Prime
Safari ya wazee wa kimataifa CAFCL, CAFCC

Muktasari:
- Taifa la Afrika Kusini linajivunia kubaki na wawakilishi watatu, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates waliopo Ligi ya Mabingwa na Stellebosch wanaocheza Kombe la Shirikisho.
WIKIENDI hii inaweza kutoa picha ya timu zipi zitacheza fainali ya michuano ya CAF msimu huu, upande wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho huku kukiwa na wababe nane wamesalia, wanne kila upande.
Taifa la Afrika Kusini linajivunia kubaki na wawakilishi watatu, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates waliopo Ligi ya Mabingwa na Stellebosch wanaocheza Kombe la Shirikisho.
Misri kuna Al Ahly na Pyramids, zote zinashiriki Ligi ya Mabingwa. Mataifa mengine yenye timu mojamoja ni Tanzania (Simba), Morocco (RS Berkane) na Algeria (CS Constantine).
Simba itacheza nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini. Mchezo wa kwanza utafanyika Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, kisha marudiano ni Aprili 27, kule Afrika Kusini.
Kwa sasa Simba wanausaka ufalme wa Afrika kwa kubeba ubingwa ambao utazidi kuwapandisha viwango vya CAF kwani hivi sasa inashika nafasi ya nne baada ya kutinga nusu fainali.
Katika kuusaka ufalme huo, Simba hii ni mara ya kwanza inacheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, michuano ambayo ilianzishwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa michuano ya Kombe la Washindi na Kombe la CAF.
Mafanikio hayo ya Simba yalisubiriwa kwa muda mrefu kwani kwa misimu sita nyuma iliishia robo fainali katika michuano ya CAF, hivyo msimu huu kuvuka hadi nusu fainali, imefungua ukurasa mpya kwao.
“Majukumu yote huwa mabegani mwangu, hilo halina shaka. Wachezaji nawaachia wafanye kazi yao na mimi nabeba presha yote mwenyewe. Nitaendelea kufanya hivyo bila kujali matokeo. Huwezi kujiunga na klabu kubwa kama Simba bila kuelewa uzito wa majukumu yake.” Hayo ni maneno ya Kocha wa Simba, Fadlu Davids, siku moja kabla ya kurudiana na Al Masry katika mechi ya robo fainali ambayo Simba ilishinda kwa penalti 4-1 na kufuzu nusu fainali.
Baada ya kufuzu, Fadlu amewapongeza wachezaji sambamba na wasaidizi wake akiwemo kocha wa makipa, Darian Wilken ambaye alionekana kutoa maelekezo ya kiufundi zaidi kwa Kipa Moussa Camara ambaye alikwenda kupangua penalti mbili kati ya tatu alizopigiwa.
Simba katika mashindano ya Kombe la Shirikisho tangu mwaka 2004, huu ni msimu wa saba inashiriki huku mara sita zilizopita hatua kubwa zaidi iliyopiga ilikuwa 2021-2022 ilipoishia robo fainali na kuondolewa kwa penalti 4-3 dhidi ya Orlando Pirates baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1. Simba ilishinda nyumbani 1-0, ikaenda ugenini kufungwa 1-0.
Mbali na msimu huo, mwaka 2007 iliishia hatua ya awali, 2010 raundi ya pili, 2011 mtoano, 2012 hatua ya pili na 2018 hatua ya kwanza.
Pia itakumbukwa mwaka 1993, Simba ilicheza fainali ya Kombe la CAF ambalo baadaye kwa muunganiko wa Kombe la Washindi, ndiyo ikazaliwa Kombe la Shirikisho. Fainali hiyo ilipoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 2-0. Ugenini ilitoka 0-0, nyumbani ikapokea kipigo cha 2-0. Katika michuano hiyo pia mwaka 1997 ikashiriki na kuishia hatua ya kwanza.

RS BERKANE
Wanatajwa kuwa ndiyo wenye nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho msimu huu, hiyo inatokana na uimara ilionao kuanzia kwenye ushambuliaji na ulinzi.
Berkane iliyoanzia hatua ya pili katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo Simba, hadi inafuzu nusu fainali imecheza mechi 10, imeshinda tisa na sare moja, haijapoteza huku ikifunga mabao 21 na kuruhusu moja pekee. Rekodi hizo ni bora zaidi ya timu zote zinazoshiriki Kombe la Shirikisho msimu huu.
Katika ushiriki wao Kombe la Shirikisho Afrika, huu ni msimu wa tisa huku ikibeba ubingwa mara mbili, 2020 na 2022, pia msimu uliopita 2024 ilipoteza mechi ya fainali kama ilivyokuwa 2019.
Kwa timu nne zilizobaki kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Berkane kutoka Morocco ndiyo yenye takwimu bora zaidi kuanzia uchezaji msimu huu pamoja na ushiriki katika mashindano hayo.

