AKILI ZA KIJIWENI: Yakoub aishi kama kipa mkubwa sasa

Muktasari:
- Ulikuwa mchezo mgumu dhidi ya timu nzuri na kubwa Afrika ya Morocco, tena ulichezwa ugenini katika ardhi ya Morocco ambayo inasifika kwa kuwa na mashabiki vichaa wa soka ambao wanajua hasa mbinu za kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu pinzani.
HAPANA shaka watu wengi hawakutegemea kipa Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania kuanza katika mchezo wa Morocco dhidi ya Tanzania juzi usiku wa kuamkia Jumatano.
Ulikuwa mchezo mgumu dhidi ya timu nzuri na kubwa Afrika ya Morocco, tena ulichezwa ugenini katika ardhi ya Morocco ambayo inasifika kwa kuwa na mashabiki vichaa wa soka ambao wanajua hasa mbinu za kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu pinzani.
Hamu ikawa ni kuona kama Yakoub Suleiman ambaye ndio kwanza alikuwa anacheza mechi ya kwanza ya Taifa Stars ataweza kuhimili presha ya Wamorocco wakiwa kwao tena katika mchezo muhimu ambao timu yao ya taifa ilikuwa inahitaji pointi.
Bila shaka benchi la ufundi la Taifa Stars lilimuandaa kisaikolojia Yakoub ambaye alidaka vizuri sana mechi ile na alionyesha hali ya kujiamini licha ya makosa madogo ya hapa na pale ambayo hata makipa wengine wazoefu huwa wanayafanya.
Kitendo cha kuaminiwa na taifa na kupewa mechi muhimu kinaashiria kuwa jamaa ana kitu hivyo anaweza kuwa msaada mkubwa kwa klabu yake na timu ya taifa kwa siku za usoni ikiwa atarekebisha baadhi ya mapungufu aliyoonyesha juzi.
Hata hivyo, ili hilo litimie, Yakoub anapaswa kuanzia sasa ahakikishe anaishi kama kipa mkubwa na wa daraja la juu nchini badala ya kuendelea kujitazama kama kipa mdogo na anayecheza timu ya kawaida ambayo sio miongoni mwa klabu zenye mashabiki wengi nchini.
Anapaswa kufanya mazoezi ya hali ya juu na ya kisasa ndani ya timu yake na pindi anapopata muda binafsi ili kulinda kiwango chake na kumuongezea uimara katika maeneo ambayo ameonyesha udhaifu.
Ajiepushe na ushiriki wa vitendo ambavyo vitaathiri kiwango na afya yake kama vile matumizi ya kupitiliza ya vilevi na ngono zembe, pia azingatie lishe sahihi ili asiathiri uzito na balansi ya mwili wake.
Kingine anachotakiwa kuepuka ni kutokubali kushawishika kupanga matokeo kwa kufanya makosa ya makusudi ili timu yake ipoteze kwani hilo litasababisha asiaminike na mwishowe atapoteza fursa hii muhimu ambayo ameipata.