Prime
Fei Toto milionea… Simba, Yanga zapishana na mabegi ya fedha

Muktasari:
- Azam, imekumbana na kigingi kizito baada ya kiungo huyo, kugoma kuongeza mkataba, akiwaambia mabosi wake ana kiu ya kwenda nje ya nchi kujaribu maisha yake.
VITA mpya kwa Simba na Yanga ni namna zinavyopambana kuonyeshana jeuri ya fedha, kumshawishi kiungo wa Azam Feisal Salum ‘Fei toto’, zikimtengea mamilioni ya kufuru kwa ofa tofauti, pia ipo klabu moja ya Sauzi.
AZAM TISHIO
Tuanze na klabu yake kwanza, Fei Toto mkataba wake na Azam, umebakiza mwaka mmoja na miezi kadhaa na msimu huu utakapomalizika, atakuwa amebakiza mwaka mmoja kamili lakini matajiri hao wa Chamazi kwa muda mrefu, wamekuwa wakimshawishi kuongeza mkataba mpya.
Azam, imekumbana na kigingi kizito baada ya kiungo huyo, kugoma kuongeza mkataba, akiwaambia mabosi wake ana kiu ya kwenda nje ya nchi kujaribu maisha yake.
Hata hivyo, mbali na Fei Toto kutoa sababu hiyo, Mwanaspoti linafahamu kiungo huyo hana shida na namna anavyohudumiwa kifedha na matajiri hao, lakini changamoto kubwa ni ubora wa kikosi chao kiushindani, akiona kama anachelewa kuwa mchezaji mkubwa zaidi.

Azam imemwekea ofa nzito Fei Toto, yenye thamani ya zaidi ya Sh900 milioni, ikiwemo nyumba, gari ya kisasa zaidi tofauti ile Toyota Harrier aliyopewa wakati anasaini mkataba wa sasa lakini zaidi ni kuboresha kwa masilahi yake makubwa.
Matajiri hao, sio tu wanataka kumbakisha Fei Toto, lakini namba zake zikiwashawishi na licha ya kukosa kiatu cha ufungaji bora kwenye ligi msimu uliopita, akaibuka kuwa mfungaji bora ndani ya klabu yake, akiwa na mabao 19 akizidiwa mabao mawili na mfungaji bora kwenye ligi kiungo wa Yanga Stephanie Aziz KI.
Msimu huu, bado Fei Toto ameendeleza ubora wake, akihusika kwenye mabao 17, akitengeneza asisti 13, ambazo ni kinara kwenye ligi, pia akifunga mabao manne akiwa amebakiza mechi nne kumaliza msimu.

OFA YA SIMBA
Simba inamtaka Fei Toto na ile kauli ya kocha wao Fadlu Davids alipozungumza mara baada ya mchezo wa Robo Fainali ya pili dhidi ya Al Masry, aliposhindwa kuficha siri ya kambi, akifichua klabu hiyo ipo kwenye mawindo ya kuwania saini ya kiungo namba 10 bora Tanzania, ambaye watu wa soka fasta tu wamemgeukia kwa Mzanzibar huyo.
Wekundu hao kwenye hesabu zao hadi sasa, ingawa hawajaifuata rasmi Azam lakini imempa ofa kiungo huyo ya Sh600 milioni na mshahara mkubwa wa kiasi kisichopungua Sh30 milioni.
Simba pia inajipanga kuishawishi Azam, kuwapa wachezaji wawili ndani ya dili hilo wakiwemo winga mmoja na kiungo wa kati mmoja wote wazawa ukiweka mbali na fedha za kununua mkataba wake lakini wekundu hao wanaona uzito kutoa kiasi cha Sh1 bilioni kumaliza dili hilo.
Wekundu hao wanatafuta saini ya Fei Toto, ikiwa ni kutamani kiungo namba 10 bora zaidi, ikiona kama staa wao msimu huu Jean Charles Ahoua licha ya kuongoza kwa kufunga mabao kwenye ligi na hata klabuni kwake akiwa na mabao 12, bado hawapi kitu kikubwa wanachotamani hasa kwenye mechi kubwa.

