Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aziz Ki afichua kinachomkwamisha Yanga

AZIZ KI Pict

Muktasari:

  • Kiungo huyo ambaye msimu uliopita alimaliza kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara akifunga 21 na asisti nane, msimu huu hadi sasa Yanga ikiwa imecheza mechi 23 na kubaki saba, amehusika kwenye mabao 14 akifunga saba na asisti saba.

STEPHANE Aziz Ki wa msimu uliopita, huwezi kumlinganisha na wa msimu huu, ukiangalia namba zake katika Ligi Kuu Bara zimeshuka sana huku mwenyewe akiweka wazi nini sababu ya yote hayo.

Kiungo huyo ambaye msimu uliopita alimaliza kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara akifunga 21 na asisti nane, msimu huu hadi sasa Yanga ikiwa imecheza mechi 23 na kubaki saba, amehusika kwenye mabao 14 akifunga saba na asisti saba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz Ki amekiri msimu huu haujawa mzuri kwake kama uliopita kutokana mambo makubwa mawili.

Amesema rekodi zake hazijashuka Yanga tu, hata kwenye timu ya Taifa ya Burkina Faso, na yote hayo ni kutokana na nguvu kubwa ambayo aliitumia msimu uliopita. 

“Nakiri msimu huu sijafanya mambo makubwa sana, hili limetokana na uchovu wa msimu uliopita na nilipambana sana kuweka sawa malengo ya klabu.

“Sio Yanga tu, pia hata timu ya Taifa langu Burkina Faso, nako sikuwa na muendelezo mzuri, lakini sasa akili yangu imetulia na inarudi uwanjani.

“Bahati mbaya nilipata maumivu ya mgongo, lakini nitakapokuwa sawa ninataka kuanzia hapa kwenye klabu yangu mpaka timu ya Taifa kufanya mambo makubwa.

“Najua ambacho watu wanasema ninapokuwa sijafanya mambo makubwa, na ni kwa sababu wanatarajia vingi kutoka kwangu, hivyo nitahakikisha narudisha kiwango wanachotaka mashabiki,” amesema Aziz Ki ambaye alitua Yanga Julai 15, 2022 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Wakati Aziz Ki anatua Yanga, kikosi hicho kilikuwa kinafundishwa na Kocha Nasreddine Nabi na msimu huo 2022-2023 alifunga mabao tisa. Huu ukiwa ni msimu wa tatu Ligi Kuu Bara, amefunga jumla ya mabao 37.


KUHUSU MAKOCHA

Msimu uliopita wakati anakuwa mfungaji bora, alifundishwa na Gamondi pekee wakati msimu huu tayari amefundishwa na makocha watatu akianza Gamondi, Sead Ramovic na sasa Miloud Hamdi.

Aziz Ki amesema ishu hiyo ya kubadilishwa makocha nayo imechangia kutokuwa na mwendelezo mzuri.

“Sababu nyingine iliyonitatiza ni mabadiliko ya makocha Yanga na yalihitaji ujasiri kwetu kama wachezaji kubadilika kwa haraka, pia majeraha madogo madogo na vyote hivi viliondoa utulivu wa kufanya muendelezo wa kiwango changu,” alisema.

Kati ya mechi 23 za Yanga msimu huu, Aziz Ki amecheza 22 kwa dakika 1528 chini ya makocha watatu, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Miloud Hamid.

Kwa Gamondi, Aziz Ki amecheza mechi 12 na kufunga bao moja la penati dhidi ya Pamba Jiji.

Chini ya Ramovic ambaye alitua Desemba 24, 2025, alicheza mechi sita na kufunga bao moja la penati dhidi ya Dodoma Jiji.

Kwa upande wa Kocha Hamdi ambaye alitua Yanga Februari 14, 2025, amecheza mechi nne na kufunga mabao matano ikiwemo hat trick moja dhidi ya KMC.


REKODI ZAKE

Katika kipindi chote ambacho ametumikia kikosi hicho, amekuwa miongoni mwa viungo muhimu na muda mwingi amepata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Ndani ya misimu mitatu, Aziz Ki amefunga jumla ya mabao 37, huku rekodi zake zikiwa na historia ya kupanda na kushuka.

Msimu wa kwanza alifunga mabao tisa, wa pili akawa mfungaji bora akifisha 21 na huu watatu akiwa nayo saba katika mechi 22 alizocheza.


DUBE AMPUNGUZIA KASI

Msimu uliopita washambuliaji Yanga walikuwa wawili, Clement Mzize na Kennedy Musonda, lakini hawakuwa na makali, ndiyo maana Aziz Ki akawa na jukumu kubwa la kufunga mabao akicheza sana eneo hilo la ushambuliaji. Ilishuhudiwa Musonda akimaliza na mabao matano, huku Mzize akifikisha sita.

Kwa kuona umuhimu wa kuwa na mshambuliaji, Yanga msimu huu ikawasajili Prince Dube na Jean Baleke na Dube ameonekana kufanya vizuri huku Baleke akiondolewa kikosini.

Ujio wa Dube, umemfanya Mzize naye kuwa na makali na kila mmoja amefunga mabao 11 jumla wakifunga 22 kati ya 61.

Wakati washambuliaji hao wakiwaka, Aziz Ki anatumika eneo lake la asili la kiungo mshambuliaji huku majukumu yake makubwa yakiwa ni kutengeneza nafasi kwa Mzize na Dube.

Majukumu hayo yamemfanya hadi sasa kuwa na uwiano sawa wa kuhusika kwenye mabao akitoa asisti saba na kufunga mabao saba.


WASIKIE WATAALAMU

Kiungo wa zamani Yanga, Ally Mayay amesema: “Katika kipindi hiki baada ya mabadiliko ya benchi la ufundi unaona kabisa kama anaaanza kurejea.

“Anachotakiwa kukifanya sasa ni kulinda imani ya kocha, lakini apunguze kujiamini japokuwa ameanza kurejea katika fomu yake.”

Kwa upande wa Sekilojo Chambua aliyewahi kuitumikia Yanga, amesema:

“Mwishoni mwa msimu uliopita alikuwa kwenye kiwango kizuri ukilinganisha na sasa hivi, lakini kiwango chake hakina mwendelezo mzuri, ukizingatia na majeraha aliyopata, utofauti wake mkubwa wa msimu huu na uliopita katika uchezaji sio mkubwa sana ila mabadiliko yapo katika ufungaji pekee.”