CS CONSTANTINE
Licha ya ukongwe ilionao timu hii kutoka Algeria, lakini unaweza kusema ni wageni kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushiriki mara tatu pekee.
CS Constantine iliyoanzishwa mwaka 1898, ina miaka 127 lakini huu ni msimu wao bora zaidi kwani mara zote iliposhiriki Kombe la Shirikisho imeishia raundi ya pili mwaka 2014 na 2016.
Kwa ujumla, timu hiyo imeshiriki mara tano michuano ya CAF, mbili Ligi ya Mabingwa, mwaka 1998 iliishia raundi ya kwanza na 2018-19 ikacheza robo fainali, hivyo kufuzu kwao nusu fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu, ni mafanikio makubwa zaidi.

STELLENBOSCH
Imeanzishwa Agosti 3, 2016 ikiwa na miaka minane tu ya uhai wao. Vijana hao wageni wa michuano ya kimataifa wakishiriki kwa mara ya kwanza, wanatokea Afrika Kusini.
Hawajafika hapo kwa bahati mbaya kwani walichokifanya hatua ya robo fainali, kimewashangaza wengi kwani imewatoa mabingwa watetezi, Zamalek kwa kuifunga bao 1-0 tena ardhi ya ugenini nchini Misri baada ya nyumbani kukaza msuli matokeo yakawa 0-0.
Inakwenda kukutana na Simba ambayo wakati Stellenbosch inaanzishwa, miaka miwili mbele Simba ikaweka mizizi kwenye michuano ya CAF ikicheza robo fainali sita ndani ya misimu saba.

MAMELODI
Ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa, unaonyesha ukongwe na uzoefu ilionao. Kumbuka timu hiyo ina rekodi ya kupata ushindi mnono zaidi katika michuano hiyo iliposhinda kwa jumla ya mabao 16-1 dhidi ya Cote Dor FC ya Seychelles. Nyumbani iliwachapa 11-1 katika hatua ya kwanza msimu wa 2019-20.
Tangu mwaka 1999 ilipoanza kuitwa Ligi ya Mabingwa, Mamelodi imeshiriki mara 16, huku moja ikiwa mwaka 1994 wakati michuano hiyo ikijulikana kama African Cup of Champions Clubs.
Misimu yao kumi iliyopita katika Ligi ya Mabingwa, imebeba taji moja mwaka 2016, huku mara tatu ikiishia nusu fainali ambapo ni 2018-19, 2022-23 na 2023-24 kabla ya msimu huu kufika tena hapo. Sasa Mamelodi wanaisaka fainali ya tatu baada ya 2001 kupoteza na 2016 kuwa mabingwa.

AL AHLY
Mabingwa wa kihistoria kunako Ligi ya Mabingwa wakiwa wamebeba taji hilo mara 12, pia ndio mabingwa watetezi.
Ubabe wao umejidhihirisha zaidi katika misimu mitano iliyopita ikibeba ubingwa mara nne ukiachana na huu ambao bado inaendelea kupambana. Katika kipindi hicho, imechukua ubingwa msimu wa 2019-20, 2020-21, 2022-23 na 2023-24.

ORLANDO
Mara 10 za kushiriki kwao Ligi ya Mabingwa tangu 1997 hadi sasa, hawajashinda ubingwa zaidi ya kushika nafasi ya pili mwaka 2013, lakini ilichukua taji mwaka 1995 wakati ikiitwa African Cup of Champions Clubs. Katika misimu sita ya mwisho kushiriki imekuwa haitoboi zaidi ya kuishia mtoano.

PYRAMIDS
Imeanzishwa mwaka 2008, ni timu ya pili kwa uchanga kwenye mashindano ya CAF kati ya zile zilizobaki msimu huu baada ya Stellebosch.
Chama hilo analolitumikia Fiston Mayele aliyewahi kucheza Yanga, lilikuwa likisota zaidi katika Kombe la Shirikisho lilipoanza kushiriki msimu wa 2019-20 hadi 2022-23 ikiwa mfululizo, kisha misimu miwili sasa ipo Ligi ya Mabingwa kuanzia uliopita 2023-24 na huu 2024-25. Bado haijashinda ubingwa.