DAKIKA ZA JIOOONI: Tabora United inasaka ufalme kimyakimya

Muktasari:
- Tabora ilipanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 ikitumia jina la Kitayosce kabla ya kubadilisha na kuwa jina la sasa na haikuwa na wakati mzuri hata kidogo.
KATI ya timu ambazo unaweza kusema zinakuja kwa kasi lakini kimyakimya ni Tabora United. Inashiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili sasa.
Tabora ilipanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 ikitumia jina la Kitayosce kabla ya kubadilisha na kuwa jina la sasa na haikuwa na wakati mzuri hata kidogo.
Lakini ikarudi vyumbani na kujitafuta upya. Katika kipindi cha miezi takribani sita sasa kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ndani ya kikosi hicho ndani na nje ya uwanja kuona namna wanaweza kujitengenezea nafasi mbele ya miamba waliyoikuta kwenye ligi.
Ni katika muendelezo huo pia katika baadhi ya mechi wamekuwa na matokeo ya kushtua ikiwemo kile kipigo walichoiangushia Yanga Jijini Dar es Salaam.

Turufu yao ya kuwekeza kwa wachezaji wakongwe imechangia kuwaweka kwenye tano za juu walipo sasa. Ni timu ambayo kimahesabu ukilinganisha na rekodi za ligi za miaka ya hivi karibuni wameshajinasua kwenye kushuka daraja kwani wana zaidi ya pointi 31.
Katika msimu wao kwanza, ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 27, baada ya kucheza michezo 30, ikishinda mitano, sare 12 na kupoteza 13, hali iliyoifanya kucheza 'Play-Off' dhidi ya maafande wa JKT Tanzania iliyomaliza ya 13 na pointi zake 32.
Mchezo wa kwanza wa 'Play-Off', uliopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora na timu hiyo ilichapwa mabao 4-0, Juni 4, 2024, matokeo hayo yakawafanya kumweka pembeni Kocha Mrundi, Masoud Djuma, kikosi kikakabidhiwa kwa Bernard Fabiano ambaye alianza na mchezo wa marudiano Juni 8, 2024, pale Meja Jenerali Isamuhyo, akaambulia suluhu, hivyo JKT Tanzania kubakia Ligi Kuu.

Baada ya hapo, Tabora ikapata nafasi ya kujitetea tena mbele ya Biashara Utd ya Ligi ya Championship kusaka nafasi ya kubaki Ligi Kuu na mechi ya kwanza ilichapwa bao 1-0, ikichezwa Juni 12, 2024 kwenye Uwanja wa Karume, mjini Musoma Mara.
Mchezo wa marudiano uliopigwa Juni 16, 2024 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, wenyeji walipindua meza na kushinda kwa mabao 2-0, yote yakifungwa na Patrick Lembo raia wa Angola, hivyo kubaki Ligi Kuu kwa jumla ya mabao 2-1.
MWANZO MPYA
Kwa sasa Tabora iliyopo nafasi ya tano na pointi 37, baada ya kucheza michezo 26, ikishinda 10, sare saba na kupoteza tisa, huu ni msimu wake bora katika Ligi Kuu Bara zaidi tofauti na uliopita, ilipokuwa inapambana na janga la kutoshuka daraja.
Msimu huu imepanda kiwango kwani hadi sasa zikiwa zimebaki mechi nne, imeongeza pointi 10 kutoka ilizomaliza nazo msimu uliopita, pia ikipanda nafasi tisa kutoka 14 hadi tano.
Hata hivyo, inahitaji kukaza ili kutoshuka zaidi ya hapo ili kuwa salama zaidi kutokana na timu iliyopo kwenye mstari wa kucheza play off kuwa na uwezo wa kuzifikia pointi zao.

