Simba, KMC ngoma ngumu

Dar es Salaam. Baada ya moto wao kushindwa kudhibitiwa katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu, John Bocco na Clatous Chama leo wana fursa nyingine ya kuthibitisha ubora wao wakati Simba itakapoivaa KMC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1.00 usiku.
Wawili hao katika michezo mitatu iliyopita ya Simba dhidi ya Coastal Union, Polisi Tanzania na Mbeya City, wamehusika katika mabao nane kati ya 10 ambayo Simba imefunga.

Bocco, ambaye anaongoza katika ufungaji akiwa na mabao nane, amefunga mabao manne katika mechi tatu zilizopita, akipachika matatu dhidi ya Coastal Union na lingine dhidi ya Mbeya City wakati Chama akifunga manne, amefunga mabao mawili katika kila mechi dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union.
KMC haina rekodi nzuri mbele ya Simba, wamepoteza mechi zote nne walizowahi kukutana katika Ligi Kuu, wakifunga mabao mawili, wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara nane.
Timu hizo zinakutana zikiwa katika kiwango na ubora wa hali ya juu, zimekuwa na matokeo ambayo hayapishani sana katika michezo mitano iliyopita.
Wakati Simba ikivuna jumla ya pointi 13 katika mechi tano zilizopita, ikipata ushindi mara nne na kutoka sare moja, ikifunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu, KMC katika mechi tano, imekusanya pointi 10, ikiibuka na ushindi mara tatu, sare moja na kupoteza moja, huku ikipachika mabao sita na kuruhusu mawili.

Kutokana na uwepo wa mchezo wa ugenini wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Platinum utakaochezwa siku saba zijazo nchini Zimbabwe, huenda kukawa na mabadiliko kadhaa katika kikosi cha Simba ili kulinda baadhi ya nyota wasipate majeraha.
Jambo kama hilo ndilo lilifanyika katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, nyota kama Luis Miquissone hakucheza, huku nahodha Bocco akitolewa mapema mwanzoni mwa kipindi cha pili, wakati huo wachezaji wanne wakibakishwa Dar es Salaam, ambao ni Ibrahim Ajibu, Larry Bwalya, Bernard Morrison na Charles Ilanfya.
Ni mechi ambayo kila timu inaitazama kama fursa ya kujiweka mahali pazuri katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa itafanikiwa kuibuka na pointi tatu muhimu kulingana na msimamo wa Ligi ulivyo.
Ushindi utawafanya KMC wanaoshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 21, wasogee hadi nafasi ya nne kwani watawapiku Ruvu Shooting kwa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa wakati kwa Simba, iwapo wataibuka na ushindi, watazidi kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo, kwa sababu watafikisha jumla ya pointi 32 na kuzidi kuiongezea presha Yanga inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37.

Kocha wa KMC, Habib Kondo alisema wanafahamu ugumu ulio mbele yao dhidi ya Simba lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Tunafahamu haitokuwa rahisi kucheza nao kwa sababu Simba ni timu nzuri na ina wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu hivyo tunatakiwa kufanya kazi ya ziada katika mchezo huo.
“Lakini kwa maandalizi tuliyofanya na ikiwa vijana watafanyia kazi vyema kile ambacho wataelekezwa kufanya, naamini tunao uwezo wa kupata matokeo mazuri dhidi yao,” alisema.
Ligi hiyo itaendelea tena Ijumaa ambapo kutakuwa na mechi nne zitakazochezwa katika viwanja tofauti nchini.
Vibonde Mwadui FC watakuwa nyumbani Mwadui Complex kuikaribisha Polisi Tanzania, wakati Biashara United watakuwa kwao, Karume Musoma kuikaribisha Mbeya City.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar wataikaribisha Coastal Union ya Tanga, wakati Azam FC wao watakuwa nyumbani, Azam Complex kuwaalika Ruvu Shooting.