Makame hahofii kusugua benchi Yanga

Muktasari:
- Abdulaziz Makame anaamini katika kujituma ndiko kunamfanya mchezaji benchi kwake liwe ndoto hivyo anaamini juhudi zake ndizo zitamfanya apangwe kikosi cha kwanza Yanga.
KIUNGO wa Yanga, Abdulaziz Makame amesema hana hofu ya kukosa namba ndani ya kikosi cha kwanza cha kocha Boniface Mkwasa na kwamba anampa nafasi kila mtu kuonyesha uwezo wake.
Makame amesema hajaona wa kumkalisha benchi ila anachokiamini ni kujituma kwa bidii ili uwezo wake uwe na faida kwenye timu.
"Sijaona ushindani wa aina yoyote ndani ya kikosi cha Yanga kikubwa ni mimi mwenyewe kuongeza bidii ya mazoezi, ninachokiamini hakuna kocha ambaye anaweza kumuweka benchi mchezaji anayeweza kusaidia timu,"
"Nipo Yanga kwa ajili ya kucheza hivyo siwezi kuilaza akili yangu kwamba mimi nitakuwa nakaa benchi, isitoshe umri wangu ni mdogo hivyo nina nafasi ya kufanya makubwa zaidi," amesema.
Nje na kikosi cha Yanga, amesema anatamani awe na namba ya kudumu ndani ya kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' akiamini kwa mchezaji aliye na ndoto za kufika mbali lazima asaidie taifa lake.
"Msimu huu lazima nitafanya mambo makubwa, nimejipanga uwezo utaongea zaidi uwanjani,"amesema.