Afcon ilivyommaliza nyota Stars

David Mwantika (kulia) akizungumza na mwamuzi katika moja ya mechi za Afcon 2019 nchini Misri

Muktasari:

  • Kuanzia hapo Mwantika akafutika kwenye ramani ya mpira wa miguu Tanzania hadi sasa. Badala ya kufaidika na Afcon, Mwantika akaponzeka nayo hadi leo. 

MASHINDANO makubwa huwa daraja la kuwavusha wachezaji wengi kutoka timu za kawaida na kwenda timu kubwa endapo watafanya vizuri. Hiki ndicho kilichotokea kwa James Rodriguez, nyota wa Colombia aliyeng’ara katika Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Mabao yake sita yalimfanya kuwa mfungaji bora, huku bao moja dhidi ya Uruguay kwenye 16 bora likichaguliwa kuwa bora la mashindano. Rodriguez akageuka lulu na wababe wa dunia, Real Madrid wakapiga hodi klabuni kwake Monaco na kumchukua kwa hela nyingi.

Au tuachane na Ulaya, tuje Afrika. Blati Toure wa Burkina Faso alikwenda kwenye Afcon 2021 akiwa hana klabu. Lakini moto aliouwasha huko ukamfungulia milango ya riziki na matajiri wa Cairo Misri, Pyramids FC wakamdaka juu juu.

David Mwantika (kulia) akizungumza na mwamuzi katika moja ya mechi za Afcon 2019 nchini Misri

Wakati kwa wachezaji hao mashindano makubwa yalikuwa neema, kwa David Mwantika wa Tanzania hali ilikuwa tofauti. Mwaka 2019 Tanzania ilifuzu kushiriki Afcon kwa mara ya pili ikiwa ni baada ya takribani miaka 40.

Kocha wake, Emannuel Amunike, nyota wa mashindano hayo mwaka 1994 alipofunga mabao mawili kwenye fainali dhidi ya Zambia na kusaidia timu yake kushinda ubingwa, akaita jeshi lake.

Katika safu ya ulinzi alichukua mabeki wanne wa kati Aggrey Morris wa Azam FC, Kelvin Yondan wa Yanga, Ali Mtoni Sonso (sasa marehemu) wa Lipuli na Vicent Philipo kutoka Mbao FC.

Wakiwa huko kabla ya kuanza mashindano Morris akapata majeraha yaliyobainika kuwa yatamuweka nje ya uwanja hadi mwisho wa mashindano. Ili kuziba pengo lake, Amunike akamuita beki wa Azam FC, Mwantika.

Mwantika akaingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kucheza kila mechi hadi safari ya Stars ilipoishia. Na siyo tu alicheza, bali alicheza vizuri japo Stars ilipoteza mechi zote.
Moja ya mechi za kukumbukwa ni dhidi ya Senegal ambayo Mwantika alipambana na mwamuzi katika lile tukio la NO NO NO!

Lakini tofauti na wenzake ambao mafanikio ya mashindano makubwa huwapa dili, Mwantika akakosa dili.

Aliporudi nyumbani kocha wa klabu yake, Aristica Cioaba, hakutaka kumtumia. Mashindano yale yalifanyika Julai 2019 na ilipofika Januari kwenye dirisha dogo Azam FC ikaachana naye.
Lakini kwa kuwa alikuwa na mkataba isingewezekana kumuacha tu hivi hivi, akapelekwa kwa mkopo Lipuli FC ya Iringa. Yeye akakataa na kukaa nyumbani Hapo akawa anajichimbia kaburi lake mwenyewe.

Kuanzia hapo Mwantika akafutika kwenye ramani ya mpira wa miguu Tanzania hadi sasa. Badala ya kufaidika na Afcon, Mwantika akaponzeka nayo hadi leo. 

Hii hali ya ajabu sana. Kwenye kikosi kile cha Stars mwenzake Sonso aliyeitwa akitokea Lipuli alisaini kuitumikia Yanga akiwa kwenye Afcon na hakucheza hata mechi moja. Kuitwa tu Stars ya Afcon kulimuongezea thamani. 

Metacha Mnata ambaye aliitwa Stars ile akitokea Mbao FC alisaini Yanga akiwa kulekule kwenye Afcon kutokana na kupanda kwa thamani yake baada ya kuitwa Stars. Lakini kwa Mwantika ilikuwa tofuati. Thamani yake ilishuka badala ya kupanda kama wenzake.

Leo hii mchezaji kama Mwantika licha ya kujivunia kucheza mashindano makubwa kama Afcon, lakini haimjii picha nzuri akikumbuka kilichompata baada yake. Mwantika, mhitimu wa VETA jijini Mbeya alisaini Azam FC 2012 akitokea Tanzania Prisons.

Aliichezea Azam FC katika zama za mafanikio zaidi katika historia ya klabu hiyo ikishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2023/14, Kombe la Kagame 2015 na 2018 na Kombe la Shirikisho la Azam 2019.