Aucho apishana na Azam FC

Muktasari:
- Jana, wakati Yanga ikishinda nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, Aucho alilazimika kucheza mechi hiyo kwa dakika 45 kisha akaomba kutoka baada kusikia maumivu na nafasi yake kuchukuliwa na Mudathir Yahya.
Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki tatu baada ya kuumia nyama za paja.
Jana, wakati Yanga ikishinda nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, Aucho alilazimika kucheza mechi hiyo kwa dakika 45 kisha akaomba kutoka baada kusikia maumivu na nafasi yake kuchukuliwa na Mudathir Yahya.
Leo, kiungo huyo amefanyiwa vipimo ambapo imegundulika atakuwa nje kwa wiki tatu, kwa mujibu wa taarifa ambayo iliyotolewa na Klabu ya Yanga.
Kwa Aucho kuwa nje kwa wiki tatu kunamfanya azikose mechi tatu kuanzia mchezo wa Azam utakaopigwa keshokutwa, Aprili 10.
Mechi zingine atakazozikosa ni ile ya ugenini dhidi ya Fountain Gate Aprili 20 na ya nyumbani Yanga itakapoikaribisha Namungo ya Lindi, Mei 13.
Hata hivyo, Yanga ina watu ambao wanaweza kuziba nafasi ya Mganda huyo kwani italazimika kuwatumia Mudathir Yahya, Duke Abuya, Jonas Mkude au Aziz Adambwile.