YANGA NAO VIPI
Yanga ambao walimuuza kwa nguvu Fei Toto Azam, nao wamemaliza mgogoro kiume kati yao na kijana wao huyo, kisha hapohapo wakampa ofay a kufuru kiungo huyo ili arejee klabu kwake kuendeleza pale alipoishia.
Yanga imemwambia Fei Toto, atakapokubali kurejea, hatarudi kinyonge, kwani itamkabidhi fedha za kufuru ikimuwekea ofa ya sh 800 milioni, ikimwambia pia itampa mshahara anaoutaka wa sh 40 milioni, ambao Azam pia inataka kumpa atakapokubali kusaini mkataba mpya.
Azam kwasasa inamlipa kiasi cha Sh23.5 milioni na ukiondoa kodi zote kwenye akaunti yake inaingia Sh15 milioni kama mshahara, mkataba huo ukiwa na thamani ya Sh390 milioni kama ada ya usajili.
Mbali na ofa hiyo Yanga pia imemtaka Fei Toto kuchagua kujengewa nyumba anapopataka lakini pia atapewa gari ya kifahari kwenye dili hilo, huku wakimwambia kuhusu kumalizana na Azam awaachie wao wanajua wapi watamalizana na mabosi wa timu yake.
Yanga inarejea kwa Fei Toto baada ya kupata uhakika wa kumuuza kiungo wao Stephanie Aziz KI, anayetakiwa na FAR Rabat, pia Raja Athletic na Wydad Athletic nazo zikiendelea kupigania saini hiyo, klabu zote hizo kutoka Morocco.
Hesabu zingine ni Yanga pia ina uhakika wa kutumia fedha ikiwa pia imepata uhakika wa kuvuna fedha nyingi kwenye hesabu za kumuuza mshambuliaji wao Clement Mzize.
Vinara hao wa ligi, wanataka Fei Toto kuziba pengo la Aziz KI kwenye kikosi hicho kuungana na mastaa wengine

KAIZER CHIEFS WAMO
Klabu pekee iliyowasilisha ofa rasmi Azam ya kumtaka Fei Toto ni Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na kiungo huyo ndiye anayetamani kwenda kuungana na kocha wake wa zamani Nasreddine Nabi, ambaye waliwahi kufanya kazi wote wakiwa Yanga.
Fei Toto ana mahaba makubwa na Nabi na anataka kwenda kuungana na kocha huyo Mtunisia lakini Mwanaspoti linafahamu wazi Kaizer maarufu kwa jina la Amakhosi, ndiyo klabu pekee iliyothubutu kukaa mezani na Azam kuomba kuuziwa kiungo huyo.
Kwenye ofa ya Amakhosi, imeweka dau mpaka kiasi cha zaidi ya Dola 300000 (Sh804 milioni) kununua mkataba wake pale Chamazi lakini kiasi hicho bado kimekataliwa.

KITANZI HIKI
Mkataba wa Fei Toto na Azam, unaweka wazi kwamba kama kiungo huyo anataka kuondoka klabuni hapo, anatakiwa kutoa kiasi cha Dola 500,000 (Sh1.3 Bilioni) na Amakhosi na Simba zimekuwa zikikimbia kutoa fedha hiyo kwa matajiri hao wa Chamazi.
AKILI YA YANGA
Yanga akili yao kubwa sana wakati wanamuuza Fei Toto Azam, waliweka makubaliano rasmi na klabu hiyo kwamba endapo kiungo huyo atauzwa kwa timu yoyote ndani ya Tanzania, basi kwenye mauzo hayo mabingwa hao wa soka nchini, watatakiwa kupata kiasi kisichopungua bilioni moja, hatua ambayo inaifanya Azam kutakiwa kufanya biashara itakayohusisha fedha nyingi zaidi ya hizo ili kuona faida ya kuwa na kiungo huyo.
Azam kama itamuuza nje ya Tanzania kiungo huyo, kipengele hicho hakitafanya kazi lakini bado Yanga itapata fedha zake kwani kuna mgao wa asilimia itaupata kwenye dau la mauzo hayo.
Hata hivyo, kipengele hicho kinawapa urahisi Yanga, kwamba kama wao watahitaji kumnunua Fei Toto, watakwepa kutumikia kifungu hicho lakini kama watamuhitaji sasa watahitajika kumpa kiungo huyo kiasi cha Dola 500000 (Sh1.3 bilioni) ili kumpata kiungo huyo fundi.

FEI AGOMA
Kama kuna kitu Fei Toto amegoma, basi ni kushawishiwa kuondoka Azam kwa vurugu na amezigomea klabu hizo, kuanzisha vurugu ya kutaka kuondoka kwenye klabu yake ya sasa akilinda heshima yake huku akizitega timu hizo kuhakikisha wao wenyewe kwenda kumalizana na matajiri hao.