Kitendo cha kusuasua msimu wake wa kwanza hadi kufikia hatua ya kucheza play off, kikawafanya viongozi kujipanga vyema msimu wa pili na kufanya usajili wa wachezaji kadhaa wazoefu akiwemo Heritier Makambo, Yacouba Sogne na Offen Chikola waliokuja kuungana na Andy Bikoko, Nelson Munganga na wengineo kuipambania timu hiyo.
Licha ya kufundishwa na makocha watatu tofauti, ila kikosi hiki kimeendelea kuonyesha ushindani, baada ya kuanza msimu na Mkenya Francis Kimanzi, akafuatia Mkongomani Anicet Kiazayidi, kisha Mzimbabwe Genesis 'Kaka' Mangombe.
Kimanzi aliyejiunga na Tabora, Julai 31, 2024 kabla ya kuondolewa Oktoba 21, 2024 kutokana na kilichoelezwa timu kuyumba, aliiongoza timu hiyo katika michezo minane ya Ligi Kuu ikishinda michezo miwili, sare miwili na kupoteza minne.
Baada ya hapo, Novemba 2, 2024, uongozi wa timu hiyo ukamtangaza, Mkongomani Anicet Kiazayidi aliyewahi kuzifundisha AS Vita, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union zote za kwao DR Congo.

Anicet tangu ajiunge na timu hiyo, aliiongoza Tabora katika michezo 14 ya Ligi Kuu, akishinda saba, sare mitano na kuchapwa miwili.
Hata hivyo, licha ya takwimu nzuri akiwa na Tabora, lakini Anicet aliondoka Machi 28, 2025, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Kocha Mzimbabwe, Genesis 'Kaka' Mangombe aliyewahi kuzifundisha Dynamos FC na Yadah Stars FC za Zimbabwe.
Tangu ateuliwe Mangombe, hajashinda mechi yoyote kati ya nne hadi sasa, akianzia hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA) na kuchapwa na Kagera Sugar kwa penalti 5-4, baada ya sare ya 1-1.
Baada ya hapo, Mangombe akaiongoza timu hiyo katika michezo mitatu ya Ligi Kuu na yote akachapwa pia dhidi ya Yanga 3-0, nyumbani Aprili 2, kisha ugenini kwa bao 1-0 mbele ya Pamba Jiji, Aprili 5 na Mashujaa 3-0, ugenini Aprili 10.
Kocha huyo bado ana nafasi ya kujitafakari kuirudisha Tabora Utd katika ushindani kupitia mechi nne zilizobaki dhidi ya Singida Black Stars (ugenini), KMC (nyumbani), Azam (ugenini) na Coastal Union (ugenini).

WANAOIBEBA TIMU
Nyota anayeibeba zaidi timu hiyo ni, Offen Chikola anayeongoza kwa mabao, akiifungia saba hadi sasa, ukiwa ni msimu wake wa kwanza na kikosi hicho tangu ajiunge nacho akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja ikishiriki Ligi ya Championship.
Mwingine ni Mkongomani Heritier Makambo mwenye mabao matano hadi sasa ya Ligi Kuu Bara, aliyejiunga na timu hiyo msimu huu pia akitokea Al Murooj SC ya Libya, huku akiwa ni mshambuliaji mzoefu baada ya kuwachezea mabingwa watetezi Yanga.
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo na michezo iliyobaki, Kocha Mkuu wa Tabora United, Mzimbabwe Genesis 'Kaka' Mangombe alisema licha ya muda wake mfupi aliokuwa nao, ila atapambania kuboresha zaidi kiwango cha wachezaji wa kikosi hicho.
"Malengo yetu ni kumaliza nafasi tano za juu msimu huu, naamini hilo linawezekana ingawa tunapaswa kupambana kwa sababu ya ushindani uliopo, itachukua muda kidogo wachezaji kunizoea, hivyo sitobadilisha mambo kwa haraka," alisema Mangombe.
Mechi zijazo
Apr 19, 2025
v Singida BS (ugenini)
Mei 14, 2025
v KMC (nyumbani)
Mei 21, 2025
v Azam (ugenini)
Mei 25, 2025
v Coastal Union (ugenini)
2017 Mwaka iliyoanzishwa Tabora Utd ikitumia jina la Kitayosce, mjini Moshi kabla ya kuhamia Tabora
60 Pointi ilizoipandisha daraja Tabora Utd baada ya kuilaza African Sports 3-0 mnamo Mei 13, 2023.
37 Pointi ilizonazo Tabora kwa sasa katika Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 16 na kushinda 10.