na mshambuliaji John Bocco na nafasi zao kuchukuliwa na Beno Kakolanya na Meddie Kagere.

Kwa muda wa dakika nne baada ya kuanza kwa kipindi cha pili lango la KMC lilikua hatarini kwani idadi kubwa ya namba ya wachezaji wa Simba walikua eno hilo wakisaka bao licha ya kuambulia patupu.
Dakika ya 62 makocha wote wawili walifanya mabadiliko KMC Alitoka Mohamed Samata na nafasi yake kuchukuliwa na Kelvin Akijiri wakati kwa Simba alitoka Mzamiru Yassin na nafasi yake kuchukuliwa na Chriss Mugalu.
Pia dakika ya 70 KMC walifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Reliant Lusajo na nafasi yake kuchukuliwa na Paul Peter.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwanufaisha Simba zaidi kwani kwa kiasi kikubwa walikuwa wakionekana kulishambulia lango la KMC.
Dakika ya 73 mwamuzi Elly Sasii aliwapatia Simba mkwaju wa penalti baada ya beki wa KMC kushika mpira kwenye eneo la hatari mkwaju uliopigwa na Meddie Kagere na kuzama nyavuni na kuwapatia Simba bao la kuongoza.
Penalti hiyo imezua mijadala mitandaoni kwa video za marejeo huku watu wakivutana uhalali wa penalti hiyo.
Wakati huo huo kocha mkuu wa KMC alimtoa Hassan Kabunda na nafasi yake kuchukuliwa na Massoud Abdallah.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Simba 1-0 KMC.